The House of Favourite Newspapers

Simba Yamchomoa Kocha Stars

0

MABOSI wa Simba wanauchukulia umuhimu mchezo wao wa watani wa jadi, Yanga ni baada ya kuwasiliana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili kupata ruhusa ya kumchukua kocha msaidizi wa timu ya taifa, Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Heroes’ Suleiman Matola, kwa ajili kuanza fasta kibarua cha kukinoa kikosi hicho.

 

Hivi karibuni Simba iliwatimua makocha wake Mbelgiji, Patrick Aussems na msaidizi wake Denis Kitambi na sasa itakuwa chini ya kocha huyo ambaye ni mchezaji wao wa zamani.

 

Matola ni kocha msaidizi wa Taifa Stars chini ya Ettiene Ndairagije na wamekuwa wakifanya kazi kwa ushirikiano mzuri.

 

Hata hivyo, jana ilikuwa mwisho kwa kocha huyo kuwa na timu hiyo ya taifa, baada ya kupata habari kuwa Simba wameshatuma barua pepe kwenye Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwa wanamtaka kocha huyo akaanze maandalizi ya kuvaana na Yanga.

Simba na Yanga watavaana Januari 4 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwenye mchezo ambao unaonekana kuwa na hekaheka za hapa na pale.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatano, Matola jana alipigiwa simu na uongozi wa Simba na kumtaka aende kwenye hoteli moja ya jijini Dar kwa ajili ya kumalizana.

 

“Matola alipigiwa simu asubuhi na kutakiwa kwenda kwenye hoteli moja hapa Dar kwa ajili ya kukutana na mabosi wa Simba wasaini nyaraka zilizokuwa zimebaki.

 

“Kule Stars wao walipewa barua na Simba na sasa siyo kocha wao tena, ingawa aliomba kuwa anakwenda Simba sasa hivi kwa kuwa kocha mkuu hayupo na baadaye atarudi, lakini jana ileile Zubeir Katwila wa Mtibwa alitua kambini Stars na kuanza kazi.

 

“Katwila alipigiwa simu usiku na kutakiwa kupanda basi mapema sana kuja Dar na kweli alitimiza hilo na kuanza kazi na timu na ndiye atasafiri.

 

“Kuhusu kurudi kwa Matola Stars, siwezi kusema lakini najua timu yoyote ya taifa, ukiondoka kurudi ni kazi sana,” kilisema chanzo.

 

Alipoulizwa Matola ambaye ni mchambuzi wa gazeti hili (tazama ukurasa wa 6) alisema kuna mambo yake binafsi anashughulikia mjini. “Kuna ishu zangu binafsi nashughulikia mjini nitakupigia,”alisema mchezaji huyo wa zamani wa Supersport ya Afrika Kusini.

Leave A Reply