The House of Favourite Newspapers

The angel of darkness-44

2

Magaidi walioshambulia katika kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi, Kenya wanasababisha vifo vya watu wengi, wakiwemo Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa.

Baada ya Watanzania hao kufa, wanawaacha yatima watoto wao mapacha, Arianna na Brianna ambao kila mmoja anapitia maisha ya tofauti kabisa na mwenzake. Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anabakia kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.

Kila mmoja anapitia mitihani ya aina yake maishani mwake. Brianna, yeye analelewa na familia ya kimaskini ya mzee Njoroge baada ya Mashango kufariki dunia kwa kugongwa na gari.

Kwa upande wa Arianna, yeye anaharibikiwa kabisa kimaisha na kuwa mtumiaji mkubwa wa dawa za kulevya, anatorokea Arusha akiwa na Diego, kijana aliyekuwa akifanya biashara ya madawa ya kulevya.

Akiwa Arusha, anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kutaka kuyabadilisha maisha yake. Mfanyabiashara huyo anamuoa Arianna na kumchukua na Diego pia kwenda kuishi naye kwenye jumba lake la kifahari bila kujua kwamba wawili hao walikuwa wapenzi.

Siku chache baada ya ndoa, Arianna anagundua kwamba amenasa ujauzito lakini anapopiga hesabu, anagundua kuwa mhusika wa ujauzito huo si mumewe Msuya bali ni Diego, jambo linalomchanganya sana.

Anajikuta akizidi kuharibikiwa kimaisha na sasa anashirikiana na Diego kutaka kumuibia Msuya kisha kutoroka pamoja. Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

“Asubuhi ilibidi niende kliniki, alinipeleka kaka Diego,” Arianna alijihami kwa kuongea uongo, Msuya akatingisha kichwa kuonesha kukubaliana naye lakini akarudia kumsisitiza kwamba muda wowote anapojisikia vibaya, ni bora apige simu ili mumewe ndiyo ampeleke hospitali.

“Sawa nimekuelewa mume wangu, nakupenda sana mwenzio na kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele naona hata mwanao naye anazidi kukupenda,” alisema Arianna huku akilishika tumbo lake, Msuya akapiga magoti kwa furaha na kulibusu tumbo la Arianna.

“Safari yangu ya kuelekea New York ni keshokutwa kama nilivyokwambia.”
“Mh! Jamani mume wangu, nitakukumbuka mwenzio, nimeshazoea kukuona kila siku, nitaishije?”
“Usijali, sitachelewa kurudi, wiki moja tu baadaye nitakuwa nimesharudi. Unataka nikuletee zawadi gani?” alihoji Msuya lakini Arianna hakumjibu. Akili zake zilikuwa zikifikiria kitu kingine tofauti kabisa.

Aliamini siku saba zinawatosha sana kufanya kila walichopanga na Diego na kutokomea kusikojulikana.
“Mbona kama una mawazo? Nakuuliza unataka nikuletee zawadi gani?” alihoji tena Msuya na kumfanya Arianna azinduke kutoka kwenye dimbwi la mawazo, ikabidi avunge kwamba alikuwa akijisikia uchungu mkali ndani ya moyo wake, Msuya akaanza kumbembeleza bila kujua kwamba mwenzake alikuwa akimsanifu.

Siku hiyo ilipita, kesho yake Msuya alianza maandalizi ya safari yake ya nje ya nchi, muda mwingi akawa bize kuhakikisha mipango yote ya safari inakamilika.

“Kesho ndiyo anasafiri, kazi itabaki kwetu,” alisema Arianna kwa sauti ya kunong’ona wakati akizungumza na Diego kwenye korido ya kuingilia ndani. Diego alitingisha kichwa kuonesha kuelewa alichoelezwa, kila mmoja akaendelea na kazi zake.Maandalizi yaliendelea na hatimaye kila kitu kikakamilika, kilichokuwa kinasubiriwa ikawa ni muda wa Msuya kuondoka tu.

“Nakuomba usijisikie vibaya mpenzi wangu, nitarudi mapema na nitakueletea zawadi nzuri ambayo naamini utaipenda. Nakuomba ujitunze na unitunzie mwanangu,” alisema Msuya kwa hisia nzito huku akimbusu Arianna sehemu mbalimbali za mwili wake hasa tumboni, msichana huyo akaendelea ‘kuekti’ kwamba alikuwa na huzuni kubwa kutokana na mumewe kutaka kusafiri na kumuacha peke yake.

