The House of Favourite Newspapers

Eliuter Mpepo: Yupo Msumbiji, Akili Ipo Ureno

0

ELIUTER Mpepo ni mmoja wa washambuliaji wazawa wanaofanya vizuri nje ya nchi, anakipiga kwa mkopo katika timu ya CD Costa Do Sol ya nchini Msumbiji.

 

Timu ya A.D Sanjoanense ya Ligi Daraja la Kwanza nchini Ureno, ilimsajili mwanzoni mwa Januari, mwaka huu kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Buildcom ya Zambia.

 

Baada ya kusajiliwa na timu hiyo ya Ureno, alipelekwa moja kwa moja kwa mkopo wa miezi sita Klabu ya CD Costa Do Sol ambao ndio mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Msumbiji.

 

Nyota huyo amefanikiwa kuipa timu yake ubingwa wa Ngao ya Jamiii dhidi ya UD Songo iliyoisha kwa sare ya 1-1. Kwenye penalti Mpepo alifanikiwa kupiga penalti ya mwisho ya ushindi na kuipa timu hiyo ubingwa.

 

Ni mwanzo mzuri kwa mshambuliaji huyo kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu ya Msumbiji inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi mwezi Aprili, mwaka huu.

 

Kuelekea ligi hiyo kuanza kutimua vumbi, Championi Jumatatu lilipata muda wa kuzungumza na mshambuliaji huyo ambaye anaweka wazi mipango yake kwa ujumla pamoja na changamoto zinazomkumba nchini humo.

 

KUCHUKUA UBINGWA UKIWA MCHEZAJI MPYA UNAJISIKIAJE?

“Najisikia vizuri sana kwani siku zote mashabiki hupenda kuona timu zao zikifanikiwa zaidi na kwa upande wangu kufunga kumenipa matumaini zaidi kwa kuwa mimi ni mchezaji mgeni katika timu hii.

 

“Maana kwa mshambuliaji, usipofunga mabao halafu ni mgeni, unawapa mashaka mashabiki kwa kuwa unaonekana kama si tishio, hutimizi wajibu wako, hivyo kwangu lipo tofauti kwani kwenye michezo sita ya kirafiki niliyocheza mpaka sasa, nimefunga mabao manne, hivyo hii inanifanya nijiamini zaidi baada ya kufanikiwa kufunga mabao na kuipa timu yangu ubingwa.

 

KUTOKA TANZANIA MPAKA ULIPOFIKA SAFARI YAKO UNAIELEZEAJE?

“Hakuna safari ambayo ni rahisi siku zote, kila safari huwa na milima na mabonde, nimepitia changamoto nyingi sana mpaka kufikia hapa nilipo, nimeanza kucheza ligi za chini kabisa hapa nchini kabla ya kufika Ligi Daraja la Kwanza na hatimaye kucheza ligi kuu.

 

“Mtu anaweza akaona ni rahisi lakini kuna ambao hawafahamu kama niliwahi kucheza ligi ya Tanzania katika timu za Mbeya Kwanza, Prisons, Singida, kisha nikaenda Buildcom ya Zambia na sasa Costal do sol ya Msumbiji ambayo nipo kwa mkopo nikitokea timu ya A.D Sanjaonense ya nchini Ureno.

 

UMESHAWAHI KUITUMIKIA TIMU HIYO YA URENO?

“Hapana sijawahi kuitumikia hata mchezo mmoja kwa kuwa waliponisajili tu wakanitoa kwa mkopo moja kwa moja kuja nchini Msumbiji.

 

UNATAMANI KUITUMIKIA TIMU HIYO?

“Natamani sana kwa kuwa ni timu ambayo ipo kwenye Bara la Ulaya sehemu ambayo naamini ni nzuri sana kwa afya ya mwanamichezo hasa mpira wa miguu.

 

“Unaweza ukashangaa kwa kuwa labda timu hiyo inashiriki Ligi Daraja la Kwanza natamani kwenda kucheza huko kuliko hapa Msumbiji ambapo nacheza ligi kuu ila kwa mtazamo wangu ni bora kucheza daraja la kwanza nchini Ureno kuliko kucheza Ligi Kuu ya Msumbiji.

 

KUNA UTOFAUTI GANI KATI YA LIGI YA MSUMBIJI NA TANZANIA?

“Bado ligi haijaanza lakini utofauti mkubwa upo kwenye miundombinu yaani viwanja vya kuchezea, Msumbiji karibia viwanja vyote vya ligi vimetengenezwa kwa nyasi bandia, tofauti na viwanja vingi vya Tanzania.

 

CHANGAMOTO ZIPI KWAKO NI NGUMU UKIWA MSUMBIJI?

“Changamoto kubwa huku Msumbiji kuna joto kali sana tofauti na Tanzania, hivyo kama nilivyokutaarifu mwanzo kuwa viwanja vya huku ni nyasi bandia hivyo ukiongeza na joto, huwa linanipa wakati mgumu sana maana viatu hupata joto kali mno, ila wenzangu wamezoea.

 

VIPI KUHUSU CHAKULA NA LUGHA YA MAWASILIANO HAVIKUPI SHIDA?

“Kuupata ugali huku ni vigumu sana, kwani kuna baadhi ya maeneo haupatikani kabisa tofauti na Tanzania kila sehemu ugali unapatikana, na mimi napenda sana ugali hivyo inanilazimu kula vyakula kama wali, kuku na vyakula vingine ambavyo Tanzania nilikuwa navitumia na huku vinapatikana.

 

“Kuhusu lugha ya mawasiliano huwa natumia zaidi English (Kiingereza) maana wachezaji wengi sana na wakazi wa huku huzungumza Kireno ambayo ndio lugha ya Taifa la Msumbiji, na mimi sikifahamu Kireno.

 

“Hivyo naongea Kiingereza na watu wachache sana kwa kuwa wanaokifahamu Kiingereza si wachezaji wengi, hii ni changamoto kubwa sana kwangu.

 

MALENGO YAKO KIUJUMLA YAPOJE KWA SASA?

“Kuhakikisha nafanya vizuri katika Ligi Kuu ya Msumbiji, kubeba taji la ubingwa wa ligi na kuibuka mfungaji bora ili niweze kurudi katika timu yangu ya Ureno ambayo naamini wamenileta huku ili nipate muda mwingi wa kucheza huku wakinifuatilia maendeleo yangu, nikifanya vizuri watanirejesha,” alisema mshambuliaji huyo.

MARCO MZUMBE, Dar es Salaam

Leave A Reply