The House of Favourite Newspapers

Taifa Stars Yaipiga Uganda, Yatinga Afcon Baada ya Miaka 39 (Picha +Video)

Kikosi cha timu ya Taifa Stars kilichoanza dhidi ya Uganda Uwanja wa Taifa.

TANZANIA imeandika historia mpya katika soka, baada ya kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka 39. Hii ni mara ya pili kwa Stars kushiriki fainali za Afcon, mara ya kwanza ilikuwa ni mwaka 1980, kipindi hicho wazee wa sasa, akina Leodegar Tenga wakiwa wachezaji.

Washambuliaji wa timu ya Taifa Stars John Bocco (kushoto) akishangilia kwa kumvuta Simon Msuva.

Stars imepata nafasi hiyo baada ya kuichapa Uganda bao 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam mbele ya wakubwa wengi wa nchi wakiongozwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Kassim Majaliwa aliyekuwa mgeni rasmi wa mechi hiyo, na mawaziri kibao akiwemo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe.

Kikosi cha timu ya Uganda kilichoanza dhidi ya Taifa Stars.

Bao la kwanza la Taifa Stars katika mchezo huo, lilifungwa na Simon Msuva dakika ya 20, aliyetumia vizuri krosi ya Gadiel Michael ambaye alikuwa amepokea pasi murua kutoka kwa John Bocco.

 

Stars ilipata bao la pili kwa penalti iliyopigwa kiufundi na Erasto Nyoni dakika ya 50, kufuatia Mbwana Samatta kumshikisha mpira Kirizestom Ntambi aliyeunawa ndani ya eneo la hatari na mwamuzi kuamuru penalti. Baada ya penalti kupatikana, John Bocco alichukua mpira kwa ajili ya kupiga, lakini Nyoni akauchukua na kupiga yeye.

Bao la tatu lilifungwa na Aggrey Morris kwa kichwa akitumia vizuri krosi iliyopigwa kiufundi na John Bocco.

 

Uganda ilikuwa imefuzu mchezo huo, lakini ilicheza kwa nguvu na kwa kutafuta matokeo mazuri. Mashabiki walionekana kuzimia, hadi bao la tatu linafungwa, walikuwa wameshazimia wanne. Sasa Stars imefikisha pointi 8 ikipaa hadi nafasi ya pili huku Uganda wakibaki na pointi zao 13 kileleni.

Katika kundi la Stars (L), kila timu ilikuwa na nafasi ya kufuzu kuelekea michezo ya jana, Lesotho ambayo ilikuwa nafasi ya pili, iliilazimisha suluhu Cape

 

Verde iliyokuwa nyumbani, na zote hizo zimetupwa nje.

 

Taifa Stars sasa imekuwa miongoni mwa timu 5 ambazo zimefuzu jana kuungana na timu nyingine 19 ambazo hadi kufikia juzi zilikuwa zimefuzu.

Timu nyingine zilizofuzu jana ni Zimbabwe na DR Congo ya kocha Mwinyi Zahera kutoka Kundi G. DR Congo ilihitaji ushindi nyumbani na iliupata dhidi ya Liberia kwa bao 1-0, huku Zimbabwe ikifuzu kwa kuichapa Congo 2-0 nyumbani katika kundi hilo.

 

Timu nyingine iliyofuzu ni Benin katika Kundi D iliyoichapa Togo 2-1 na kuungana na Algeria iliyokuwa tayari imefuzu, wakati Libya na Afrika Kusini, mmoja amefuzu katika mchezo wa jana usiku wa Kundi E. Afrika Kusini ilihitaji sare ugenini, wakati Libya ilihitaji ushindi.

Uwanja wa Taifa jana ulikuwa umejaa ‘full’ hata kabla ya mechi. Zikiwa zimebaki dakika 15 mpira kuanza, tayari mashabiki walikuwa wakizuiwa kuingia uwanjani huku nje wakiwa wamerundikana kwa wingi. Ndani ya uwanja, kutokana na kukosa viti, mashabiki wengi walikuwa wamekaa kwenye ngazi na nje polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya, na jumla walipiga saba.


Hadi kufikia muda wa mechi, uwanja ulifungwa kutokana na kujaa.