Usiku huo ulipita huku Msuya akitumia muda mrefu kumbembeleza mkewe. Kesho yake asubuhi, familia nzima ilijiandaa na safari ya kumsindikiza Msuya uwanja wa ndege ikaanza. Walipofika uwanjani hapo, Msuya alikamilisha taratibu zote na kuagana na mkewe, Arianna, Diego na wanaye waliokuwa wameongozana na mfanyakazi wa ndani wa nyumbani kwake.

Wote wakampungia mikono wakati akiingia ndani ya jengo la uwanja huo. Walipohakikisha amepotea kwenye upeo wa macho yao, wote walirudi kwenye gari na safari ya kurejea nyumbani ikaanza huku Arianna na Diego wakionesha kuwa na furaha kubwa ndani ya mioyo yao.

Kwa kuwa hakukuwa na ndege kubwa inayosafiri kutoka jijini Arusha kwenda jijini New York, Marekani, ilibidi Msuya asafiri mpaka jijini Nairobi alikoenda kubadilisha ndege na kupanda kwenye Airbus 380, mali ya Kampuni ya KLM (Koninklijke Luchtvaart Maatschappij) ya Uholanzi na safari ya kuelekea jijini New York ikaanza.
***
Vuguvugu la ujambazi lilizidi kushamiri kwenye mpaka kati ya Tanzania na Kenya na kusambaa kwenye eneo lote la Jiji la Arusha ambapo watu wanaosaidikiwa kuwa raia wa Somalia, waliokuwa wakipenya kupitia mpaka wa Namanga, walikuwa wakiendesha vitendo vya uporaji mabenki, maduka ya kubadilishia fedha na utekaji wa magari.

Jeshi la polisi lilikuwa na kazi kubwa ya kudhibiti wimbi hilo la ujambazi huku changamoto kubwa ikiwa ni ubora wa silaha walizokuwa wanatumia majambazi hao ukilinganisha na zilizokuwa zinatumiwa na polisi. Ilibainika kuwa wengi wao hutoroka na silaha za kivita nchini Somalia ambako machafuko ya wenyewe kwa wenyewe yalikuwa yamepamba moto na silaha hizo ndizo zilizokuwa zikitumika pia kwenye ujambazi.

Oparesheni za jeshi la polisi za kushtukiza zilikuwa zikifanyika mara kwa mara na kufanikiwa kuwanasa Wasomali wengi ambao baada ya kukamatwa walikuwa wakiwekwa mahabusu kwenye Kituo Kikuu cha Polisi mkoani humo.

“Tutahakikisha tunapambana na wimbi hili la ujambazi na kuutokomeza kabisa. Tunawaomba wasamaria wema wenye taarifa zinazoweza kutusaidia kuwanasa wahusika, watupe nasi tutazifanyia kazi,” Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha alikuwa akizungumza na waandishi wa habari, habari ambayo ilirushwa na karibu vituo vyote vya runinga.

“Unaona wanaume wanavyoitetemesha nchi?” Diego alimwambia Arianna wakiwa wameketi sebuleni, muda mfupi baada ya kumsindikiza Msuya, wote wakacheka na kugongesheana mikono.
“Hivi unaonaje na sisi huu mchongo wetu tuutengeneze kwa namna ambayo itakuwa rahisi watu kuhisi kwamba tumevamiwa na majambazi na kuporwa? Hata Msuya hawezi kuelewa.”

“Mh! Wazo zuri lakini linahitaji umakini wa hali ya juu, si unaona polisi walivyochachamaa? Tusije tukaingizwa kwenye mkumbo tukaonekana tunashirikiana nao bure!”

“Shaka ondoa, niachie mimi nitalishughulikia hilo suala, we endelea kuweka mambo sawa kwa kukusanya kila kitu unachoona kitatufaa na mimi ngoja nitengeneze mazingira ili siku tukiondoka ionekane tumevamiwa na majambazi,” alisema Diego wakati akijadiliana na Arianna kwa sauti ya chini, wakapeana saa ishirini na nne kila kitu kiwe kimekamilika.

Baadaye Arianna alienda chumbani kwao ambako alichukua begi la mumewe ambalo lilikuwa tupu, akalifungua na kuliweka juu ya kitanda, akafungua droo ya kitanda na kuanza kutoa fedha na madini ya Tanzanite ambayo mumewe alikuwa ameyahifadhi. Alipomaliza kutoa kwenye droo moja, alihamia kwenye nyingine, akasomba fedha zote, madini pamoja na bastola ya mumewe na kuviweka kwenye begi.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

2 Comments
  1. alex rodrick says

    naona kabisa maisha ya taabu yanaanza kuwanyemelemea ktk maisha ya,Diego,na Arriana na furaha ya muda mfupi jkiwakabili haya tusubili……..

  2. devotha gervas says

    mbona briana ha2mwoni au amekufa tayar

Leave A Reply