The House of Favourite Newspapers

Kuelekea Tamasha la Mjue Mtunzi; Upande wa Pili wa Mtunzi Joseph Shaluwa

0
Joseph Shaluwa, Mwandishi wa Habari na Mtunzi

 

SANAA ya filamu na muziki wa kizazi kipya ni miongoni mwa sanaa zenye nguvu na zinazojulikana na wengi zaidi hapa nchini. Ukimtaja Ali Kiba, Diamond, Ray, Jux, Zuchu, JB, Kajala, Wolper na majina kama hayo yanajulikana kwa kasi zaidi.

 

Lakini kuna upande wa pili wa utanzu wa Fasihi Andishi, ambapo humu kuna vichwa vingi vinavyofanya vema kwenye medali hiyo. Isivyo bahati thamani na heshima yao haikuzwi au haiwekwi kwenye mzani unaotakiwa katika jamii.

 

Kwa uchache ukiambiwa utaje majina ya watunzi wa riwaya wa kizazi cha sasa, huwezi kuacha jina la Joseph Shaluwa. Huyu ni mwandishi mahiri ambaye ameanzia kuandika katika magazeti Pendwa kwa miaka mingi.

 

Hussein Tuwa, Mtunzi na Rais wa Uwaridi

 

Amepitia kampuni mbalimbali, lakini amefanya kazi kwa muda mrefu zaidi katika Kampuni ya Global Publishers Ltd, ambayo ipo chini ya Eric Shigongo, ambaye kwa sasa pia ni Mbunge wa Jimbo la Bushosa, Mwanza.

 

Mpaka sasa, Shaluwa anaandikia Gazeti la Championi Ijumaa, riwaya yake inayoendelea sasa inaitwa Kengele ya Mazishi.

 

Katika kutafuta thamani yake, Shaluwa aliamua kujiunga na Umoja wa Waandishi wa Riwaya Wenye Dira (Uwaridi) tangu mwaka 2015 ili kuunganisha nguvu katika kutetea masilahi ya watunzi wa riwaya nchini Tanzania.

 

UWARIDI chini ya Rais wake, Hussein Issa Tuwa, imeshafanya mengi kwa jamii – waandishi wenyewe – na kwa wapenzi wa riwaya nchini. Taasisi hiyo ilibuni tamasha ambalo huwakutanisha waandishi wa riwaya na mashabiki wao kila mwaka.

 

Prof. Adolf Mkenda, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia

 

Tamasha hilo lililopewa jina la MJUE MTUNZI, kwa mara ya kwanza lilifanyika Februari 23, 2020 katika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shule ya Sayansi na Teknolojia, Sayansi – Kijitonyama, jijini Dar es Salaam.

 

Huu ni msimu wa pili, ambapo mwaka jana lilipumzishwa kwa sababu ya janga la ugonjwa wa UVIKO 19. Katika tamasha la mwaka huu, litafanyika Julai 3, 2022, siku ya Jumapili katika Ukumbi wa NSSF – MAFAO HOUSE, Ilala – Boma jijini Dar es Salaam.

 

Mwandishi Joseph Shaluwa ni miongoni mwa watunzi watakaozindua vitabu vyao vipya siku hiyo.

Hapa amezungumza nami na kueleza kuhusiana na maisha yake binafsi kwa uchache lakini zaidi kuhusiana na tamasha lao hilo.

 

JOSEPH SHALUWA NI NANI?

“Ni mume wa Upendo – baba wa watoto wanne – Ben, Kelvin, Eric na Erica. Ni mtunzi wa riwaya, mwandishi wa habari na mtaalamu wa Saikolojia a Uhusiano.

 

“Nimezaliwa Moshi, mkoani Kilimanjari lakini asili yangu ni Mnyiramba wa Mkalama, Singida. Kwa sasa ninaishi na kufanya kazi jijini Dar es Salaam.”

 

UMESHATOA VITABU VINGAPI?

“Nimeandika vitabu vingi sana, lakini vilivyochapishwa mpaka sasa ni 22, hiki cha HILIKI YA TUNU ambacho kinakwenda kuzinduliwa Jumapili hii ni cha 23.

 

“Vitabu vingine vya hivi karibuni ni MAISHA YA NDOA, CHORATA, WINO MWEKUNDU, MOYO WANGU UNAUMA na MATEKA UGHAIBUNI.”

 

UNAWEZAJE KUTENGA MUDA WA KUTUNGA RIWAYA NA FAMILIA?

“Ni rahisi sana, ni suala la kujipanga. Mfano zaidi ya kuandika riwaya, pia naimba Kwaya Kuu, kanisani kwetu. Nafanya biashara na ujasiriamali pia.

 

“Nafundisha vijana katika shule za msingi na sekondari kuhusiana na elimu rika na kujitambua. Yote haya ni kwa sababu ya kutenga muda.

 

“Jambo la msingi ni kufanya kitu unachokipenda. Niseme ukweli nafurahia sana ninachokifanya, ndiyo maana napanga ratiba yangu vizuri.”

 

HEBU NIAMBIE, UWARIDI NI NINI?

“Ni Umoja wa Waandishi wa Riwaya Wenye Dira Tanzania – UWARIDI. Tunaongozwa na Hussein Tuwa kama Rais wetu, Katibu Mkuu Ibrahim Gama, Katibu Mwenezi, Maundu Mwingizi na Mhazini, Lilian Mbaga.

