The House of Favourite Newspapers

Mwanamke Alivyomfanya Zezeta Kaka Yangu – 32

0

ILIPOISHIA

Tulifika katika geti la yule mwanamke na polisi wakashuka huku wakiwa na silaha zao. Sisi tuliambiwa tusishuke mpaka kwanza polisi wapate uthibitisho kwamba yupo.

Je, watamkuta huyo mwanamke?

SONGA NAYO.

Ngo, ngo, ngo,” ni mlio wa geti wakati polisi mmoja mwenye cheo cha sajenti akigonga geti kubwa jeusi.

Hatukusikia sauti ya mtu yeyote ikiitikia huko ndani ya ua lakini kama ilivyo kawaida yao, tulisikia sauti ya mlio wa viatu ko, ko, ko, ko, ikiashiria kuwa mtu alikuwa akija getini, hii ni kwa sababu sehemu yote ndani ya geti kulikuwa kumesakafiwa.

Kwa kuwa tulikuwa ndani ya gari nilichungulia na kuona kinachoendelea pale getini. Mlango ulifunguliwa kidogo, nikaona sura ya yule msichana wa kazi wa yule mwanamke aliyemfanya kaka yetu zezeta.

Alipowaona askari uso wake ulionekana una wasiwasi na akaachia geti na likafunguka lote tukawa tunaona mpaka ndani.

“Hujambo?” alisalimia yule mkuu wa upelelezi wa polisi wa wilaya (OC CID) akiwa na simu yake ya upepo mkononi.

“Sijambo, shikamoo!”

“Marahaba. Mama yupo?”

“Eeeh yupo… ngoja nikamuangalie.”

“Mbona unatoa majibu mawili? Acha kutetemeka. Sema. Yupo au hayupo?”

“Sijamuona tangu nilipoamka. Inawezekana yupo au katoka.”

“Kwani anapotoka huwa hakuagi?”

“Inategemea, anaweza kuniaga au asiniage.”

“Anakuaga inapotokea nini na huwa hakuagi kikitokea kitu gani?”

“Hata bila kutokea chochote, anaweza kuniaga au asiniage.”

“Oke, twende ndani ukamcheki.”

Kamanda yule na askari wake waliingia ndani ya gari la polisi, ‘difenda,’ nalo liliingizwa. Sisi kwa kuwa tulikuwa kwenye gari dogo, nasi tukafuata kwa nyuma kwa mwendo wa polepole.

Hata kabla mlango haujafunguliwa na yule msichana wake wa kazi, yule mama alifungua mlango huku akiwa ametoa macho, bila shaka alichungulia kwenye dirisha na akaona polisi, hivyo kutongoja agongewe mlango.

“Polisi vipi mnakuja kwangu kama mimi jambazi, imekuwaje?” alihoji bila hata kusalimiana na askari wale.

“Mama mimi ni mkuu wa upelelezi wa wilaya nipo na askari wangu wanne pamoja na wageni wengine ambao wapo kwenye ile gari ndogo.”

“Sawa. Mnanituhumu nini?”

“Kabla sijakuambia tunachokutuhumu, saini hii hati ya upekuzi.”

Alipewa karatasi nyeupe, akaisoma kisha kuigeuza, akarudia tena kuiangalia pale mbele.

“Mnataka kupekuwa nyumbani kwangu kwa kosa gani?”

“Mama usitufundishe kazi, saini kwanza karatasi, nini tunapekua ni suala la baadaye, tunakwenda hatua kwa hatua.”

Yule mama alipewa kalamu, akasaini.

“Hapa mjumbe wenu ni nani?” aliuliza kamanda wa polisi wakati anaipokea ile hati iliyosainiwa.

“Ni nyumba ya tatu hapo kulia.”

“Lazima akaitwe ashuhudie upekuzi huu.”

“Sasa kosa ni nini?”

“Akaitwe kwanza huyo mjumbe ili naye asikie tunachokitafuta.” Nilitamani kujitokeza ili anione maana akiniona tu, atajua ni kwa nini polisi wanataka kumpekua. Alitumwa yule msichana wa kazi kwenda kumuita mjumbe.

Je, mjumbe atapatikana na itakuwaje? Fuatilia Jumanne ijayo.

Leave A Reply