The House of Favourite Newspapers

TUZIELEWEJE NDOA ZA LULU, TANASHA?

NDOA ni mpango wa Mungu. Ndoa inaleta heshima fulani katika jamii. Unaposikia fulani ni mume au mke wa mtu huwa kuna utofauti na yule mtu ambaye bado hajaingia kwenye ndoa. Japo wanaume huipenda ndoa kama sehemu ya kujitengenezea heshima lakini inaaminika kwamba wanawake ndio ambao huipenda zaidi ndoa. 

 

Wanawake huipenda zaidi ndoa kutokana na wao kujisikia vibaya pale wanapochelewa kuingia na umri ukawa unawatupa mkono. Tofauti na wanaume ambao wao haiwasumbui sana hata wakioa wakati umri umewatupa mkono.

 

Kwa kulitambua hilo, utaona ni jinsi gani wanawake wanakuwa wanatamani zaidi kuingia kwenye ndoa haraka. Kwenye ulimwengu wa mastaa Bongo wapo mastaa ambao wameingia kwenye ndoa na kuachika lakini wapo ambao ndoa zao zimekuwa zikisubiriwa kwa hamu.

 

Miongoni mwa ndoa hizo zinazosubiriwa kwa hamu ni ile ya mpenzi mpya wa mkali wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Tanasha Donna na ile ya muigizaji aliyepitia mapito mazito Bongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’.

TANASHA

Tanasha mwenye maskani yake nchini Kenya, aliingia kwenye uhusiano na Diamond mwishoni mwa mwaka jana, yakasemwa mengi kuhusu kufunga ndoa lakini mpaka sasa hakuna dalili za ndoa.

 

Ndoa ya Tanasha ilikuwa inasubiriwa kwa hamu kutokana na sababu mbili; moja ni kutokana na umaarufu wa Diamond kama ataweza kweli kutulia na kuoa lakini pili ni kutokana na kuwa na rekodi ndefu ya msururu wa warembo ambao amewapitia huku baadhi yao akiwaahidi ndoa na kuwaacha solemba.

 

Diamond akajinasibu kuwa ndoa yake ingefanyika Februari 14, mwaka huu lakini ilipofika siku hiyo ikapigwa kalenda na kusema ameahirisha hadi pale itakapotangazwa tena. Hapo ndipo Wabongo waliokuwa na yao moyoni wanapojiongeza na kuona labda ni changa la macho kama ilivyokuwa kwa mpenzi wake aliyepita, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ ambaye naye aliahidiwa ndoa, akaishia kuzalishwa watoto wawili.

 

Tanasha ana nafasi kubwa ya kumshawishi Diamond kama kweli anaitaka ndoa kwa Diamond. Inawezekana akakutana na ugumu kutokana na ile imani ya baadhi ya mastaa kwamba unapooa unapoteza mashabiki na umaarufu lakini ‘hakuna mkate mgumu mbele ya chai’, tuisubirie.

LULU

Joto la ndoa ya Lulu nalo lilipanda sana mwishoni mwa mwaka jana hususan baada ya mrembo huyo kutoka gerezani alipokuwa anatumikia kifungo cha kuua bila kukusudia. Akavalishwa pete ya uchumba na mchumba wake, watu wakawa wanasubiria ndoa.

 

Wakati inasubiriwa, mambo yakaanza kuzungumzwa mengi kuhusu ndoa hiyo. Kuna ambao walisema itafungwa kwa siri, wengine wakasema itafungwa tu hadharani lakini mpaka sasa bado hatujasikia tarehe rasmi ya ndoa hiyo.

 

Kumekuwa na kimya kirefu huku tukimuona Lulu akifanya mambo mbalimbali katika jamii ikiwemo kuuza mavazi yake na mambo mengine. Suala la ndoa halizungumzwi tena. Kuna wakati iliwahi kuvuma kwamba alifunga ndoa ya siri nje ya nchi lakini hata hivyo wenyewe hawajakubali wala kukanusha.

 

Zilitajwa ishu za vikao vya baadhi ya watu wa karibu wa mumewe mtarajiwa kwamba wameshaanza maandalizi ya ndoa lakini hakuna uthibitisho kuhusu uwepo wa vikao hivyo, vinafanyika wapi na ndoa itakuwa lini.

TUZIELEWEJE?

Ndoa za mastaa hawa zinatajwa kuwa na hadhi kubwa sana endapo zitafungwa kutokana na umaarufu wao lakini tunashindwa kuzielewa ndoa hizi kwamba zipo au hazipo? Kama zipo mbona hatuoni shamrashamra? Nini kimetokea? Tuwasikilizie!

Makala: Erick Evarist

Comments are closed.