The House of Favourite Newspapers

The angel of darkness – 25

Magaidi walioshambulia katika kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi, Kenya wanasababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa.

Baada ya Watanzania hao kufa, wanawaacha yatima watoto wao mapacha, Arianna na Brianna ambao kila mmoja anapitia maisha ya tofauti kabisa na mwenzake. Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anabakia kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.

Kila mmoja anapitia mitihani ya aina yake maishani mwake. Brianna, yeye analelewa na familia ya kimaskini ya mzee Njoroge baada ya Mashango kufariki dunia kwa kugongwa na gari.

Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anauza kinyemela nyumba aliyoachiwa na wazazi wake na kutorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.

Akiwa Arusha, anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kutaka kuyabadilisha maisha yake. Wanakubaliana wamdanganye mfanyabiashara huyo kwamba wawili hao ni ndugu wa damu wakati ukweli ni kwamba wawili hao ni wapenzi.

Hatimaye wawili hao wanahamia kwenye jumba la kifahari la Msuya. Mapenzi kati ya Arianna na Msuya yanaanza kukolea, jambo linalosababisha Diego awe kwenye wakati mgumu sana kihisia kutokana na wivu uliokuwa ukimsumbua.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

“Ahsante bae (mpenzi)!” alisema Arianna na kumrukia Msuya mwilini, wakakumbatiana na kugandana kama ruba huku machozi ya furaha yakiendelea kumtoka Arianna. Ndani ya muda mfupi tu tangu afahamiane na Msuya, alijikuta akiishi kwenye ulimwengu mwingine tofauti kabisa.

Wakiwa wamekumbatiana kwa mahaba, wote walisikia mlango ukigongwa, bila hata kuuliza chochote Arianna akajua lazima atakuwa ni Diego.

“Atakuwa ni kaka Diego, ngoja nimsikie anasemaje,” alisema Arianna huku akijitoa kwenye mikono ya Msuya, akaenda kufungua mlango ambapo macho yake yaligongana na ya Diego, kwa makusudi akafungua mlango ili Diego aone kwamba Msuya alikuwepo ndani kwani kwa jinsi anavyomjua, angeanza kuzungumzia mapenzi na kuharibu kila kitu.

“Niko na shemeji yako, vipi ulikuwa unasemaje?”
“Nilitaka kukujulia hali maana hatujaonana tangu asubuhi,” Diego alijivunga ili kumpoteza maboya Msuya. Akaingia ndani na kumsalimia kwa heshima.

“Nilitaka kujua kama dada yuko salama maana tangu asubuhi hatujaonana, basi mimi niko sebuleni,” alisema Diego baada ya kumsalimu Msuya, akatoka na kuwaacha wawili hao, akaelekea sebuleni huku moyo wake ukiwaka moto kutokana na wivu wa kimapenzi.

“Siyawezi haya mateso, hata kama Msuya ana pesa isiwe sababu ya kunitesa kiasi hiki, haiwezekani! Na mimi nina moyo unaosikia maumivu,” Diego alijisemea moyoni huku akiwa amekaa kwenye runinga kubwa ya kisasa (flat screen) pale sebuleni kwa Msuya.

Japokuwa kwa kipindi kirefu alikuwa kwenye uhusiano na Arianna siyo kwa sababu anampenda bali ili akidhi haja zake za kimwili, kitendo cha kuona Msuya anamuonesha mapenzi mazito msichana huyo kilimfanya aanze kujisikia wivu mkali ndani ya nafsi yake.

Ni hapo ndipo alipogundua kwamba kumbe ukiachilia mbali kukidhi haja zake za kimwili, alikuwa akimpenda Arianna kutoka ndani ya moyo wake na hakuwa tayari kuona anampoteza. Aliendelea kuumia ndani ya moyo wake pale sebuleni huku akiwa hajui nini cha kufanya.

“Unaonaje kama mdogo wako badala ya kukaa tu hapa nyumbani na kufanya kazi ndogondogo tumtafutie chuo ili kesho na keshokutwa na yeye awe na kazi yake, aanzishe familia yake?” Msuya alimuuliza Arianna baada ya Diego kutoka na kuwaacha.

“Ni wazo zuri mume wangu lakini tangu akiwa mdogo Diego alikuwa akiwasumbua sana wazazi wetu, hakuwa akipenda kusoma, labda ujaribu kuzungumza naye wewe shemeji yake anaweza kukuelewa,” alisema Arianna na kuzidi kumpoteza maboya Msuya, akaamini kweli wawili hao walikuwa ndugu wa kuzaliwa.

Baadaye walitoka na kwenda kujumuika na Diego sebuleni, wakawa wanapiga stori za hapa na pale lakini Diego alionesha wazi kwamba hakuwa sawa. Wivu ulikuwa ukimtesa ndani ya moyo wake, jambo ambalo Arianna alilijua na kukosa cha kufanya.

Baadaye chakula kiliandaliwa, wakala pamoja na kuendelea kutazama runinga sebuleni hapo mpaka muda wa kulala ulipofika. Diego ndiye aliyekuwa wa kwanza kuaga na kuelekea chumbani kwake kulala, akawaacha Msuya na Arianna wakiwa pale sebuleni.
“Haya usiku mwema mume wangu, mimi naenda kulala,” alisema Arianna huku akisimama lakini Msuya alimzuia na kumtaka aendelee kukaa.

