The House of Favourite Newspapers

Mh! Eti Ray, Steve Nyerere Nao Mapedeshee

0

ray nyerere na bella (2)
MIAKA michache iliyopita, nilipata kuwa mdau mkubwa wa muziki wa dansi, nikipatikana katika karibu kumbi zote ambazo bendi kubwa zilifanya mambo yao jijini Dar es Salaam. Huko, nilikutana na watu wengine waliokuwa na ‘wazimu’ zaidi kuliko mimi.

Hawa, waliitwa majina ya kutukuzwa na wanamuziki, wengi wao wakitajwa kwenye nyimbo. Ninamkumbuka ‘mshkaji’ Fikiri Madinda, Papaa Chosta, Hussein Makabureta, Jack Pemba, Chief Kiumbe, Mwakamele mkubwa na mdogo wake Macdonald Mwakamele, kuwataja kwa uchache.

Hawa, sifa yao kubwa ilikuwa ni kuwatunza wanamuziki na wacheza shoo. Kwao, kupoteza shilingi laki tano hadi milioni moja kwa siku haikuwa ishu. Utamuona Mango Garden akimwaga fedha jukwaani kwa Twanga Pepeta, ukadhani ameishiwa, lakini baadaye unapohamia Msasani Club unakutana naye anafanya vitu vyake kwa Wazee wa Ngwasuma.

Na hiyo, ni kuanzia Ijumaa wikiendi inapoanza. Kwa hesabu za haraka ni kwamba hawa jamaa kwa siku hizo tatu, walikuwa na uwezo wa ‘kugawa’ zaidi ya milioni tatu kila wiki kwa wanamuziki. Ni lazima walikuwa na mfereji usiokauka.

Siyo mwendaji sana kwenye kumbi hizo siku hizi, lakini hata mara moja moja ninapokumbushia, siwaoni. Baadhi yao nimeambiwa wamefulia na wengine wanaishi kwa kujificha. Wachache bado wapo vizuri lakini wamebadili aina ya maisha.

Katika siku za hivi karibuni wameibuka mapedeshee wapya kutoka Bongo Movies. Walianza wadada Wema Sepetu na hasimu wake Kajala Masanja, wakishindana kutunza wasanii katika maeneo tofauti walikoenda. Sitawajadili sana hao kwa sababu moja tu kubwa, ni watoto wa kike!

Lakini sasa kuna Steve Nyerere na kwa mbali anakuja Vin cent Kigosi ‘Ray’. Nao hivi sasa wanagawa fedha ‘kama hawana akili nzuri’ kwa wasanii majukwaani. Sijui maisha yao kivile, lakini chanzo chao kikubwa cha fedha ni filamu. Ninalijua soko la filamu lilivyo na ninaujua uwezo wao wa uigizaji na hata malipo wanayolipwa kwa kazi wanazocheza nayajua.

Kwamba kazi hizo zinawalipa na kuwapa jeuri ya kumtunza mtu laki tano au milioni? Pengine wana chanzo kingine cha mapato ambacho sikijui, lakini je, kinawapa uhalali huo?

Wanapataje fedha na wanatumia vipi yanaweza kuwa ni maisha yao ambayo hayanihusu, lakini hili halinizuii kuwashauri, hasa katika wakati ambao vijana wana changamoto nyingi za kukabiliana na maisha.
Hawa wametoka familia za kawaida kabisa ambazo wengi wa ndugu zao wana maisha ya kudunduliza, bila kujali kama wapo mjini au kijijini. Na ukute wana matatizo ya msingi, lakini wanakosa msaada wa karibu kwa kuwa hela ni ngumu.

Leo hii wanaposoma gazetini kuwa Papaa Steve au Pedeshee Ray ‘wametupa’ milioni moja mbele ya macho ya kamera, hakika inawauma. Siyo ajabu siku au wiki kadhaa nyuma, watu hawa waliwahi kuwaomba msaada!
Haya ni maisha ya kutaka sifa. Kama umepata mchongo uliokupa fedha nyingi, kuna haja gani ya kuonesha hadharani? Vijana wanaojitambua, hawajioneshi katika vitu vinavyoweza kuwashushia hadhi kama hivi, bali huwekeza kimyakimya kwa faida ya kesho.

Kama fedha ni nyingi, kwa hadhi ya majina yao, ingependeza zaidi kama wangewatafuta watu wenye uhitaji maalum kama yatima, wazee wasiojiweza, wagonjwa mahospitalini na kuwapa chochote, badala ya kufanya mambo yenye kuashiria kujikweza.

Mambo kama haya hufanywa na watu wenye nia ya kutafuta majina ili wayatumie kwa utapeli au kupata wanawake hapa mjini, vitu ambavyo Ray na Steve tayari wanavyo, sasa wanatafuta nini?

Leave A Reply