The House of Favourite Newspapers

The Angel Of Darkness – 26

Magaidi walioshambulia katika kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi, Kenya wanasababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa.

Baada ya Watanzania hao kufa, wanawaacha yatima watoto wao mapacha, Arianna na Brianna ambao kila mmoja anapitia maisha ya tofauti kabisa na mwenzake.  Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anabakia kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.

Kila mmoja anapitia mitihani ya aina yake maishani mwake. Brianna, yeye analelewa na familia ya kimaskini ya mzee Njoroge baada ya Mashango kufariki dunia kwa kugongwa na gari.

Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anatorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.

Akiwa Arusha, anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kutaka kuyabadilisha maisha yake. Wanakubaliana wamdanganye mfanyabiashara huyo kwamba wawili hao ni ndugu wa damu wakati ukweli ni kwamba wawili hao ni wapenzi.

Hatimaye wawili hao wanahamia kwenye jumba la kifahari la Msuya. Mapenzi kati ya Arianna na Msuya yanaanza kukolea, jambo linalosababisha Diego awe kwenye wakati mgumu sana kihisia kutokana na wivu uliokuwa ukimsumbua kila kukicha.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Hivi unanifanya mimi sina akili Arianna si ndiyo?”

“Kwani vipi Diego? Hebu punguza hasira tuzungumze.”

“Tuzungumze nini? Unataka kuzungumza nini na mimi,” alisema Diego huku akimsogelea mwilini Arianna, mishipa ya hasira ikiwa imesimama kichwani mwake.

“Kwani mimi kosa langu ni lipi?”

“Ina maana hujui kosa lako Arianna? Tulikubaliana tumekuja hapa kufanya kazi lakini mbona wewe unaanza kuchanganya mapenzi na kazi?”

“Kivipi Diego mbona sikuelewi?”

“Umeanza kumpenda Msuya, haiwezekani umfanyie vitu ambavyo hata mimi hujawahi kunifanyia. Na mimi nina moyo na nasikia maumivu, kwa nini unacheza na hisia zangu?” alisema Diego, Arianna akashusha pumzi ndefu na kumtazama Diego usoni.

“Punguza wivu Diego, mimi ni wako na hakuna kinachoweza kunibadilisha.”

“Umeshaanza kubadilika Arianna, au kwa sababu mimi sina pesa?” Diego aliendelea kulalama, ikabidi Arianna aanze kumtuliza. Akamkumbatia kimahaba na kumbusu kwenye paji la uso, akawa anaendelea kumpa maneno matamu yaliyosababisha kijana huyo atulie.

Kama kawaida yao, Diego alitoa Cocaine na bomba la sindano, wakajifungia mlango na kujidunga mpaka kila mmoja ‘alipokolea’, wakajikuta wakiwa kitandani wakilisakata kabumbu katika mechi ya kirafiki isiyo na refa wala jezi.

Baadaye Diego alitoka bila kuonekana na mtu yeyote na kumuacha Arianna akiwa hajitambui kwa usingizi mzito uliosababishwa na madawa aliyojidunga sambamba na uchovu wa mechi ya kirafiki kati yake na Diego.

Kama ilivyokuwa kwa siku iliyopita, Arianna alishinda kutwa nzima akiwa amelala fofofo. Alikuja kuzinduka majira ya saa kumi na mbili jioni, akaenda kuoga na kurudi chumbani kwake ambako alificha ushahidi wote wa bomba la sindano na mabaki ya madawa ya kulevya kwani alikuwa na uhakika kwamba Msuya akirudi lazima aende chumbani kwake kumsalimu.

Alichokihisi ndicho kilichotokea kwani muda mfupi baadaye, alisikia mlango wa chumba chake ukigongwa kisha Msuya akaingia na kumkuta Arianna akiwa amejilaza kitandani. Kwa mahaba makubwa alimkumbatia na kumbusu kwenye paji la uso, Arianna akawa na kazi ya ziada kujificha ili Msuya asimshtukie kwamba alikuwa amelewa.

Kisingizio chake kiliendelea kuwa kilekile, kwamba bado anaumwa ndiyo maana alikuwa kwenye hali hiyo. Msuya hakutaka kumhoji sana, akamuacha apumzike, yeye akaelekea chumbani kwake. Chakula cha usiku kilipoandaliwa, Msuya alimfuata Arianna chumbani na kutoka naye mpaka sebuleni, wakajumuika na Diego ambaye muda wote alikuwa kimya.

