The House of Favourite Newspapers

The Angel of Darkness-18

0

Shambulizi kubwa la kigaidi linatokea kwenye kituo kikubwa cha biashara nchini Kenya, Kikuyu Mall na kusababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Wakenya, Watanzania na watu wengine kutoka mataifa mbalimbali.

Miongoni mwa wahanga wa tukio hilo la kikatili, wamo Watanzania, Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam, mkewe, Asia Mustafa na watoto wao mapacha waliokuwa bado wachanga, Arianna na Brianna.

Kwa bahati mbaya, Ndaki na mkewe wanapoteza maisha katika tukio hilo, maiti zao na za Watanzania wengine zinasafirishwa mpaka nchini Tanzania ambako hatimaye wanazikwa.

Pacha wa kwanza, Arianna anapatikana na kurejeshwa nchini Tanzania ambako anakabidhiwa kwa ndugu zake. Bado haifahamiki pacha mwingine, Brianna yuko wapi na juhudi za kumtafuta zinaendelea.

Upande wa pili, mwanamke mwenye upungufu wa akili, Mashango anamuokota Brianna kwenye shambulizi hilo na baadaye anahamia kwenye kitongoji cha watu maskini, Mathare, pembezoni kidogo mwa Jiji la Nairobi, mahali anakoweka makazi yake.

Maisha yanazidi kusonga mbele huku mtoto huyo japokuwa alikuwa mdogo, akimpa changamoto kubwa za kimaisha Mashango. Baadaye Brianna anaanza masomo na kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele ndivyo maisha ya Mashango yanavyoanza kubadilika.

Anaanza kufanya biashara ya mbogamboga na matunda na kuishi maisha ya kawaida kama binadamu wengine. Hata hivyo bado kuna watu ambao hawaamini kwamba mwanamke huyo amepona, wanamfanyia fitina za hapa na pale na kusababisha akamatwe na mgambo wa Jiji la Nairobi.

Hata hivyo anaonekana hana hatia. Wanamuachia lakini kwa bahati mbaya, wakati akirejea kwenye eneo lake la biashara anapata ajali mbaya ya kugongwa na gari na kupoteza maisha papo hapo.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…Ilikuwa ni ajali mbaya mno, kila mtu aliyeiona alishika kichwa, watu wakaanza kukimbilia kule alipokuwa Mashango, damu zilitapakaa, alirusha miguu yake huku na kule, alihema kwa nguvu, kifua kilipanda juu na kushuka chini, mwili ulichubuka, alipasuka kichwani, kwa mbali ubongo ulianza kutoka utosini mwake, hali iliyomfanya kuonekana kuwa kwenye hali mbaya. Wasamaria wema walijaribu kumsaidia lakini walikuwa wamechelewa, tayari alikuwa amekata roho.

“Ameua!”

“Ameua.”

“Halafu mbona anawasha gari? Mzuieni asiondoke, dereva gani anakosa utu kiasi hicho, huyo anakimbiaa!” alisema mwanaume mmoja kwa sauti ya juu lakini wote walikuwa wameshachelewa, dereva aliyemgonga Mashango alirudisha gari nyuma kwa kasi, akakata kona na kuingia kwenye barabara ya mtaa wa pili kwa kasi kubwa.

Baadhi ya watu wenye magari walioshuhudia tukio hilo walijaribu kumfukuzia na magari yao lakini ilikuwa ni sawa na kazi bure, tayari alishawapotea. Umati mkubwa wa watu ukaanza kumiminika eneo la tukio. Kila aliyemtazama Mashango pale chini alipokuwa ameangukia, damu na ubongo vikiwa vimemwagika kwenye lami, hakurudia kumtazama zaidi ya mara moja.

Ilikuwa ni picha mbaya na ya kutisha mno ambayo hakuna ambaye angependa kuitazama mara mbili. Ilibidi mwanamke mmoja avue khanga yake na kumpa mwanaume aliyeonekana kuwa na roho ngumu, akausogelea mwili wa Mashango na kuufunika.

***

Brianna akiwa na wanafunzi wenzake wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Mathare iliyopo kwenye kitongoji cha watu maskini cha Mathare jijini Nairobi, walikuwa wakirejea shuleni baada ya kumaliza masomo. Wakiwa wanatembea pembezoni kabisa mwa barabara kama walivyofundishwa na walimu wao, walishtushwa na umati mkubwa wa watu uliokuwa umekusanyika mita kadhaa mbele.

“Pale kuna nini?”

“Sijui, labda itakuwa ajali, wajua hii barabara yapita magari yaendayo kwa kasi kama stima,” alijibu mwanafunzi mwingine kwa Kiswahili chenye lafudhi ya nchi hiyo. Harakaharaka wakawa wanakimbia kuelekea eneo hilo ili nao wakajionee kilichotokea.