Kikosi cha Taifa Stars kilichoanza kiliwakilishwa na Aishi Manula, Hassan Kessy, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Gadiel Michael, Erasto Nyoni, Mudathir Yahya, Farid Mussa/Himid Mao dk 69, Mbwana Samatta, Simon Msuva/ Thomas Ulimwengu 89 na John Bocco/Fei Toto 80. Uganda; Dennis Onyango, Awany Timothy, Taddeo Lwanga, Emmanuel Okwi/Milton Karisa dk 50, Kirizestom Ntambi, Nico Wadada, Godfrey Walusumbi, Faruku Miya/Lubega Edrisa dk 69, Allan Kyambadde, Patrick Kaddu/ Shabanb Muhhamed 79 na Moses Waisw.

Baada ya Mpira kuisha, kocha Emmanuel Amunike alimwagiwa maji kwa furaha na watu wa benchi la ufundi. Shiza Kichuya alikuwa akicheza ngoma kwa furaha wakati mpira ukielekea mwishoni. Ofisa Habari wa Simba, Haji
Manara alitangaza mpira wa Cape Verde na Lesotho umeisha, hivyo Manula ambaye alikuwa na mpira golini akapiga magoti na kusali kabla ya kuupiga. Kama Lesotho ingeshinda, ushindi wa Stars ungekuwa hauna maana. Ilikuwa ni shangwe kwani Dennis Onyango ambaye ni kipa bora zaidi Afrika, alitunguliwa mabao matatu.


UGANDA WAINGIA KWA STAILI YA AINA YAKE

 

Wakati timu zinaingia uwanjani kupasha, Uganda walianza kuingia wachezaji 10 pekee wa ndani na makipa watatu. Baada ya dakika 5 wakaingia wengine tisa. Waliingia uwanjani kwa staili tofauti wakiwa wamevaa jezi za mechi, wakati Stars waliingia wakiwa wamevaa jezi za mazoezi.

 

STARS YATUMIA STAILI YA SIMBA

 

Taifa Stars waliingia na staili ambayo Simba wamekuwa wakiitumia kwenye mechi za kimataifa. Waliingia kupitia kona ya uwanja upande wa Kaskazini Magharibi sehemu ambayo Simba waliingilia na kuifunga AS Vita 2-1. Lakini pia katika mechi dhidi ya
Yanga, Simba waliingilia upande wa Kusini Magharibi na kushinda 1-0.

 

VURUGU, ASKARI WAPIGA MABOMU YA MACHOZI

 

Upande wa geti la Uhuru linalotokea Uwanja wa Ndani, mashine za kuangalia tiketi zilizidiwa nguvu kutokana na foleni kubwa ya mashabiki, wengi walikuwa wakipanda juu ya uzio na kurukia ndani. Mashabiki wengine walikuwa wakirusha mawe, kuona hivyo polisi walikuja na kuanza kupiga mabomu ya machozi. Mashabiki kadhaa wakiwemo wa kike, walionekana kupata majeraha kutokana na vurugu.

 

Vurugu zilikuwa kubwa mno kutokana na mashabiki wengi kurundikana nje kwa kukosa tiketi. Kuna mashabiki wengi walipakizwa kwenye magari ya polisi na kushikiliwa kutokana na kuruka ukuta. Baadaye askari walilazimika kutumia maji ya kuwasha kwa ajili ya kuwaondoa mashabiki magetini, na hadi kufikia saa 11:00 jioni uwanja ulikuwa umekaribia kujaa wakati kukiwa na rundo la mashabiki nje waliotaka kuingia.

 

TWANGA PEPETA YAWA KIVUTIO…

Bendi ya Twanga Pepeta jana iliwakosha mashabiki Taifa baada ya kuimba nyimbo ikiwataja wachezaji wa Stars, na kila lilipotajwa jina la nahodha Mbwana Samatta mashabiki walishangilia kwa nguvu zaidi.

 

DROO YA MAKUNDI Droo ya makundi inatarajiwa kupangwa Aprili 12, mwaka huu jijini Cairo, Misri, ikiwa ni fainali za kwanza za Afcon kushirikisha timu 24 badala ya 16 kama ilivyokuwa awali.

Comments are closed.