The House of Favourite Newspapers

National Public Speaking Competition, Mchujo wa Pili Vipaji Kama Vyote

0

SHINDANO la National Public Speaking Competition limeendelea kupasua anga baada ya jana Jumapili kukamilisha hatua ya mchujo wa pili kwa kuwapata washiriki 80.

 

 

Shindano hilo linalenga kusaka vipaji hasa kwa vijana wenye uwezo mkubwa wa kuzungumza katika hadhara mbalimbali ambalo limeanzishwa na kampuni ya Global Publishers.

 

 

Shindano hilo linaloitwa National Public Speaking Competition, lilizinduliwa Novemba 2019 kwa mchakato wa kugawa fomu kwa vijana Tanzania nzima baada ya kuzijaza walizirudisha katika ofi si za kampuni hiyo Sinza Mori jijini Dar.

 

 

Mchujo huo umefanyika kwa muda wa siku tatu kwa lengo la kutafuta washiriki 80 katika washiriki 170 ambao walipenya kwenye usaili wa kwanza uliofanyika mapema mwezi huu.

 

 

Washiriki hao ambao asilimia kubwa ni vijana, walifanya usaili huo mbele ya jopo la majaji ambao walionyesha kuvutiwa na uwezo wa washiriki wengi walivyoweza kuzungumza kwa ushawishi mkubwa kabla ya kwenda katika hatua ya pili ambayo itakuwa ya mchujo.

 

 

Mratibu wa shindano hilo, Pacifi c Ibrahimu anasema kuwa ni mara ya kwanza kwa shindano hilo kufanyika nchini na katika nchi za Afrika Mashariki limefi kia katika hatua kubwa baada ya vipaji vya washiriki kusababisha kuongeza siku kutokana na kuonyesha uwezo mkubwa wa kuzungumza mbele ya majaji wa shindano hilo.

 

 

Ibrahimu alieleza kuwa, awali walitegemea kupata washiriki 30 ambao wangeweza kuingia kambini kwa ajili ya kuendelea na mashindano hayo lakini imeshindikana kufanya hivyo kutokana na washiriki kumwaga nondo za kutosha ambazo zimepelekea majaji kubadili uamuzi wao walioupanga mwanzoni.

 

 

“Kiukweli tunashukuru mchakato wa shindano letu unaenda kwa sababu tumetoka kwenye kutoa fomu 400 lakini wakaweza kufi ka washiriki 300 na kati ya hao tukapata washiriki 170 kwa ajili ya hatua ya mchujo wa pili ambao tumekamilisha jana baada ya kuwa kwenye mchakato kwa siku tatu mfululizo.

 

 

 

“Lakini sasa hivi idadi ya washiriki haitakuwa ile ya 30 ambayo tuliitangaza sasa hivi tumepata washiriki 80 ambao nao tutaendelea kuwapunguza kwenye mchujo wa mwisho ambao utatoa washiriki kati ya 40 au 30 ambao wataingia kambini kwa ajili ya kuendelea na mashindano.

“Tumeamua hivi kwa sababu kubwa ya majaji kupagawishwa na vipaji vya washiriki kwa sababu kila anayeingia anakuwa yupo moto kutokana na nondo zake lakini pia wanaonyesha wana vipaji vikubwa ndiyo maana majaji wakaona wabadilishe njia ili kutoa fursa kubwa kwa hawa ambao wamepita.

 

“Kikubwa wadau wanapaswa kuelewa kwamba washiriki wote ambao mpaka sasa wameshatolewa ni washindi kwa sababu wameonyesha uthubutu mkubwa juu ya mashindano haya ambayo ni mara ya kwanza kufanyika katika nchi za Afrika Mashariki hivyo sisi tunajivunia wao.

“Lakini waliobahatika kusonga mbele wanatakiwa wakaze buti kwa sababu vita ya ushindani bado haijaisha hivyo wasijisahau kabisa na kuona wameshashinda kwa sababu bado kuna mchujo wa mwisho ambao tutaweka wazi lini utaanza kwa ajili ya kupata wale ambao watakuwa na vigezo vya kuingia kambini kwa ajili ya kupata mafunzo kutoka kwa majaji wetu huku mchakato wa shindano ukiendelea.

 

“Nadhani watu wengi watakuwa wanataka kuelewa kwa nini tumeamua kufanya shindano la kumtafuta mtu mwenye uwezo wa kungumza mbele ya hadhara kwa ngazi ya kitaifa kwa sababu malengo yetu ni kuhakikisha tunazalisha vijana wenye uwezo wa kusimama katika mkusanyiko wa watu wakazungumza kwa kufuata vigezo vya uzungumzaji kwenye mihadhara.”

 

 

Hata hivyo, Mkuu wa Kitengo cha Global TV, Calvin Nyorobi, alisema kuwa kwa sasa shindano hilo linaonekana kupitia Global TV Online huku lengo kubwa la kufanya hivyo ni kuionyesha jamii ambayo itaweza kupigia kura washindi utakapofi kia mchakato wa kufanya hivyo.

 

“Kikubwa naomba watu wafuatilie shindano hili kupitia chaneli yetu ya Global TV Online ambayo inapatikana katika mtandao wa YouTube lakini pia unaweza kusubscribe ili uweze kuona matukio mengine ya habari tutakayokuwa tunarusha na jambo hili litaonekana duniani hatua kwa hatua,” anasema Nyorobi.

 

MAKALA: IBRAHIM MUSSA, Dar Salaam

Leave A Reply