Tofauti na wenzake, Brianna alijihisi kuwa mzito ghafla, akawa ni kama amepigwa na bumbuwazi fulani ingawa hata mwenyewe hakujua ni kwa nini.

“Brianna twende tukaangalie ajali,” alisema mwanafunzi mwenzake wakiwa tayari wameshamuacha mita kadhaa lakini mwenyewe aliendelea kutembea kwa hatua za taratibu. Kadiri alivyokuwa anakaribia eneo hilo ndivyo mapigo ya moyo wake yalivyokuwa yanazidi kuongezeka, japokuwa alikuwa mdogo sana kiumri, alishajua kwamba kuna kitu hakipo sawa.

Akiwa amekaribia kabisa eneo hilo, alipigwa na butwaa kuona kiatu kilichokuwa kinafanana na cha mama yake, Mashango kikiwa kimeangukia mtaroni huku kikionesha kuwa na damu.

Kwa tahadhari kubwa aliinama pale kwenye mtaro huku akizidi kutetemeka, akakichukua na kukitazama vizuri na kugundua kuwa kilikuwa ni cha mama yake kwani hata siku walipoenda kununua kwenye Soko la Mathare walikuwa pamoja na yeye ndiye aliyemshauri mama yake kununua kiatu hicho.

 Ghafla alikurupuka kutoka pale mtaroni alipokiokota kile kiatu na kuanza kukimbia huku akipiga kelele, akapenya kwenye miguu ya watu wote waliokuwa wamekusanyika na kuuzunguka mwili wa Mashango uliokuwa bado umelala palepale kwenye lami wakisubiri askari wa usalama barabarani.

Katika hali ambayo hakuna aliyetegemea, wote walishtuka kumuona mtoto mwenye umri mdogo, akiwa amevaa nguo za shule akikimbilia pale maiti ilipokuwa imefunikwa, bila woga akaifunua upande wa kichwani na kupiga kelele kwa nguvu, hali iliyozua taharuki kubwa eneo hilo.

“Mamaaa! Jamani mama umeniacha na nani mama’angu?” alisema Brianna kwa sauti ya juu na kuanza kulia kwa uchungu, watu waliokuwa na mioyo myepesi walijikuta nao wakishindwa kujizuia na kuanza kumwaga machozi, hasa walipokuwa wakimtazama jinsi mtoto huyo alivyokuwa anajaribu kumuinua Mashango pale chini alipokuwa amelala na kusababisha shati lake la shule liloane kwa damu.

Ilibidi busara za kiutu uzima zitumike kumtoa mtoto huyo eneo hilo na kuufunika tena mwili wa mama yake, kazi ambayo haikuwa nyepesi kwa jinsi mtoto huyo alivyokuwa analia kwa uchungu. Watu waliacha kuutazama ule mwili na kumgeukia mtoto huyo ambapo hata alipoulizwa wanaishi wapi, alishindwa kujibu zaidi ya kuendelea kulia kwa uchungu huku akilitaja jina la mama yake.

Kwa bahati nzuri, askari wa usalama barabarani waliwasili muda mfupi baadaye na kwa kusaidiana na wasamaria wema, walisaidiana kumbeba Mashango na kumlaza juu ya machela maalum ya polisi, askari hao wakambeba na kumpakiza kwenye gari walilokuja nalo.

“Yupo na mwanaye.”

“Yupo wapi?”

“Yule anayelia sana pale pembeni aliyeshikwa na yule mwanamke.”

“Hebu mleteni,” alisema askari mmoja, ikabidi Brianna ambaye tayari shati lake la shule lilikuwa limelowa damu utadhani na yeye amepata ajali, achukuliwe na kupakizwa kwenye gari la polisi pamoja na mwili wa mama yake, huku akiendelea kulia kwa uchungu.

Haraharaka gari hilo likaondoka na mwili wa Mashango na safari ya kuelekea hospitalini ikaanza ambapo madaktari walithibitisha kwamba ni kweli tayari ameshakata roho.

Ikabidi Brianna achukuliwe mpaka kwenye chumba maalum ambapo askari mmoja mwanamke alianza kumtuliza na kumuuliza maswali mbalimbali, ikiwa ni pamoja na sehemu wanayoishi na kama walikuwa na ndugu yeyote.

Hata hivyo, Brianna alishindwa kujibu chochote zaidi ya kuendelea kulia tu, hali iliyowapa wakati mgumu askari pamoja na madaktari kujua namna ya kumsaidia mtoto huyo kutoa taarifa kwa ndugu na jamaa wa marehemu ili taratibu za mazishi zianze kufanywa.

Leave A Reply