“Ni umoja unaosimamiwa na wanachama wenyewe. Unawasaidia watunzi kujitambua, kutambulika na kuthaminiwa katika jamii ya wasoma vitabu. Mfano mzuri ni hili tamasha letu la Mjue Mtunzi. Kwa hakika linatuheshimisha watunzi.”

 

UNAWEZA KUZUNGUMZIAJE TAMASHA LA MJUE MTUNZI?

“Naishiwa maneno lakini niseme, linazidi kupanda hadhi mwaka hadi mwaka. Angalia… ni mwaka wa pili huu tunafanya, lakini kuna hatua kubwa tumepiga.

 

“Kwanza mgeni rasmi ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Adolph Mkenda, MC wetu mwaka huu ni wa viwango vya juu, mkongwe Taji Liundi lakini pia hata ukumbi wetu – ni wa hadhi ya juu zaidi.

 

Shaluwa akiwa na baadhi ya washiriki wa Tamasha la Mjue Mtunzi 2020

 

“Ni full kiyoyozi, nawashauri watu waje na makoti yao, maana siyo kwa ubaridi ule! Mwenyewe nimeshakwenda mpaka pale NSSF na nimeshuhudia ‘mufindi’ ulipo mle ndani. Ni tamasha zuri, la kistaarabu.

 

“Lakini hata mdhamini wetu ni mkubwa na mdau wa vitabu nchini. Tumedhaminiwa na Elite BookStore. Kwahiyo unaweza kuona ni kwa namna gani, ni tamasha lenye hadhi ya juu.”

WATU WATARAJIE NINI KWENYE TAMASHA HILO?

“Kwanza dhamira kubwa ni kuwakutanisha na watunzi wao. Kutakuwa na watunzi watatu watakaokaa kwenye kiti cha siku ambao wataelezea maisha yao na baadaye watajibu maswali.

 

“Kama mtakumbuka mwaka 2020, walikuwa ni Hussein Tuwa, Lilian Mbaga na Lelo Mmasy. Kwa kawaida huwa watunzi wawili wanatoka ndani ya Uwaridi na mmoja nje ya Uwaridi. Je, mwaka huu ni kina nani? Hiyo ni big surprise. Ufike tu NSSF Ilala, Jumapili.

 

“Kuna matukio ya kupiga picha kwenye zulia jekundu, lakini pia huwa kuna soko kubwa la vitabu siku hiyo. Kutakuwa na meza nyingi za wauza vitabu ambao wamekubaliwa kufanya hivyo na uongozi, hivyo basi, andaa tu pesa yako ya vitabu.”

 

HILIKI YA TUNU KI KITABU CHA NAMNA GANI?

“Ni Love Story kali sana, ambayo imeandikwa kiu-uzima. Kwa kweli kinawafaa watu wazima tu na hasa wanandoa. Ingawa kimeandikwa katika ufundi, kikiwa na mapenzi sana, lakini lengo ni kuelimisha wanandoa.

 

“Ni stori tamu, ndefu lakini isiyochosha. Fikiria ni kitabu cha kurasa 510. Siyo cha kawaida. Watu wajipange kukipata kitabu hicho kuanzia Jumapili, siku ya Mjue Mtunzi.”

 

VITABU VYAKO UNACHAPIA WAPI?

“Kwa muda mrefu nilikuwa nachapiwa na wachapaji tofauti tofauti kwa bei kubwa, lakini kwa sasa nachapa mwenyewe kwa gharama nafuu sana. Ninayo kampuni ya uchapaji, ambayo pia tunapokea kazi za waandishi wengine.

 

“Bei yetu ni rafiki sana na kazi zetu ni bora. Unapata kazi yako ndani ya muda mfupi sana. Nawakaribisha waandishi wenzangu JOPASHA PRODUCTION tufanye kazi. Hata ukiwa na mtaji wa laki moja tu, kwetu unachapiwa kitabu.”

 

WASOMAJI WATAKUFIKIAJE?

“Napatikana sana mitandaoni kwenye kurasa zangu, nikitumia jina la Joseph Shaluwa (Facebook) au kwenye ukurasa wangu wa simulizi za joseph shaluwa (Facebook), @josephshaluwa (Instagram) na @Joseph Shaluwa (Twitter).

 

“Kazi zangu zinapatikana kwenye Gazeti la Championi Ijumaa, Jarida la Jahazi (kwenye meli na boti za Kilimanjaro – zinazofanya safari za Dar – Unguja – Pemba na  Jarida la Twiga – Inflight Magazine, linalopatikana kwenye ndege za Air Tanzania.) Zaidi ni kwenye vitabu vyangu.”

 

KITABU HIKI KITAPATIKANA VIPI?

“Kwanza siku ya uzinduzi, lakini baadaye vitaanza kuuzwa katika Duka la Kona ya Riwaya – Kinondoni Block 41, Come & Read BookStore – Ununio na Kwa George – Posta Mpya. Mikoani vitabu vinatumwa kwa gharama nafuu. Kwa mawasiliano zaidi, wasomaji wanifuate kwenye kurasa zangu za mitandao ya kijamii kwa ufafanuzi zaidi.”

Leave A Reply