The House of Favourite Newspapers

Waziri Alipokiri Kuwa Mchawi-39

1

ILIPOISHIA WIKIENDA
Nikanyamaza tena kwa sababu alichosema kilikuwa ni cha ukweli na ukweli ukidhihiri, uongo hujitenga.
“Leo atachukuliwa mtoto na kesho nitachukuliwa mimi, bora nijiepushe mapema. Naenda kwetu.”
SASA ENDELEA…

Akilini mwangu nilikuwa nawaza jinsi ya kuepukana na aibu ile. Mke wangu akiondoka pale nyumbani atakwenda kuyaeleza yale mambo kwa wazazi wake. Dar es Salaam ni kama hii, umbeya mwingi. Keshokutwa tu nitajikuta nimeandikwa magazetini kuwa nimekimbiwa na mke wangu kwa uchawi.
Je nitasalimika kufukuzwa kazi kama rais atasoma habari hizo? Nikajiuliza.

Huenda rais asiamini habari za magazeti, anaweza kumuita mke wangu ikulu na kumuuliza ukweli wa habari hizo na mke wangu kwa sababu ya hasira akamueleza kila kitu.
Hapo nitakuwa nimekwisha!

Nikajiuliza nifanye nini ili niweze kuepukana na fedheha ambayo ingeweza kunitokea pindi mke wangu akiondoka hapo nyumbani kwa hasira.
Kwa vyovyote vile, nilijiambia, nisingeweza kumzuia mke wangu kuondoka pale nyumbani kwa sababu alikuwa ameshapata hofu. Kuondoka kwake kulikuwa muhimu. Na hata mimi niliona aondoke tu kwa ajili ya kumuokoa mtoto wetu ingawa sikuwa na uhakika kuwa huko aendako angesalimika.

Wakati nikiwaza hayo, mke wangu alikuwa ameingia chumbani. Baada ya muda kidogo alitoka akiwa ameshika begi lake lililokuwa limejaa nguo.
Nilihisi lilikuwa na nguo zake na za mtoto.
Hii ni safari isiyo na marejeo! Nikajiambia kimoyomoyo.

Mke wangu alielekea kwenye mlango wa kutokea nje. Nikamuuliza:
“Ulikuwa ukizungumza na nani kwenye simu?”
“Nilizungumza na mama na pia nilimuita dereva aje anichukue.”
“Mama yako ulimueleza nini?”

“Nilimueleza kuwa ninarudi kwake.”
Mke wanagu akagundua ufunguo haukuwepo kwenye mlango.
“Njoo unifungulie mlango,” akaniambia.

Nikanyanyuka nilipokuwa nimeketi nikamfuata kwenye mlango.
“Sasa huyo mama yako ulimueleza sababu gani zinazokurudisha?” nikamuuliza tukiwa kando ya mlango.
“Nilimueleza kila kitu, kwa nini nimfiche?”
“Ulimueleza kuwa mimi ni mchawi?”

“Hebu nifungulie mlango!” Mke wangu akaniambia kwa sauti kali akikwepa kujibu swali langu.
Baada ya msichana huyo kugundua kuwa nilikuwa mchawi, hata ile nidhamu na mimi alikuwa hana tena. Kweli mchawi si mtu wa kuheshimika popote hata akiwa waziri!
Mchawi siku zote huonekana ni mtu dhalili tu.

Nilianza kushuhudia mwenyewe heshima yangu ikianza kuporomoka kwa mke wangu!
Lilikuwa jambo lililonisikitisha sana lakini sikuwa na jinsi.
Ufunguo wa mlango nilikuwa nimeushika mkononi. Nikamfungulia mlango. Alipokuwa anataka kutoka nikamuuliza tena:

“Umemueleza mama yako kuwa mimi ni mchawi?”
Lilikuwa swali la kitoto sana lakini mwenyewe sikujijua kwa vile yalikuwa yameshanifika.
“Ni siri yangu mimi na yeye,” mke wangu akaniambia huku akitoka pamoja na mtoto.
“Hata kama umemwambia kuwa mimi ni mchawi sidhani kama ataamini. Mimi nitakuja kumueleza ukweli halisi.”

“Ukweli halisi upi? Wa kutaka kumtoa kafara mtoto wetu?” Mke wangu akaniuliza kijeuri.
Hapo nikajikuta nimehamaki.

“Mke wangu naomba tuheshimiane, naona lugha yako kwa leo imebadilika sana!”
Mke wangu hakujibu kitu. Aliliweka begi lake chini akamuweka mtoto vizuri kisha akaliinua begi.
“Kama wewe unaondoka, nenda na ukweli kwamba tumekuwa tunasumbuliwa na wachawi wanaotaka kumchukua mtoto wetu lakini siyo kwenda kunivunjia heshima mbele ya mama,” nikamwambia huku nikiizuia sauti yangu kuonesha hasira.

Mke wangu hata hakunijali kamwe.
Alikuwa akitazama saa yake mkononi kama vile aliona dereva aliyemuita alikuwa akichelewa.
Mara tukamuona mlinzi akimfungulia geti dereva huyo aliyewasili.

Mke wangu alipomuona alishuka haraka kwenye baraza ya nyumba, akaelekea kwenye gari letu.
Dereva alikuja kunisalimia kisha akaenda kwenye banda la gari.

Kwa vile ufunguo wa gari hilo tunauacha ndani ya gari, alifungua mlango akajipakia na mke wangu naye alifungua mlango wa nyuma akajipakia na mwanawe.

1 Comment
  1. Hussein hassani says

    mweeeeeee

Leave A Reply