The House of Favourite Newspapers

Afande Sele: Kiki Haziji Kwa Staili Hiyo

0
Afande Sele.

SIYO sawa nikisema kila mmoja anamfahamu Afande Sele, kwa sababu wakati akitwaa ufalme wa mashairi pale kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar, mwaka 2004, teknolojia haikuwa katika levo tuliyonayo kwa sasa kiasi kwamba atambe kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.

Lakini ukweli ni kwamba, Seleman Msindi ambaye ndiye Afande Sele tunayemfahamu, ni mmoja kati ya wasanii wakongwe wenye kufahamika sana nchini kutokana na kazi kubwa na nzuri ambayo ameifanya kwa kipindi chote alichofanya Hip Hop.

 

Afande Sele anawakilisha Hip Hop ya ukweli iliyofanywa na marapa wa kizazi chao, ambao walizungumza kuhusu maisha ya jamii inayowazunguka. Kizazi hiki kinawakutanisha watu kama Sugu, Profesa Jay, Solo Thang, Balozi Dola Soul kwa kuwataja wachache. Nimefanya kazi kwa ukaribu na simba huyu wa Morogoro, ninaufahamu uwezo wake vizuri kichwani.

 

Unapofika wakati wa kuandika mashairi na kuyatengeneza ili yalete ujumbe kwa jamii, Afande Sele ni miongoni mwa wasanii wachache wanaoweza kukufumbua macho na kupata uelewa wa kutosha. Kuzitaja nyimbo zake ambazo amewahi kuzifanya ni kama kumkosea heshima, maana ana kazi nyingi na zinazofahamika sana, lakini kwa kukusaidia, ukitaka kujua uelewa wake, jaribu kusikiliza nyimbo zake za awali kabisa, kama Darubini Kali, aliyofanya na kundi lake la Watu Pori na Mtazamo, aliowashirikisha Prof Jay na Solo Thang.

 

Kuna wakati Afande Sele aligeuka kuwa ‘shamba’ la mapromota kuvuna hela, kwani alikuwa akigombewa kila siku asimame jukwaani. Kama hakutengeneza ‘empire’ yake wakati huo, ni lazima ajutie sana kwa sababu wenye kiswa
hili chao wanasema bahati haiji mara mbili.

 

Kinachonifanya niongee na Afande Sele hapa, badala ya kumpigia simu moja kwa moja, ni kwa heshima ya nafasi yake katika jamii baada ya kuwa ametoa maoni yake kutokana na hukumu ya msanii, Elizabeth Michael ‘Lulu’ kwenda jela miaka miwili kwa kosa la kumuua bila kukusudia, msanii mwenzake, Steven Kanumba. Katika ukurasa wake wa Facebook, Afande Sele aliandika maneno makali akimtuhumu marehemu Kanumba kama ndiye chanzo cha kuharibikiwa kwa maisha ya Lulu.

 

Alikumbushia jinsi binti huyo mdogo, alivyokutana naye usiku wa manane katika ukumbi mmoja wa burudani, wakati kimsingi kwa umri wake alistahili kuwa nyumbani amelala. Kutokana na ukali wake, nililazimika kwanza kujiri dhisha kama maneno haya kaandika ‘mtu pori’ mwenyewe, hivyo nikabofya namba zake na akanihakikishia kuwa ni yeye.

 

Kuthibitisha hivyo akaniongezea na maneno mengine kuwa jamii yetu ina tatizo la kuogopa kusema ukweli na kusingizia kuwa ‘marehemu hasemwi vibaya’! Miongoni mwa maneno ‘makali’ aliyoyaandika Afande Sele ni pamoja na kudai kuwa hakuweza kuhudhuria mazishi ya Kanumba, licha ya kuwa wakati wa kifo chake alikuwa jijini Dar es Salaam, kutokana na tabia yake hiyo ya kutembea na Lulu, wakati akijua kabisa kuwa alikuwa binti mdogo aliyehitaji malezi mema.

 

Ingawa nakubaliana naye kuhusu dhana ya kuogopa kusema ukweli kwa kuwa tu anayesemwa amefariki, lakini napingana naye kwa sababu maneno anayoyasema leo, yangekuwa na thamani zaidi kwa jamii kama angeyasema wakati ule kila mmoja akifahamu kuwa Kanumba alikuwa akijihusisha kimapenzi na Lulu.

 

Tatizo la watu wazima kutembea na wasichana wadogo halikuanza kwa Kanumba, bali lipo siku zote na hapa kwetu, ushahidi wa mazingira unaonesha linafanywa zaidi na wasanii kwa vile mashabiki wao wengi ni watoto wa shule.

 

Ni vipi mtu akifikiri kuwa Afande anatafuta kiki kusimama na kuongea miaka mitano baada ya mtu kufariki, wakati angeisaidia sana jamii kama angesema wakati ule, hata kama asingemtaja jina? Nimshauri Afande Sele kuwa kwake kioo cha jamii, kunampa uwanja mpana zaidi wa kuzungumza kitu chenye afya kwa watu wanaomzunguka. Huu ni wakati wa kufunguka ‘live’ ili watu wapate ujumbe mapema, kuliko kusubiri na kuongea baadaye maana kwa maisha ya kiki waliyonayo wasanii, ni rahisi watu kudhani anatafuta ‘nitoke vipi’.

Leave A Reply