The House of Favourite Newspapers

DC Chongolo Kutoa Tuzo Kwa Mitaa Misafi

0

 

MKUU wa Wilaya ya Kinondoni,  Daniel Chongolo,  ameanzisha kampeni ya utoaji tuzo kwa mitaa itakayofanya vizuri kwenye suala la usafi ambapo kila mtaa utapatiwa zawadi ya fedha.

 

Aidha amewaonya wananchi wanaotupa taka hovyo na hivyo kuwataka watendaji hao kusimamia sheria kwa watakaojihusisha na uharibifu huo wa mazingira ikiwemo kulipa faini kwa mujibu wa sheria.

 

Ametoa kauli hiyo leo, wakati wa ufunguzi wa semina elekezi kwa wenyeviti wa serikali, wajumbe wa mitaa na watendaji kata iliyofanyika katika ukumbi wa King Solomoni Oyster Bay ambako amesisitiza kuwa lengo la kampeni hiyo ni kuongeza motisha katika kuboresha halmashauri hiyo kuwa katika muonekano mzuri, na kuwasisitiza watendaji hao  na wenyeviti wa mitaa kuisimamia kwa ukamilifu.

 

Amefafanua kuwa tuzo hiyo itatolewa kila baada ya miezi mitatu ambapo mtaa utakaoibuka na ushindi utapatiwa fedha taslimu kiasi cha shilingi 500,000, mshindi wa pili sh. 300,000 huku mshindi wa tatu akipata 200,000.

“Halmashauri ya Kinondoni ni safi, lakini tunatakiwa kufanya vizuri zaidi, kwa mantiki hiyo tunakuja na kampeni ya usafi wa kila mtaa, watakaofanya vizuri watapatiwa zawadi ya fedha, na fedha hizo zitabaki kwenye mitaa yenu kwa ajili ya shuguli nyingine,” amesema.

 

”Watakaoendesha mchakato huo ni nyie wenyeviti na wajumbe wa mitaa, kazi yangu mimi ni kuweka fedha kwa ajili ya kutoa zawadi, na kampeni hiyo tunaanza leo hii tarehe nne mwezi wa 12 kwa hiyo ikifika tarehe nne mwezi watatu 2020 tutatoa tuzo hiyo kwa mitaa itakayokuwa imeshinda.

 

Ameongeza kuwa pamoja na tuzo hizo kutolewa amewataka watendaji kusimamia sheria na kanuni za utunzaji mazingira ikiwemo kutoza faini kwa watu wanaotupa taka hovyo kwani kwakufanya hivyo wataongeza ufanisi na ubora wa mitaa kuendelea kuwa misafi.

 

“ Zipo sheria za usafi ambazo zimewekwa kwa mujibu wa sheria lakini hazifuatwi, watendaji, wenyeviti na wajumbe mliopo hapa nendeni mkazisimamie vizuri,”amesisitiza.

Katika hatua nyingine  amewataka viongozi hao kusimamia mapato vizuri sambamba na kuepuka rushwa kwa kuwa kufanya hivyo kutawaingiza kwenye matatizo makubwa.

 

“ Kuna suala la rushwa, niwaonye msijihusishe na mambo hayo, leo hii hapa kuna maafisa kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wapo hapa na wao watawaeleza madhara ya kupokea au kutoa rushwa, niwaombe sana msikilize kwa makini na mkayafanyie kazi,” ameongeza.

 

Kwa upande wake ofisa utumishi mkuu wa Halmashauri hiyo, Faudhia Nombo, amesema kuwa lengo la mafunzo hayo elekezi ni kuwawezesha viongozi hao ili waweze kutekeleza majukumu ya usimamizi na uendeshaji wa shughuli mbalimbali katika mitaa yao kwa kuzingatia sera, sheria, taratibu, kanuni na miongozo iliyopo ili kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Leave A Reply