The House of Favourite Newspapers

Kocha wa Liverpool Atoa Hongera Kwa Guardiola

KOCHA wa Liverpool, Jurgen Klopp, amesema kuwa hakika Manchester City walikuwa na msimu mzuri ndiyo maana wametwaa ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu. Manchester City wameutwaa ubingwa huo baada ya kufanikiwa kufikisha pointi 98 na kuwazidi Liverpool kwa pointi moja ambapo wao walipata pointi 97.

 

Kocha wa Liverpool, Juggen Klopp, amesema kuwa lilikuwa pigo kubwa kwake kuukosa ubingwa huo ambao alikuwa ameuwania kwa muda mrefu lakini hana jinsi kwa kuwa kila mmoja ameona jinsi ambavyo wamepambana.

 

Klopp alikuwa na matumaini ya kutwaa ubingwa huo hadi kipindi cha kwanza kinamalizika cha mchezo wake wa mwisho, lakini baada ya City kushinda mabao 4-1 kila kitu kiliharibika.

 

Hata hivyo, kocha huyu raia wa Ujerumani amesema siyo muda wa kulalamika bali ni kupambana na kuhakikisha kuwa msimu ujao timu yake inafanikiwa kuwazuia City kutwaa ubingwa wa tatu mfululizo. Kocha huyo anatafuta ubingwa wa kwanza kwa Liverpool ambao waliutwaa mara ya mwisho mwaka 1990.

 

Akizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari Klopp ambaye alikuwa akishangiliwa na mashabiki wa Liverpool hata baada ya mchezo kumalizika na timu yake kukosa ubingwa, alisema anawapongeza City kwa kutwaa ubingwa huo.

 

Kocha huyo alisema anampongeza Pep Guardiola kwa kutwaa ubingwa huo kwa mara ya pili mfululizo. “Sitaki kukataa, hakika City walikuwa na msimu bora sana na walionyesha kiwango cha hali ya juu kwenye michezo yao yote.

 

“Kwanini usiwapongeze msimu huu tumekosa ubingwa na wamechukua City, hakuna jambo lingine zaidi ya kusema kuwa wamefanya vizuri sana. “Jambo pekee ambalo kila mmoja anatakiwa kufahamu ni kwamba tutakwenda tena msimu ujao kuhakikisha kuwa tunachukua ubingwa huu na kuwazuia City kuutwaa mara ya tatu mfululizo.

Pep Guardiola

“Kuna mmoja amesema kuwa tuliweza kupambana msimu huu na haamini kama msimu ujao tunaweza
kupambana zaidi, lakini nataka kusema kuwa msimu ujao tutakuwa bora zaidi ya msimu huu.

 

“Man City walikuwa vyema sana kifedha, halikuwa jambo rahisi kwa timu nyingine kuwapita kirahisi, lakini tunajiandaa kwa ajili ya msimu ujao na tutakuwa bora zaidi ya msimu huu,” alisema kocha huyo ambaye timu yake iliichapa Wolves mabao 2-0 kwenye mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu England.

 

Kocha huyo ambaye wakati anasaini mkataba kwenye kikosi cha Liver-pool mi-aka mitatu iliyopita alisema kuwa ukifika msimu huu ndiyo mashabiki wamuulize kuhusu ubingwa amesema kuwa wachezaji wake walionyesha kiwango cha juu sana, lakini anafahamu kuwa kuna mambo mengi sana mazuri yanakuja.

 

“Kuna mambo mengi sana yanakuja, ni jambo la kuendelea kupambana kwenye kila mchezo ambao tutacheza, mnatakiwa kukumbuka kuwa tupo kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mwaka wa pili sasa,” alimalizia. Mbali na kukosa ubingwa Liverpool ndiyo timu ambayo imemaliza msimu huu ikiwa imefungwa mabao machache kuliko zote ikiwa imeruhusu mabao 22.

Comments are closed.