The House of Favourite Newspapers

Merciless Billionaires – 46

0

us-dollarsWAKATI dunia nzima ikiamini Inspekta Masala ameuawa na mwili wake kutupwa majini ambako baadaye uliokotwa na kitambulisho chake kuonekana, mpelelezi huyo machachari ameingia Washington DC kwa ndege binafsi akitokea Bangkok, amepokelewa uwanjani na viongozi wa CIA, Interpol na Scotland Yard, yeye mwenyewe haamini kama yuko hai.Je, nini kilitokea mpaka akawa mzima? Nani aliyetupwa majini? SONGA NAYO…

HALIKUWA jambo rahisi sana kwa Inspekta Masala kuamini hasa alipojikuta yupo hai, tena nchini Marekani katika Jiji la Washington, akipokelewa uwanja wa ndege na viongozi wa mashirika makubwa ya upelelezi duniani, wakati alipotekwa na kuchomwa sindano alikuwa nchini Thailand katika Jiji la Bangkok akitokea nyumbani kwa Jen kuchukua picha ambako alimwacha msichana huyo amelala kitandani akiwa maiti.

Alijiuliza maswali mengi bila kupata majibu na alitamani apewe maelezo juu ya kilichotokea mpaka akajikuta Washington, hakuna aliyemjibu badala yake alitakiwa atulie mpaka watakapofika ofisini.

Hicho ndicho kilichotokea, alipotolewa tu uwanjani alipelekwa Hoteli ya Little Flower, kubwa ya nyota tano ambako aliandaliwa vizuri na kuvalishwa nguo mpya safi, kupata chakula cha mchana na baadaye kuchukuliwa kupelekwa ofisi za makao makuu ya CIA.
“Tell me what happened?” (Niambieni kilichotokea!)

“We sent our boys to Bangkok, where a plan was laid down to fake your death!”(Tuliwatuma vijana wetu kuja Bangkok, ambako mpango uliandaliwa kusingizia umekufa!)

Mkurugenzi huyo wa CIA alienda mbele zaidi na kumsimulia Inspekta Masala jinsi maiti ilivyonunuliwa hospitali kuu ya Bangkok, ikakatwa kichwa kwa makusudi, kuvalishwa nguo za Inspekta Masala ambaye alivalishwa nguo nyingine mpya, maiti hiyo ikaenda kutupwa majini, mfukoni ikiwa imewekewa kitambulisho cha Inspekta Masala, lengo likiwa ni kuuaminisha ulimwengu kwamba alikuwa amekufa, gari alilolitumia pia likaachwa ufukweni.

Kilichofuata baada ya hapo ilikuwa ni kusafirishwa haraka kuletwa Washington ambako mpango wa kwenda kuwasaka Dk Viola na nduguye Vanessa ungeandaliwa tena upya, maana kama wasingefanya hivyo, hata Inspekta Masala pia angeuawa kama ilivyotokea kwa wapelelezi wengine na hiyo ingekuwa hasara kubwa sana.

“Bahati nzuri picha zao nimezipata!”
“Hebu tuzione!”
“Hizi hapa.”

Alijibu Inspekta Masala akikabidhi picha mbili.
“Katika hii ya kwanza ni yenyewe kabisa lakini hii ya pili siyo rahisi kuamini, maana hawa ni wazee wawili wa Kijapan!”
“Basi ndiyo wao, yule daktari aliyewafanyia upasuaji ni hatari katika mambo ya upasuaji wa kubadili sura!”

“Ndiyo maana walimuua ili kupoteza ushahidi!”
“Kabisa, hata hivyo wamechelewa, kama wangemuua Jen kabla hajanipa hizi picha ndiyo ingekuwa kazi ngumu zaidi!”
“Kwa hiyo upo tayari kuendelea na kazi?”
“Kabisa.”

“Utaanzia wapi?”
“Kwa sababu hivi sasa kila mtu anaamini mimi ni marehemu, nitafutieni hati nyingine ya kusafiria na ikiwezekana kazi tofauti ili niweze kuzunguka duniani nikiwasaka!”
“Hilo litafanyika na kwa ushauri wangu nafikiri upate kitambulisho cha Shirika la Mazingira Duniani, ili uwe unazunguka kila sehemu kama mtaalam wa mazingira!”
“Sawa kabisa, jina pia libadilishwe!”

“Nadhani uitwe Profesa Abdulkarim Rahim au unaonaje?” aliongea Mkurugenzi Msaidizi wa CIA, John Captain.
“Ha! Ha! Haa!” Inspekta Masala akacheka.

“Nafikiri linafaa.” Mtu mwingine akaongezea.
Haikuwa kazi ngumu hata kidogo kwa CIA kukamilisha zoezi la kumpatia Inspekta Masala hati ya kusafiria na vitambulisho vyenye jina la Profesa Abdulkarim Rahim, kila kitu kilipokamilika, safari yake ya kwanza akiwa mtaalam wa mazingira ilimrejesha tena Bangkok mwezi mmoja baadaye, dunia ikiendelea kusikitikia kifo cha kinyama cha Inspekta Masala.

