The House of Favourite Newspapers

Jini Mweusi 51

0

Hali ya sintofahamu inazuka jijini Dar es Salaam kufuatia kupotea mfululizo kwa machangudoa katika mazingira ya kutatanisha. Taharuki kubwa inazuka kwani ndani ya kipindi kifupi tu, zaidi ya machangudoa kumi na moja wanapotea na hakuna anayejua walikopotelea.

Jambo hilo linasababisha jeshi la polisi kuingilia kati. Kinachozidi kuzua utata, wote wanapotea katika mazingira yanayofanana. Mwanaume mmoja asiyejulikana, aliyekuwa anatembelea gari la kifahari aina ya Volkswagen, aliyekuwa akienda eneo hilo usiku wa manane ndiye anayehusishwa na wote wanaopotea.

Upande wa pili, kijana aliyekuwa na mwonekano tofauti na binadamu wa kawaida, Dickson Maduhu au Zinja kama wenzake walivyokuwa wakimtania, amejiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Hisia kali za mapenzi zinasababisha kijana huyo aanze kutoka usiku na kwenda kutafuta machangudoa.  Hivyo baadaye anahamishiwa Dar es Salaam.

Mara baada ya kufanikiwa kuwa DCP, Dickson anajikuta akinogewa na penzi la changudoa mmoja aitwaye Pamela, umbo lake, ngozi vinamchanganya na kujikuta akianza kumganda pasipo kujua kwamba ukaribu wake na msichana huyo ungeweza kubadilisha kila kitu.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Magreth hakutaka kukurupuka, alitaka kufanya vitu kimyakimya, yaani kumchunguza rafiki yake mpaka pale ambapo angepata ukweli wa mambo ili ajue ni kitu gani cha kufanya.

Alijipanga, hakutaka kushtukiwa kabisa. Siku iliyofuata ambapo Pamela alirudi nyumbani, alimtembelea na kumchangamkia kama ilivyo siku nyingine, yote hayo aliyafanya kwa sababu alihitaji kufahamu mwanaume aliyekuwa akitembea naye aliishi wapi, kwani hata yeye alikuwa akimhitaji kwa sababu alikuwa bwana wake kitambo.

Alihakikisha hachezi mbali na simu ya Pamela, alijitahidi kufuatilia namna ya kutoa loki za kwenye simu kwa mtindo wa kuzungusha pattern, alipozikariri, kazi ikawa kwake kuifungua na kufanya yake.

Alimvizia Pamela alipokwenda bafuni kuoga ndiyo ukawa muda wake wa kuchukua simu yake kisha kuanza kuiangalia palepale kitandani. Alitoa loki kisha kuanza kuangalia namba zilizoingia jana usiku, muda ule ambao alitakiwa kuondoka nyumbani.

Jina alilokutana nalo lilikuwa Mapesa, akajua kwamba hiyo ndiyo namba ya huyo bwana aliyekuwa na wasiwasi naye. Alichokifanya ni kuchukua simu yake na kuangalia namba, zilikuwa za mtu yuleyule, mwanaume aliyekuwa akilala naye kwa malipo makubwa.

“Ndiye yeye!” alisema Magreth huku akiachia tabasamu pana na la kinafiki.

Huo ndiyo ukawa mwanzo wa kazi yake ya kumtafuta mwanaume huyo. Kitu cha kwanza alichokitaka ni kufahamu mahali alipokuwa akiishi, hilo wala halikuwa tatizo, kwa sababu alikuwa rafiki kipenzi wa Pamela, ndani ya siku chache tu akafahamu mahali alipokuwa akiishi mwanaume huyo, Dickson.

Kilichofuata ni kuanza kumvizia, kila siku usiku alihakikisha anakwenda nyumbani kwa mwanaume huyo, anakaa nje kwa mbali huku akimsubiri aingie nyumbani kwake kwa lengo la kwenda kuzungumza naye lakini kila siku aliambulia patupu, hakuwa akibahatika kuonana na mwanaume huyo, kwani mara nyingi alikuwa akilala hotelini na Pamela, aliporudi ilikuwa ni asubuhi.