“Yaani unataka kwenda kulala peke yako wakati mimi nipo? Haiwezekani, naomba tukalale wote chumbani kwangu,” alisema Msuya kwa sauti ya chini, Arianna akaachia tabasamu hafifu na kutingisha kichwa kuonesha kukubaliana na alichokisema, Msuya akainuka na kumshika mkono Arianna, akamsaidia kuinuka pale alipokuwa amekaa kisha taratibu wakapandisha ngazi za jumba hilo la kifahari la Msuya mpaka kwenye chumba chake cha kifahari.

“Nakupenda sana Arianna, wewe ni mwanamke wa kipekee kwangu, nipo tayari kufanya chochote kwa ajili yako.”

“Kweli Msuya?”
“Kweli mpenzi wangu, nitakutunza na kukulinda kwa uwezo wangu wote mpaka mwisho wa maisha yangu, sipo tayari kuona unapatwa na tatizo lolote.”

“Kama kweli unanipenda naomba unioe niwe mkeo halali wa ndoa,” alisema Arianna, Msuya akamsogeza karibu yake, akamkumbatia kimahaba na kumbusu mdomoni.
“Niambie unataka nikuoe kwa ndoa ya aina gani?”

“Nataka unioe kwa ndoa ya kifahari, nataka kupendeza mpaka kila mtu ashangae kisha twende kula fungate mbali kabisa, ikiwezekana hata nje ya nchi,” alisema Arianna, wazo ambalo Msuya alilikubali kwa moyo mkunjufu, akamtaka Arianna kuwa na subira kidogo wakati mipango ya ndoa ikianza kufanywa.

Maneno hayo ya Msuya yalimfurahisha mno Arianna, sasa akawa na matumaini makubwa kwamba yupo kwenye mikono salama na baada ya kuhangaika sana, hatimaye alikuwa amepata mtu wa kutulia naye.

Kama ilivyokuwa kwa usiku wa siku iliyopita, wawili hao walijikuta wakielea kwenye dimbwi la mahaba lenye kina kirefu, wakalala pamoja usiku kucha mpaka asubuhi ambapo Arianna aliwahi kuamka kuliko mtu mwingine yeyote na kuanza kumuandalia Msuya nguo alizotakiwa kuvaa siku hiyo.

Akazipiga pasi vizuri, akamsafishia viatu na kumuwekea kila kitu tayari kisha akatoka na kuelekea chumbani kwake kuendelea kupumzika. Msuya aliposhtuka usingizini, alifurahi sana kukuta kila kitu kimeshaandaliwa na Arianna, akaamka na kuelekea bafuni na muda mfupi baadaye akaanza kuvaa.

Japokuwa wafanyakazi aliowaajiri ndani ya nyumba hiyo walikuwa wakimfanyia kazi zote lakini uwepo wa Arianna ulimfanya Msuya ajihisi kuwa na amani kubwa ndani ya moyo wake. Lile tabasamu ambalo kwa kipindi kirefu lilitoweka kwenye uso wake, tangu alipofiwa na mkewe, sasa lilianza kuchanua upya kwenye uso wake kutokana na mapenzi ya dhati aliyokuwa akioneshwa na Arianna.

Baada ya kumaliza kujiandaa, alitoka mpaka kwenye chumba cha Arianna na kumkuta akiwa amejilaza kitandani, akichezea simu yake mpya. Akaingia na kumkumbatia kisha akambusu na kumshukuru kwa yote yaliyotokea tangu usiku uliopita mpaka asubuhi hiyo.

“Hizi pesa baadaye nitamtuma dereva aje kuwachukua awapeleke ‘shopping’ wewe na shemeji yangu Diego, nataka kukuona ukiwa na furaha,” alisema Msuya, Arianna akafurahi mno na kumbusu kwenye paji lake la uso, akatoka na kumsindikiza mpaka kwenye maegesho ya magari.

Tofauti na siku iliyopita, siku hiyo Msuya alichagua gari jingine la kisasa, Range Rover Evoque na kuondoka nalo, Arianna akamsindikiza kwa macho huku akimpungia mkono mpaka alipopotea kwenye upeo wa macho yake.

Kumbe kwa muda wote huo, Diego alikuwa akifuatilia kila kitu kilichokuwa kinaendelea kupitia dirisha la chumba chake, alipoona Msuya ametoka tu, harakaharaka naye alitoka mpaka nje na kumfuata Arianna.

“Vipi Diego, kwema?”
“Siyo kwema, nahitaji kuzungumza na wewe Arianna.”
“Basi huna haja ya ‘kupaniki’, twende ndani tukazungumze, hawa wafanyakazi wasije wakatuona bure wakamfikishia Msuya taarifa,” alisema Arianna kwa sauti ya upole, Diego akashusha pumzi ndefu huku akionesha kuwa na jazba, wakaingia mpaka ndani na kwenda moja kwa moja chumbani kwa Arianna.

“Hivi unanifanya mimi sina akili Arianna si ndiyo?”
“Kwani vipi Diego? Hebu punguza hasira tuzungumze.”
Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.

Comments are closed.