The House of Favourite Newspapers

Adui wa Maisha Yako ni Wewe!

0

Watu wengi wanapata madhara makubwa katika maisha yao kutokana na kuishi maisha ya kujikosea wenyewe.

 

“Amenionaje mpaka ameamua kunisaliti?” Huu ni mfano wa makosa ya kujikosea mwenyewe, kwani kujiuliza maswali ya namna hii hukaribisha majibu yanayoumiza zaidi kuliko tukio lenyewe.

 

Nikukumbushe mapema kuwa, adui mkubwa wa maisha yetu ni mawazo yetu. Tukimudu kuyashinda, tumeyashinda maisha yote.

 

Wanasema: “Lile aliwazalo mjinga ndilo linalomtokea.” Ninaposema kujikosea ni namna tunavyozichukulia changamoto za maisha yetu na kuishia kuona kama hatustahili kuzipata au tunaonewa nazo.

 

Nirejee mfano nilioutoa wa mtu ambavyo hufikiria pale anaposalitiwa. Wengi hujipa majibu ya kudharauliwa na kujivika udhaifu wakati mwingine siyo ukweli wa dhambi walizofanyiwa.

 

Kufikiri kwamba mkeo anakusaliti kwa sababu huna fedha ni kujikosea, kwa sababu wapo wanaume wenye fedha nyingi lakini wake zao wanawasaliti.

 

Ukijihukumu kwamba mke anakudharau kwa sababu una kasoro fulani, kumbuka kuna watimilifu wa mambo mengi lakini pia wanadharauliwa tena kwa viwango vikubwa.

 

Ndugu yangu; maisha ni foleni unaposimama na kutazama walio mbele yako usisahau kugeuka; utawaona wengi wako nyuma yako wanatamani kusimama mahali ulipofika.

 

Kujikosea ni tatizo kubwa linalowakabili wengi na ukitazama madhara mengi hutokea pale mtu anapojiona si kitu katika maisha yake ingawa katika hali ya kawaida hakuna sura halisi ya wao kudunishwa na wengine au changamoto wanazokutana nazo; wanajikosea wenyewe.

 

Nikukumbushe; kila lililokuumiza na litakalokuumiza katika maisha yako linatokana na fikra zako namna zinavyokosea tafsiri mambo kwa kukukandamiza au kukupa unyonge ambao pengine haupo!

 

Kwa mfano, mtu anapokutukana, kukukashifu ni jukumu lako kupitia mawazo yako kuamua kuhuzunika au kufurahi.

 

Ukiambiwa ‘huna akili’ na ukajikosea kwa kuamini hivyo; hata kama unazo akili nyingi na watu wanakutegemea utaumizwa sana na neno hilo.

 

Lakini ukiambiwa ‘wewe una sura mbaya’; ukakataa kujikosea na kuamini kuwa, wewe ni mzuri utakuwa mzuri miongoni mwa wazuri  na kashfa hiyo haitakuumiza kabisa.

 

Naamini nikisema hivi utakuwa unanielewa vizuri. Pengine unaweza kuniuliza, unawezaje kuacha kujihukumu katika dunia hii yenye changamoto na matatizo mengi?

 

Njia pekee ya kuweza kukoma kujikosea mwenyewe ni ‘KUJIPENDA’. Kuwa mwenye thamani wa kwanza miongoni mwa wenzako na uamini kuwa huna mbadala wako.

 

Ukiishi kwa kujipenda, fikra zako zote zitakuwa ni kujifurahisha hata kama umezungukwa na matatizo mengi kiasi gani na imani yako itaishi na wewe katika msemo huu. “YOTE YATAPITA.”

 

Faida kubwa ya kuepuka kujikosea na kuishi kwa imani ya ‘yote yatapita’ kutakusaidia kukuongezea nguvu ya kushinda matatizo yako.

 

Moyo uliovunjika ni sawa na Simba aliyekufa. Simba aliyekufa ataogopwa akitazamwa kwa mbali lakini akisogelewa atachezewa mkia hata na watoto wadogo.

 

Tukiishi maisha ya kujikosea wenyewe, watu wanaweza kutuona kwa mbali kama wenye thamani lakini kumbe ni wafu tunaoweza kuchezewa kimaisha hata na tatizo la kukosa kiberiti ndani ya nyumba.

Leave A Reply