The House of Favourite Newspapers

Acha ujuha, dai risiti!

0

risitiSasa ninalazimika kudai risiti kwa kila huduma, maana mambo yamekuwa ndivyo sivyo kabisaaa. Yaani mambo yaliyokuwa bure zamani siku hizi watu wanadai malipo tena kwa kutangaza kabisa hadharani. Juzi tu nimesoma mdada mmoja msupastaa katangaza kuwa anaetaka kuwa mpenzi wake ajipange, hataki mapenzi na mtu ambaye akimuomba hela ya matumizi amwambie eti hana.

Haya mapenzi ya kidot kom mbona kizungumkuti? Mapenzi gani ya kupangiana masharti? Sasa kama ukiwa Juha unakubali masharti namna hiyo, kwanza ujue kabisa kuwa wewe kweli wakuja. Yaani asubuhi unaamka tu unasikia “Bebi leo nataka kula soseji na mayai ya kukaanga yenye mbogamboga ndani na kipande cha samaki, maziwa fresh na juisi, naomba alfu ishirini nimtume dada akanunue.” Unatoa.

Nusu saa baadaye “Bebi naona losheni yangu imeisha huwa natumia ile inaitwa D’Or naomba alfu stini nikanunue” Unatoa.

“Bebi nataka kwenda Mbagala kumsalimia dada naomba alfu hamsini za teksi na hela kidogo ya kumpa dada anaumwa, laki na ishirini zitasaidia” Unatoa.

Wakati yuko kwa dada anakupigia simu, “Bebi huku nimemkuta dada mmoja anauza madira mazuri, nimechukua matatu shilingi alfu stini naomba unitumie kwenye simu” Unatoa.

“Bebi nataka kurudi ile hela ya teksi haitoshi” Unatoa.

“Bebi napita hapa saluni kuosha nywele, usinitumie pesa ntamkopa tumlipe kesho bebi, shilingi elfu hamsini tu” Unajibu ‘Sawa’.

Akifika home anakwambia kachoka analala ila, “Bebi leo nitoe out nasikia kuna klabu mpya wenzangu wote wameshaenda kasoro mimi tu. Halafu sina hata nguo ya kuvaa tukienda huko ntakimbia hapo kwa Da Tunu ameleta nguo nzuri toka China japo anikopeshe tumlipe wiki ijayo au siyo bebi?” Unakubali.

Jioni mnatoka, kwa masharti kuwa teksi iwafuate tena ambayo ataagiza yeye, anakwambia “Bebi tupitie kwa Anko Kitime kwanza tule mishkaki ana mishkaki mizuri sana” Mnapitia mnanunua mishkaki kama thelathini hivi na chips. Kisha ndipo mnaelekea klabu.

Kufikia saa saba, laki tatu imefutika kwa vinywaji vyenu na vya rafiki zake, wewe mwenyewe umekunywa maji chupa ndogo mbili. Siku ya kwanza imeisha mnarudi kulala.

Mkiamka mzunguko unaanza,  aise dai risiti kwa kila kitu hapo, maana katika kila risiti kuna pasenteji inayobaki kwa serikali na katika hela ile ndiyo tunapeleka huduma kwa wananchi…!!!!!

Leave A Reply