The House of Favourite Newspapers

Nape Kutoka ‘Bakibencha’ Hadi Mbunge Pendwa wa JPM

KATIKA kipindi cha miaka miwili, mmoja wa wabunge watatu machachari aliyekuwa na uwezo wa kusimama bungeni kuikosoa Serikali na chama chake, ni Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye (CCM).

 

Hali hiyo ilisababisha kuwepo kwa vijembe na majibizano kutoka kwa watawala na mbunge huyo aliyekuwa katika kundi la wabunge watatu, Hussein Bashe (CCM) na Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo).

 

Kundi hilo lilitunukiwa jina la ‘bakibencha’ na Zitto kutokana na umaarufu wa wabunge hao waliokuwa wanakaa sehemu moja bungeni kabla ya Bashe kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Kilimo.

 

Misimamo na ukosoaji wa Nape ulianza kuvuma punde tu baada ya kutenguliwa katika nafasi yake ya Uwaziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo mwezi Machi 23, 2017 na nafasi yake kuchukuliwa na Dk Harrison Mwakyembe.

 

Nape alivuliwa majukumu yake siku moja baada ya kupokea ripoti ya kamati ya uchunguzi kuhusu uvamizi wa kituo cha habari.

 

KUTISHIWA BASTOLA

Hata hivyo, zimwi la sakata hilo halikumuacha Nape baada ya kuitisha mkutano na waandishi wa habari jijini Dar ambao ulizimwa na vyombo vya usalama.

 

Itakumbukwa kuwa Nape alipofika karibu na eneo la kikao alizuiwa na askari kutoka kwenye gari huku wakimshika kwa nguvu na kumtishia kwa kumnyooshea bastola. Hali hiyo ilimfanya kuongea kwa hasira akitaka kujua nia ya askari hao, wakati kundi kubwa la waandishi wa habari wakitaka wamuachie Nape aongee.

 

AWASHA MOTO

Baada ya kukumbwa na matukio hayo, Nape alianza kutoa kauli nzito na misimamo mikali iliyomfanya kuwa mmoja wa wanasiasa walioonekana kuvuta hisia.

 

Moja ya mijadala yake bungeni ni pamoja kupinga mapendekezo ya Serikali katika Sheria ya Fedha wa mwaka 2018 kwa kuchukua asilimia 100 ya tozo za mauzo ya korosho nje ya nchi (export levy) kupelekwa mfuko mkuu wa fedha za Serikali.

 

Pengine uzito wa kauli za Nape uliongezeka baada ya Rais Dk John Magufuli ‘JPM’ kutoa tamko lililoonesha namna alivyokerwa na hatua ya wabunge wa mikoa ya Kusini kuipinga hatua ya Serikali juu ya fedha hizo. Rais Magufuli alisema alikuwa amefikia uamuzi wa kupoteza wabunge wote.

 

Hata hivyo, Nape alirejea jimboni kwake baada ya kumalizika kwa vikao vya Bunge la Bajeti na kuwaeleza wapigakura wake kwamba, ametoa maisha yake ili kuwatetea wakulima wa korosho na kwamba yuko tayari kwa lolote.

 

Kumbukumbu zinaonesha Nape aliwahi kuandika katika akaunti yake ya Twitter; “Watu hawa wanapambana na hali zao! Waliniuliza bombardier ndiyo nini na sisi wa vijijini tutafaidikaje au ni kwenu mjini tu!?”

 

AOMBA MSAMAHA KWA RAIS

Septemba 10 ndiyo ulikuwa uwanja mpya kati ya Nape na Rais Magufuli baada ya mbunge huyo kwenda Ikulu na kuonana na Rais Magufuli na kumuomba msamaha.

 

Ingawa si Nape wala Rais Magufuli waliozungumza kwa nini wamekutana, lakini Septemba mwazoni kuliibuka sauti za viongozi zikiwamo za wabunge wa CCM, January Makamba (Bumbuli) na William Ngeleja (Sengerema) wakizungumzia suala la waraka ulioandikwa na makatibu wakuu wa CCM wastaafu; Yusuf Makamba na Abdurahman Kinana.

 

Hata hivyo, Rais Magufuli alisema; “Na mimi nimeshamsamehe tena kwa dhati kutoka moyoni mwangu, nimeshamsamehe na nimeshamsamehe kweli. Nape nenda ukafanye kazi, Mungu akujalie.”

 

Katika kudhihirisha sasa mambo ni shwari, Rais Magufuli alifanya ziara katika Mikoa ya Lindi na Mtwara na kuwaeleza wananchi wa Mtama namna anavyompenda Nape kwa kuwa ni mchapakazi na kuongeza kuwa angelikuwa na binti angempatia amuoe.

 

Ni dhahiri kuwa ‘bakibencha’ imevurugika, kwa kuwa amebaki Zitto peke yake kama mkosoaji mkuu, kwa kuwa tayari Bashe ameteuliwa kuwa naibu waziri, jambo ambalo hawezi kukosoa Serikali bungeni zaidi ya kuitetea, ilihali Nape ambaye sasa ni mbunge pendwa kwa Rais Magufuli anatazamwa na wengi iwapo ataendeleza cheche zake ama lah!

STORI: GABRIEL MUSHI, DAR

Comments are closed.