The House of Favourite Newspapers

Mimba kuyeyuka kimaajabu kwatikisa

0

DUNIA ina maajabu mengi, ila mkoani Mbeya kinachotikisa kwa sasa ni mimba kwa baadhi ya akina mama kuyeyuka kimaajabu; UWAZI lina habari kamili.  Chanzo chetu kutoka eneo la tukio, kilimuita mwandishi wetu: “Njoo katika Kijiji cha Kilasilo Kata ya Ikimba wilayani Kyela mkoani Mbeya, kuna wanawake wanabeba mimba za jini.”

MIMBA ZA MAJINI NI ZIPI?

Mwandishi wetu alipomhoji mtoa taarifa kuhusu ‘mimba za jini’ alijibiwa: “Zipo nyingi tu, wanawake wanapata ujauzito, lakini baadaye unayeyuka kimiujiza au wanajifungua kiumbe cha ajabu.”

MWANDISHI ENEO LA TUKIO

Mwandishi wetu alipofika eneo la tukio na kufanya mazungumzo na baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Kilasilo, walisema kuna matukio ya kishirikina yanaendelea kijijini hapo na wengine kukana kujua chochote. Hata hivyo, safari ya mwandishi wetu ilifika kwa dada Huruma (26) (jina la pili tunalihifadhi) mkazi wa kijiji hicho ambaye alidai kuwa yeye ni miongoni mwa wanawake ambao wamekumbwa na mkasa wa mimba yake kuyeyuka kimaajabu.

Mwanamke huyo ambaye uchunguzi wa UWAZI umebaini kuwa ndiye aliyekoleza madai hayo ya ‘mimba za jini’ alisema katika mahojiano maalumu kuwa:

“Huu ulikuwa ni ujauzito wangu wa pili, wa kwanza nilijifungua salama bila matatizo na hadi sasa mtoto yupo hai. “Nilipopata mimba ya pili, nilianza kuhudhuria Kliniki tangu ilipofika miezi minne na madaktari walibainisha kweli nilikuwa na ujauzito na kadi ya kliniki wakanipa.”

UJAUZITO WAKE WAYEYUKA

“Sasa juzi (Jumatano iliyopita) asubuhi, nilienda hospitali ya wilaya Kyela nilikokuwa nahudhuria kliniki yangu. “Nesi aliponipima akasema sina ujauzito! Nikamuuliza umekwenda wapi wakati mwezi uliopita ulikuwepo na mlisema unaendelea vizuri? Akanijibu ‘wewe jua tu kwamba huna mimba’. “Kusema kweli nilishikwa na mshangao na huzuni kubwa, nikabaki najiuliza sasa sina mimba na hili tumbo kubwa lote la nini?”

TUMBO NALO LANYAUKA KAMA PUTO

Mwanamke huyo aliongeza kuwa baada ya kurejea kutoka hospitali huku akiwa na majibu hayo, akashangaa tumbo lake nalo likayeyuka na kubaki dogo.

“Si unaniona (alimuonesha mwandishi tumbo) huku akimpatia kadi ya kliniki aliyokuwa akiitumia na daftari ambalo majibu ya kutokuwa mjamzito yaliandikwa.

TAHARUKI KIJIJINI

Marry Kiliwa mkazi wa Kilasilo, alisema yeye ni mmoja wa majirani wa dada huyo ambaye amemshuhudia mwanamke huyo kwa miezi kadhaa akiwa mjamzito, lakini ameshangaa kumuona hana mimba.

“Mimi nilipomuona hivi nikajua katoa, sasa aliposema tunashangaa imeenda wapi?” Alisema Marry.

Naye Ezekia Mwakasekele, mwenyekiti wa kitongoji cha Kilasilo, alisema ni tukio la kwanza la kushangaza kutokea kijijini humo.

“Ndugu mwanahabari, siwezi kulizungumzia kwa kina suala hilo kwani dada huyo hajawahi kuja ofisini kwetu akieleza tatizo lililomkuta.

“Nakosa majibu ya kutoa, lakini hata kama ni masuala ya ushirikina, serikali hii haiamini uchawi, hivyo jambo hili lipo nyuma ya pazia,’’ alisema Mwakasekele bila kufafanua zaidi anaposema nyuma ya pazia anamaanisha nini?

Katule Kingamkono diwani wa kata hiyo alisema, tukio hilo aliliona kwenye mitandao ya kijamii lakini yeye hajafika kwenye makazi ya dada huyo kuzungumza naye, hivyo hawezi kulizungumzia tukio hilo kwa kina.