Magreth alifuatilia kwa takriban wiki mbili ndipo siku moja akafanikiwa kuliona gari la Dickson likianza kuingia ndani ya jumba hilo la kifahari. Kwa kasi kubwa, Magreth akajitoa kule alipokuwa amejificha na kuanza kupiga hatua za haraka kuelekea lilipokuwa geti la nyumba ile, alitaka kuzungumza na mwanaume huyo.

Alipolifikia gari, kwa haraka akaenda katika mlango wa gari na kuanza kugonga kioo huku akihitaji kufunguliwa.

Dickson aliyekuwa ndani alishtuka, akaanza kujiuliza mtu huyo alikuwa nani mpaka kupata ujasiri wa kutaka kufunguliwa mlango. Kitu cha kwanza alihisi kwamba alikuwa jambazi, alipomwangalia vizuri, alikuwa msichana ambaye wala hakumfahamu vizuri kutokana na mwanga hafifu.

Kabla hajashusha kioo cha gari, akahakikisha anaangalia sehemu nyingine kama kulikuwa na watu wengine ambao alihisi ndiyo waliomtuma msichana huyo, alipoona amani imejaa, akashika bunduki yake kama tahadhari kisha kushusha kioo.

“Nikusaidie nini binti?” aliuliza Dickson, garini mwake hakukuwa na mwanga mkali. Mkono wake wa kushoto ulishikilia bunduki kisiri.

“Umenisahau mpenzi?” aliuliza Magreth, Dickson akashtuka, kwani sauti aliyoisikia haikuwa ngeni, na hata alipomwangalia vizuri msichana huyo, aligundua kwamba alikuwa Magreth.

“Mage…”

“Ndiyo mimi kipenzi. Nimekukumbuka sana,” alisema msichana huyo.

“Umepajuaje hapa?”

“Nani? Mimi? Mbona nimepajua kawaida tu.”

“Mmh!”

“Usijali mpenzi!

Kitendo cha Magreth kupafahamu alipokuwa akiishi lilionekana kuwa kosa kubwa, alijua fika kwamba mwisho wa siku msichana huyo angegundua kwamba yeye alikuwa kamanda mkuu jijini Dar es Salaam.

Alichokifanya ni kumchangamkia kisha kumchukua na kuelekea naye ndani, tena huku akihakikisha anaivaa kofia yake. Magreth alionekana kuwa na furaha mno, kitendo cha kuona kwamba mwanaume huyo amempokea kwa mapenzi motomoto, kilimfurahisha.

Akamchukua na kumpeleka ndani huku akihakikisha gari amelipaki vizuri. Alipofika humo, hakuwasha taa sebuleni, aliunganisha naye mpaka chumbani kisha akamlaza kitandani.

Alichokitaka ni kumuua msichana huyo tu. Alihitaji kuwa na amani, hakuhitaji presha, alijua fika kwamba endapo angemuacha msichana huyo basi kitu ambacho kingefuata ni aibu kubwa.

Magreth angejua kwamba nyumba ile ni ya kamanda wa jeshi la polisi na mwisho wa siku kuwatangazia watu kwamba mtu huyo alikuwa bwana wake. Alipofikiria mambo yote hayo, hakuona sababu ya msichana huyo kuendelea kuwa hai.

Alipofikishwa kitandani na kulazwa chali, alifurahi kwa kuona kwamba hatimaye alifanikiwa kumrudisha bwana wake mikononi mwake. Alijiachia kitandani pale, alijiweka vizuri tayari kwa kumkaribisha Dickson katikati ya miguu yake pasipo kujua kwamba mwanaume huyo alikuwa na vitambaa kadhaa mikononi mwake kwa ajili ya kumziba pumzi na kumuua. Hilo, Magreth hakulitambua kwa sababu ya giza.

Je, nini kitafuatia? Usikose riwaya hii ya kusisimua Alhamisi ijayo kwenye gazeti hilihili.

Leave A Reply