The House of Favourite Newspapers

ACT Wazalendo Wameyasema Haya Kuhusu Rais Magufuli Kumteua Prof. Kitila Mkumbo

Leo asubuhi Rais John Pombe Magufuli amemteua Mshauri wa Chama chetu Prof. Kitila Mkumbo kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Chama cha ACT Wazalendo kimepokea kw mikono miwili taarifa juu ya uteuzi wa mshauri wa chama chetu Kwa sababu imeonyesha kuwa Rais ameona kuwa hata Watanzania walio kwenye Vyama vya Upinzani wana uwezo, weledi na uzalendo wa kutumikia nchi yetu.

Kwa nafasi hii ya Ukatibu Mkuu wa Wizara, ndugu Kitila hawezi kuendelea kuwa Mshauri wa Chama nafasi ambayo inamfanya kuhudhuria vikao vyote vya Chama ikiwemo Kamati Kuu. Ndugu Mkumbo ameandika barua ya kujiuzulu nafasi yake ya mshauri wa Chama na kubaki kuwa mwanachama wa kawaida tu. Nimeipokea barua yake na kumkubalia Kwa maslahi mapana ya nchi yetu.

ACT Wazalendo tunamshukuru ndugu Kitila Mkumbo kwa mchango wake katika uongozi wa Chama chetu kwa wakati wote ambao alikitumikia Chama chetu kama mshauri wa chama. Msimamo wa chama chetu ni utumishi wa kizalendo kwa Taifa utokanao na kila mwananchi, ndio msingi wa kaulimbiu yetu ya ‘Taifa Kwanza, Leo na Kesho’, hivyo basi tunamtakia kila la kheri ndugu Kitila katika utumishi wake kwa Taifa letu katika nafasi yake hii mpya.

Wizara Hii ni kubwa na muhimu Sana kwa nchi yetu. Maji ni tatizo moja kubwa ambalo wananchi wetu wanakumbana nalo na Kama Taifa hatujaweza kulimaliza.

Tunamtakia kila la kheri ndugu Mkumbo katika kuongeza nguvu kumaliza kero ya maji na kuhakikisha tunaimarisha Kilimo cha Umwagiliaji nchi nzima. Tunamsihi aanze na ajenda ya Mfuko wa Maji Vijijini na kuanzishwa Kwa Wakala wa Maji Vijijini utakaosimamia upatikanaji wa Maji Kwa wananchi wetu.

Kwa hatua hii, tunaona Rais ameamua kuunganisha nchi yetu Kwa kufanya kazi na watu wote bila kuwabagua Kwa itikadi zao za vyama. Watanzania ni wamoja na kauli za kuwagawa zinaumiza zaidi Taifa kuliko kuliweka pamoja. Tunaamini kuwa Rais Ana nia njema katika uteuzi huu na sisi tumempa baraka zote Mwanachama wetu mwanzilishi wa Chama kwenda kwenye nafasi ya juu zaidi ya utumishi wa umma. Tunaamini hatamwangusha Rais na muhimu zaidi hatawaangusha Watanzania.

Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama – ACT Wazalendo
Aprili 4, 2017
Dodoma.

=================================

Baada ya kuzungumza na waandishi wa habari leo, aliulizwa maswali mawili na waandishi wa habari ambapo aliyajibu.

Kwa namna moja ama nyingine chama kitaathirila vipi kwa kuguswa kwa Prof. Kitila?

Tutakuwa tumepoteza mtu ambae anatushauri katika chama, anatusaidia katika uendeshaji wa chama. Kutakuwa na changamoto katika uendeshaji wa chama lakini tumepewa vichwa ili viweze kufikiri ni namna gani ya kukabiliana na changamoto ambazo zitakuwa zinatokea, kwa hivyo tutaangalia ni namna gani ya kuzitatua changamoto hizo.

Hii siyo njia ya kuwafuta machozi ACT Wazalendo kutokana na kukosa nafasi ya kupeleka mgombea wa ubunge katika Bunge la Afrika mashariki?

Wengine wanaweza wakaona kama ni namna ya kuwafuta machozi ACT wazalendo. Wengine wanaweza kutafsiri kama ni njia ya kukinyong’onyeza chama kwa sababu Prof. Mkumbo anapoenda kuwa katibu mkuu hatojihusisha tena na chama. Atafanya kazi kulingana na kanuni na taratibu za watumishi wa umma. Lakini sisi yote hayo tunayaona kama mawazo na maoni ya watu.

Sisi tulijiuliza tulinde chama au tulinde nchi? Tukaona kwamba hatuwezi kuwanyima watanzania mtumishi mwenye uweledi kama Mkumbo kuwatumikia wananchi.

Comments are closed.