Siku hiyo ilipita, maisha yakawa yanazidi kusonga mbele huku Diego akizidi kumganda Arianna kama ruba. Ikawa kila Msuya akiondoka kwenda kazini na kuwaacha wawili hao nyumbani, lazima wajidunge madawa ya kulevya kisha wakutane kimwili mpaka kila mmoja aridhike. Kutokana na madawa aliyokuwa anatumia, Arianna hakuona ugumu wowote kuwaridhisha wanaume wawili kila siku kiasi kwamba haikuwa rahisi kwa Msuya hata kuhisi kwamba Diego alikuwa mume mwenzie.

Kadiri siku zilivyokuwa zinazidi kusonga mbele ndivyo mipango ya ndoa kati ya Arianna na Msuya ilivyokuwa inazidi kupamba moto ambapo wawili hao walikubaliana kufunga ndoa ya Kikristo itakayofuatiwa na sherehe kubwa ambayo bado walikuwa hawajaamua wataifanyia ukumbi gani.

Hali ilikuwa mbaya kwa Diego ambaye kadiri muda ulivyokuwa unasonga ndivyo wivu ulivyokuwa unamtesa ndani ya moyo wake. Japokuwa awali alikuwa anajitahidi kuizoea hali ya kuchangia mapenzi na Msuya, taarifa za wawili hao kufunga ndoa zilikuwa sawa na mkuki ndani ya moyo wake.

Aliamini yeye ndiye anayepaswa kuwa mume halali wa Arianna kwa sababu anamfahamu kwa undani na yeye ndiye aliyekuwa wa kwanza kumfahamu akiwa bado msichana mdogo kabisa.

Kwa jinsi Msuya alivyokuwa akijitahidi kumuonesha mapenzi mazito Arianna, alijua mwisho wake lazima msichana huyo atanogewa na kumsahau kabisa Diego, jambo ambalo hakuwa tayari kuona linatokea.

Kwa kuwa alikuwa anaujua udhaifu wa Arianna, alichokifanya Diego ni kuzidi kumuongezea dozi ya madawa ya kulevya, ikawa kila siku anaongeza kipimo cha madawa, hali iliyomfanya Arianna ambaye angalau sasa alikuwa na mwonekano mzuri kutokana na matunzo aliyokuwa anayapata, kuanza kurudi kwenye hali yake ya zamani.

Taratibu akaanza kupoteza tena hamu ya kula, hali iliyosababisha mwili wake udhoofike sana ndani ya kipindi kifupi. Akawa hawezi kufanya chochote zaidi ya kushinda kutwa nzima akiwa amelala, jambo ambalo lilianza kumpa wasiwasi Msuya.

“Kwani umepatwa na nini Arianna wangu jamani, naona unapungua sana uzito, muda wote unashinda umelala na hata uso wako umebadilika. Kwa kifupi umekuwa mtu mwingine tofauti kabisa na yule Arianna ninayemfahamu mimi,” Msuya alimuuliza Arianna jioni moja akiwa chumbani kwake baada ya msichana huyo kukataa kwenda kujumuika na wenzake sebuleni kwa maelezo kwamba hajisikii vizuri.

“Nahisi ile malaria bado haijaisha,” alisema Arianna kwa sauti ya kichovu.

“Sasa kama ni hivyo kwa nini unakuwa mgumu ninapotaka kukupeleka hospitalini ukafanyiwe vipimo vyote?”

“Hakuna haja ya kwenda hospitalini, nitapona tu Msuya wala usijali.”

“Unajua kwamba siku ya harusi yetu imekaribia sana, sasa kwa hali hiyo uliyonayo itakuwaje?”

“Nitakuwa sawa Msuya usijali,” alisema Arianna kwa tabu. Hata ule ukaribu kati ya wawili hao ulioanza kujengeka na kushamiri ndani ya siku chache tangu walipoanza kuishi pamoja, ulififia kwa kasi. Arianna akapoteza kabisa ule uchangamfu wake, akawa mzito wa kuzungumza na kufanya jambo lolote, hali iliyozidi kumuacha Msuya kwenye wakati mgumu.

Alichokifanya Msuya, ilikuwa ni kumtafuta daktari wake aliyekuwa akiitibu familia yake kwa kipindi kirefu, akaongozana naye mpaka nyumbani kwake akiwa na vifaa vyote kwa ajili ya vipimo. Msuya aliamua kufanya hivyo bila kumwambia Arianna kwa sababu alijua lazima ataleta kipingamizi.

“Arianna! Nimekuja na daktari inatakiwa akupime vipimo vyote ili tujue unaumwa nini,” alisema Msuya baada ya kuingia ndani kwake na daktari huyo. Arianna aliyekuwa amelala, akashtuka mno kupewa taarifa hizo, kijasho chembamba kikaanza kumtoka.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda.

Comments are closed.