MGANGA MKUU ANENA

Mariam Mgwere, mganga mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Kyela, alisema:

“Kuna wakati huwa inatokea mwanamke akajiona mjamzito na hata vipimo vikabaini, lakini baadaye akaonekana hana ujauzito.

“Nikushauri mwandishi, uwasiliane na watoa huduma wanaohusika na masuala ya mimba kwa akina mama watakuwa na majibu ya kutosha.”

MATUKIO MENGINE YA AJABU

Kabla ya kuwatafuta wataalam wa afya kama alivyoshauriwa, mwandishi wetu aliendelea kufanya uchunguzi na kubaini kuwa imani za kuwepo kwa ‘mimba za jini’ imeenea mkoani Mbeya.

“Haya matukio yapo, sema kuna wanawake yanawatokea lakini hawasemi kwa sababu wanaogopa kuhusishwa na masuala ya ushirikina.

“Hivi karibuni katika Kijiji cha Njisi Kata ya Kajunjumele wilayani Kyela, kuna mwanamke mmoja alishika ujauzito wa ajabuajabu kwa miezi 13, alipokuja kujifungua, akajifungua kiumbe cha ajabu kinachofanana na chura,” chanzo chetu kilisema.

Mama mmoja ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini, alimwambia mwandishi wetu kuwa:

“Mimi kuna mwanangu alipata ujauzito ukapotea kimaajabu, hivi ninavyokwambia hadi leo anahangaika kushika mimba, kitu ambao nawaomba wana Mbeya hasa huku kwenye kitongoji chetu tuzidishe maombi ili huyu pepo mchafu atoke.”

DAKTARI AFAFANUA KITAALAM

Akifafanua kitaalam kuhusu matukio kama hayo, Dk. Sadick Sizya kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili alisema, mimba kuyeyuka hutokea kwa nadra katika mazingira mbalimbali.

“Kwanza inaweza kutokea pale ambapo mimba imetunga nje ya mfuko wa uzazi, kwa maana hiyo mama akipima ujauzito kwa njia za kawaida kama mkojo, vipimo vitaonesha ipo lakini akipima kwenye tumbo la uzazi haionekani.

“Nakumbuka kisa kama hiki kilinitokea kule Ifakara mkoani Morogoro ambapo nilikuwa namhudumia mgonjwa wa aina hii, mimba ilitunga nje ya mfuko wa uzazi kwa hiyo alipoenda kupima kwenye Ultrasound ambayo inapima mfuko wa uzazi, mimba haikuonekana, lakini baada ya kufanya vipimo vingine, tukagundua mimba ipo nje ya mfuko wa uzazi, tukamfanyia operesheni na tunamshukuru Mungu wote mama na mtoto walitoka salama.

“Kwa hiyo, kuna matukio ya aina hiyo, lakini kingine ni kwamba kuna mimba ambazo wakati inatunga na kukua, ikatokea mtoto akafia tumboni, kama mama asipojigundua mapema kuna uwezekano mimba hiyo ikanyonywa na mwili wa mama, yaani ikayeyuka.

“Kitaalam tunaita Lithopedion, kesi za aina hii zimefanyiwa utafiti hivi karibuni na Jarida maarufu la masuala ya Afya la Rotal Society of Medicine ambapo lilitoa ripoti ya utafiti ambao unaonesha zaidi ya wanawake 290 duniani, wametokewa na kitu cha namna hiyo.

“Pia kuna mama mmoja raia wa Algeria, kwa upande wake mimba iliyeyuka, ikakaa muda wa miaka 30 tumboni, lakini yule mama akiwa na umri wa miaka 73, alipoenda kufanyiwa kipimo cha CT Scan ikaonekana mimba ipo kwenye nyonga, hapo ni kwamba mtoto baada ya kufariki, mabaki yake yakanyonywa na mwili wa mama ndiyo maana hapo tumbo linaweza kunywea,” alisema.

Aidha, pamoja na hayo, alisisitiza umuhimu wa kuendelea kufanya utafiti na kufuatilia baadhi ya tafiti zinazotolewa na taasisi nyingine duniani kuhusu matukio ya aina hiyo na kuwashauri wanawake kuendelea kufuatilia afya zao za uzazi hata pale ambapo mimba zao zinayeyuka katika mazingira ya kutatanisha.

Leave A Reply