The House of Favourite Newspapers

Waziri Alipokiri Kuwa Mchawi-29

0

ILIPOISHIA WIKIENDA
Baada ya polisi huyo kufanya marekebisho, alikwenda kumfahamisha mkuu wa kituo ambaye alitoka ofisini kwake akiwa ameshika lile kadi la gari langu.
“Umekuja na funguo ya lile gari?” akaniuliza.

“Ndiyo ninayo.”
“Twende nikakukabidhi.”
Mimi na mkuu huyo wa kituo tulitoka nje na kwenda lilipokuwa gari hilo.

Tulilikagua gari hilo kwa pamoja kisha nikajaribu kuliwasha. Gari liliwaka bila tatizo.
“Sasa mheshimiwa kama umeshatoa maelezo yako unaweza kuchukua gari lako, tutakapokuhitaji tutakuita,” Mkuu huyo wa kituo akaniambia.
SASA ENDELEA…

“Sawa.”
Nilimuita yule dereva wa gari hilo nikamwambia alipeleke nyumbani kwangu.
“Tafadhali usimueleze kitu chochote mke wangu,” nikamwambia.
Wakati namwambia hivyo, mke wangu akanipigia simu hapohapo.
“Hello… mke wangu niaje?” nikamuuliza.

“Umeondoka na gari gani?”
“Nimeondoka na gari lako. Gari la ofisini limepelekwa gereji lakini tayari nimempa dereva akuletee,” nikamdanganya.

“Huyo dereva mlikutana wapi?”
“Nilimpigia simu kumuita ofisini kwangu, atakuja nalo sasa hivi.”
Nikajua kwa tabia ya mke wangu angeniuliza swali Lingine, nikawahi kumkatiza:
“Tutaonana mchana.”
Kabla hajajibu chochote nikakata simu.

“Sasa nenda nalo hili gari,” nikamwambia yule dereva ambaye alijipakia kwenye gari hilo. Na mimi nikaenda kujipakia kwenye gari la serikali. Tukaondoka.
Wakati gari likiwa katika mwendo, badala ya kufadhaika kutokana na matukio yaliyotokea, nilijikuta nikifurahi kwa kuona kuwa nimeweza kuwadanganya polisi pamoja na kumdanganya mke wangu na kulimaliza tatizo langu.

Kwa hapo nilijiona mjanja kama sungura. Sikuwa nikifikiria kwamba kutakuja siku ambayo nitakwama.
Nilikuwa nikiamini kuwa japo nilivurumishwa nyumbani kwa waziri mkuu, uchawi nilioufanya utawezesha kumfukuzisha kazi waziri huyo mtu mzima aliyekwishapita umri wa kustaafu.

Nikajiambia kama rais angejua, asingeweka waziri mkuu wa umri ule ambaye kichwa chake hakina tena jipya zaidi ya kurudia yaleyale.

Ili kuwa na serikali imara, nilizidi kujiambia. Rais alitakiwa kuteua waziri mkuu kijana ambaye fikira zake zinaendana na wakati, si yule ambaye fikra zake zimepitwa na wakati.

Watu wa umri ule ndiyo wale ambao kila siku wanawaagiza mgambo kupambana na wafanyabiashara ndogondogo badala ya kulitafutia ufumbuzi tatizo lao.
Na kwa hapa nchini kwetu ni mimi peke yangu mwenye sifa za kuwa waziri mkuu, nikajiambia.

Kutahamaki gari lilikuwa limeshasimama katika eneo la maegesho mbele ya jengo la wizara yangu. Nilifungua mlango nikashuka na kuingia katika mlango mkuu wa jengo hilo. Nilikuwa nimechelewa sana kufika kazini kutokana na muda mwingi kuupoteza kituo cha polisi. Lakini kwa vile mimi mwenyewe ndiye niliyekuwa bosi wa wizara, sikujali sana kwa kujua hakukuwa na mtu yeyote wa kunihoji chochote.

Nilipoingia ofisini mwangu nilichapa kazi hadi saa tano ambapo nilianza kusikia habari za tukio la usiku uliopita nyumbani kwa waziri mkuu likizungumzwa na wafanyakazi.
Na mimi nilijidai kuuliza ili nielezwe ni nini kimetokea nyumbani kwa waziri mkuu.

Nikaelezwa kwamba kulikuwa na kichaa aliyeingia nyumbani kwa waziri mkuu na kukita kimba la kinyesi mbele ya mlango kabla ya kuvurumushwa na polisi waliokuwa wakilinda nyumba hiyo.

Lakini baadhi ya wafanyakazi hao walikuwa wakihoji polisi hao walikuwa wapi hadi kichaa huyo akapita kwenye geti. Walikuwa wakishauri kuwa polisi hao wangekamatwa kwa kosa la uzembe kwani kama kichaa huyo angefanikiwa kuingia ndani kabisa angeweza kusababisha madhara.

Mimi nilikuwa nikiyasikiliza tu yale mazungumzo nikijifanya kama nilikuwa sijui lolote.
Nilitarajia labda habari ya kukamatwa kwa gari langu ingeelezwa lakini sikuisikia.
Ilipofika saa sita mchana mke wangu akanipigia simu. Kadiri ile mimba yake ilivyokuwa inazidi kukua, tabia yake nayo ilikuwa inabadilika kidogokidogo. Kila wakati alikuwa ananipigia simu hata kama hatakuwa na neno la maana la kuniambia.

Pia amekuwa mkali na kupenda kuhoji vitu hata visivyomhusu. Nikaipokea haraka simu yake kwa kujua kuwa kama ningechelewa kuipokea, ingekuwa sababu ya kuanza kugomba.

“Hello my darling…!” nikamwambia.
“Utarudi saa ngapi?” akaniuliza swali hilo kwa jazba.
“Kwa nini unaniuliza hivyo?”
“Kwa nini nisikuulize, mimi si mke wako? Unataka akuulize nani?”
Je, nini kiliendelea? Usikose kufuatilia kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda siku ya Jumatatu.

Leave A Reply