The House of Favourite Newspapers

Kwa Chama Hili Yanga, Hamponi Ligi Kuu

0


YANGA haitaki masihara, tayari imekamilisha usajili wa baadhi ya wachezaji katika kuhakikisha wanafanya vema kwenye msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Baadhi ya wachezaji wa kigeni wameanza kutua nchini tayari kwa kuanza msimu ujao unaotarajiwa kuwa mgumu kutokana na kila timu kupania kufanya vema.Wakati Yanga wakiendelea na usajili mpya, tayari imeanza kutangaza kuachana na baadhi ya wachezaji ambao ni Mghana, Lamine Moro, Fiston Abdoulrazack huku pia Metacha Mnata akihusishwa kuwa njiani kutemwa.

 

Katika kuelekea msimu ujao, kikosi cha Yanga kinatarajiwa kuwa na mabadiliko makubwa na hiyo kutokana na idadi ya wachezaji wapya waliosajiliwa.Kikosi cha Yanga kinatarajiwa kuwa na maingizo mapya ya wachezaji saba ambao wote tishio ambacho kitakuwa hivi;

 

1. ERICK JOHORA
Ni kipa namba moja wa Aigle
Noir ya Burundi ambaye ni raia wa Tanzania na amejiunga Yanga kwa mkataba wa miaka miwili kama mchezaji huru anayekuja kuchukua nafasi ya Metacha Mnata ambaye hivi karibuni alisimamishwa na uongozi wa timu hiyo kwa utovu wa nidhamu.

2. SHABAN DJUMA
Anakuja kumpa
changamoto ya ushindani beki wa kulia Shomari Kibwana aliyejihakikishia namba katika kikosi cha kwanza akimuweka benchi Paul Godfrey ‘Boxer’ anayetajwa kutolewa kwa mkopo. Djuma tayari amesaini mkataba wa miaka miwili Yanga akitokea AS Vita ya DR Congo.

 

3. DAVID BRYSON
Beki wa zamani wa KMC
FC aliyejiunga na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili kama mchezaji huru, anakuja kuiongezea nguvu safu ya ulinzi ya kushoto, ujio wake huenda ukamuondoa Adeyum Saleh au Yassin Mustapha.

 

 

4. PARTENE COUNOU
Yupo katika hatua za
mwisho kukamilisha usajili wake kama mchezaji huru akitokea Al-Hussein SC ya nchini kwao Benin, aliwahi kuichezea Klabu ya Akwa United ya Nigeria. Anakuja kuchukua nafasi ya Mghana, Lamine aliyesitishiwa mkataba wake. Kwenye nafasi hii pia kuna beki mtemi kutoka DC Motema Pembe, Henock Inonga Banga ambaye amemalizana na Yanga.

 

5. DICKSON JOB
Yeye ataendelea kuwepo
katika kikosi cha Yanga, hiyo ni kutokana na kiwango kikubwa ambacho amekionyesha ambacho kimelishawishi benchi la ufundi la timu hiyo, linaloongozwa na Nasreddine Nabi ambaye tangu ametua nchini amekuwa akimtumia yeye mara nyingi.

 

6. MUKOKO TONOMBE
Kati ya wachezaji
walionyesha kiwango bora na kuthibitisha ubora wake ndani ya uwanja ajiunge na Yanga. Yeye ataendelea kuwepo katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

 

7. TUISILA KISINDA
Amepewa majina mengi tangu
ajiunge na Yanga katika msimu uliopita, hiyo ni kutokana na aina ya uchezaji anayoitumia kwa kucheza kwa kasi wakati akiwa anaukokota mpira na kati ya majina hayo aliyopewa ni Hussein Bolt ambaye ni mwanarihadha wa kimataifa.

 

8. FEISAL SALUM ‘FEI TOTO’
Bado yupo na ataendelea
kusalia katika kikosi cha kwanza cha Yanga, hiyo ni kutokana na ubora aliokuwa nao ambaye mara baada ya mchezo wa Ligi Kuu Bara wa Kariakoo Dabi, Rais wa Makampuni ya GSM, Gharib Salim Mohammed alimzawadia gari aina ya Toyota Athlete Crown.

 

9. HERITIER MAKAMBO
Amerejea tena katika kikosi
cha Yanga, tangu alipoondoka 2019 kuelekea Horoya AC ya Guinea. Ni kati ya wachezaji vipenzi vya timu hiyo na
anaingia moja kwa moja
kutokana na uwezo na ubora wake kufahamika, msimu wa 2018/19 alikuwa kinara wa mabao Yanga akitupia 17. Tayari amesaini mkataba wa miaka miwili.

 

10. FISTON MAYELE
Tayari yupo nchini huko
kwenye Kambi ya Yanga iliyopo Kijiji cha Avic Town, Kigamboni, amesaini mkataba wa miaka miwili. Amejiunga na Yanga kama mchezaji huru baada ya mkataba wake kumalizika AS Vita ya DR Congo.

 

11. JIMMY UKONDE
Naye yupo nchini na juzi
alikuwepo katika kikosi kilichocheza mchezo wa kwanza wa michuano ya Kagame wakati timu hiyo ilipocheza dhidi ya Big Bullets ya nchini Malawi, uliomalizika kwa sare ya bao 1-1. Nyota huyo anajiunga na timu hiyo akitokea UD Songo ya Msumbiji. Ana kasi, mzuri kwenye chenga na anaweza kutengeneza nafasi nyingi.

STORI NA WILBERT MOLANDI

Leave A Reply