Kazi aliyokuwa anatakiwa kuifanya Bangkok ilikuwa ni moja tu, kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bangkok kuangalia kwenye kamera za uwanja huo katika tarehe ambazo alihisi Dk Viola na nduguye Vanessa waliondoka, ili kujua walipanda ndege ya shirika gani kuelekea wapi. Alipata ushirikiano mkubwa sana kutoka kwa Shirika la Mazingira ya Bangkok ambao walimpokea kama mwenyeji wao, wakampeleka uwanja wa ndege ambako alionyesha kitambulisho chake cha CIA na kuruhusiwa kuzipitia kumbukumbu za kamera za uwanja.

“So they traveled to Dar es Salaam by Thai Air?”(Kwa hiyo walisafiri kwenda Dar es Salaam kwa Shirika la Ndege la Thailand?) alijiuliza mwenyewe akishangaa baada ya kugundua ujanja walioufanya na majina na hati za bandia za kusafiria walizotumia.

Alikiri mwenyewe kwamba wanawake hao walikuwa ni viumbe wenye akili nyingi kuliko wanaume wengi duniani, hivyo kushughulika nao alitakiwa awe ni mtu mwenye akili mara mbili zaidi yao maana kosa kidogo tu lingeweza kusababisha kifo chake! Usalama wake duniani ulitegemea wanawake hao kuendelea kuamini kuwa alikuwa marehemu, vinginevyo wakati wowote ule jina lake lingeweza kubadilika na kujikuta akizikwa.

Hakuwa na sababu yoyote ya kuendelea kubaki Bangkok nchini Thailand, sababu alishaelewa wabaya wake walikuwa wapi, alichokifanya ni kuchukua ndege siku iliyofuata na kuruka hadi Dubai ambako alipumzika kwa saa nne kabla hajaruka tena kuelekea Dar es Salaam ambako alitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, saa kumi na mbili jioni.

“Back home!”(Nimerejea nyumbani!) alijisemea moyoni mwake akiwa amesimama nje ya uwanja huo madereva teksi wakimzonga ili wampe huduma.
“Come! Come brother!”(Njoo! Njoo kaka!) mmoja wa madereva alisema.
“Shilingi ngapi kutoka hapa kwenda katikati ya jiji, tuseme New Africa Hotel?”
“Hamsini tu kaka!”

“Hamsini? Kaka unaniona mtalii?”
“Basi arobaini!”
“Bado nyingi, twende nitakupa thelathini.”
“Utaniongezea tano mdogo wako!”
“Basi twende!”

Inspekta Masala aliingia ndani ya gari na kuketi kiti cha kando ya dereva, safari ikaanza kuelekea katikati ya jiji, mwendo wa kama nusu saa hivi aliingiza mkono wake ndani ya koti na kutoa picha moja ambayo alimwonyesha dereva teksi na kumuuliza kama aliwafahamu watu waliokuwa kwenye picha hiyo.

“Sana tu, hawa si ni mzee Jonathan Magafu na Andrew Kisanji matajiri kinoma, washkaji wamenunua kisiwa halafu wameshusha bonge la kitu, wanatisha, wanavyuma kama serikali halafu ni watu fresh mbaya, wanasaidia sana jamii, wamejenga mashule kibao na wanasaidia yatima na wajane!” dereva alimwaga sifa nyingi.
“Aiseee!”

“Kwani vipi bro umekuja kuwatembelea?”
“Ndiyo.”
“Wewe unawafahamu wale?”
“Rafiki zangu!”

“Unatisha au nikupeleke kisiwani wanakoishi? Nitaacha gari kwenye maegesho halafu tutapanda boti zao!”
“Hapana, nipeleke tu hoteli ya New Africa.”

Moyoni mwake Inspetka Masala alikuwa na furaha mno, kazi yake hatimaye ilikuwa inakaribia kufika mwisho baada ya kusumbuka kwa muda mrefu kuwasaka Dk Viola na Vanessa, sasa alikuwa amewakaribia na kilichobaki ilikuwa ni kuwatia mbaroni, baada ya hapo angechukua likizo ya maisha yake yote apumzike kijijini kwao Bupandwa ambako alikuwa anajua watu walikuwa na huzuni wakiamini alishakufa.

“Siku nikitokea sijui itakuwaje?” aliwaza gari ikizidi kwenda mbele kwa kasi.
Dakika kumi na tano tu iliegeshwa mbele ya jengo la Hoteli ya New Africa, Inspekta Masala akashuka kisha kushusha begi lake ambalo lilipokelewa na mpokea wageni wa hoteli, kabla hajaingia ndani alichomoa noti tatu ya dola kumi kumi na kumkabidhi dereva teksi, alijua akibadilisha zingekuwa zaidi ya shilingi elfu thelathini lakini aliamua kumpa na zawadi kidogo kwani njiani aliongea sana kwa sababu gari yake haikuwa na redio.

“Ahsante sana braza, wewe mtu poa, utafikiri Denzel Washington bwana!” dereva alimmwagia sifa Inspekta Masala sababu ya tipu aliyopewa.

Inspekta aliingia moja kwa moja hadi mapokezi, hapo alipokelewa na kufanya taratibu zote za kuingia hotelini kisha kupelekwa moja kwa moja chumba namba 215, ghorofa ya pili, akamshukuru aliyembebea mzigo kwa dola tano, kisha kufunga mlango na kujitupa kitandani akitafakari kazi iliyokuwa mbele yake.

JE, nini kitaendelea? Atawakamata? Fuatilia siku ya Jumatano katika Gazeti la Championi Jumatano.

Leave A Reply