The House of Favourite Newspapers

Afariki, Azikwa, Arudi Nyumbani

ARUSHA: Hali ya taharuki imewakumba wakazi wa Kijiji cha Leto-Mamsera, Kata ya Makidi, Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro kufuatia tukio la mkazi mmoja wa eneo hilo aliyekuwa amefariki dunia miezi miwili iliyopita kuibuka ghafla nyumbani kwake ikielezwa kuwa amefufuka.

 

Marehemu huyo aliyetajwa kwa jina la Richard David Tarimo (28) alifariki kifo cha kutatanisha Machi 30, mwaka huu baada kula nyama aliyoletewa na ndugu yake mmoja na baadaye kuanza kujisikia vibaya na kufariki dunia ghafla wakati akikimbizwa hospitalini kwa matibabu.

 

MSIKIE MKEWE

Mke wa marehemu aitwaye Mary Richard alieleza kuwa siku ya mazishi ya mumewe huyo kuliibuka jambo la kushangaza kutokana na udongo uliochimbwa kwenye kaburi hilo kutotosha baada ya kulifukia.

Kutokana na hali hiyo, padri aliyekuwa akiongoza misa ya kumwombea marehemu wakati wa mazishi hayo, alihoji kwa nini kaburi halijai udongo ndipo baadhi ya waombolezaji walipomjibu kuwa haliwezi kujaa kwa sababu marehemu amechukuliwa kimazingara.

 

Mke huyo alisema wiki mbili baada ya marehemu kuzikwa amekuwa akimtokea mkewe barabarani mara kwa mara na kumtaka afunge Novena kwa siku tisa kwani huko aliko anateseka.

Mary alisema kuwa Mei 20, mwaka huu marehemu mumewe aliibuka ghafla ‘laivu’ nyumbani kwake, jambo lililomshangaza na watu wengine kupigwa butwaa baada ya kudaiwa kufufuka.

 

“Niliamua kufunga Novena na baada ya kumaliza mfungo wa siku tisa ndipo ghafla akatokea mchungaji mmoja ambaye sikuwa namfahamu na kunieleza kuwa marehemu mume wako atarejea.

“Siku iliyofuata marehemu mume wangu aliibuka nyumbani kwangu lakini hakuwa anaongea chochote, alikuwa hajitambui ndipo watu wengi wakiwemo majirani walipojitokeza na kuanza kumshangaa huku wengine wakitaka kumgusa kuona kama kweli alikuwa ni binadamu wa kawaida,” alisema Mary.

 

TAHARUKI KWA WANANCHI

Hata hivyo, hali ya taharuki iliibuka nyumbani hapo baada ya wananchi kutaka atolewe nje wamwangalie, jambo lililowalazimu wachungaji walioitwa eneo hilo kwa ajili ya kumuombea, kuondoka na mume huyo wa mtu aliyefufuka ambapo alienda kuhifadhiwa nyumbani kwa wachungaji kwa ajili ya maombezi.

Mei 22 mwaka huu, ndipo Richard alipofika nyumbani hapo akiwa anaongea na kumuuliza mkewe hali ya watoto wake na kutaka abandikiwe maji ya kuoga.

 

Hata hivyo, mkewe alimpatia chakula na alipomaliza kula alipelekewa maji na kuoga na baadaye jioni majira ya saa 10 alitoweka nyumbani katika mazingira ya utata bila kuaga.

“Mei 22 mwaka huu, mume wangu alikuja na kuniuliza hali ya mtoto wake nilimjibu hajambo akaomba nimbandikie maji ya kuoga, nilimpatia chakula kwanza kisha akaenda kuoga na alipomaliza kuoga alivaa nguo zake akatoweka. Lakini baadaye nikaambiwa amerudi kule kwa wachungaji,’’ alisema Mary.

 

Mamia ya wakazi wa kijiji hicho waliokuwa wamefurika nyumbani kwa marehemu walilizingira kaburi la lake wakitaka lifukuliwe ili waangalie walichozika baada ya marehemu kuonekana akiwa hai ndani ya miezi miwili.

Hata hivyo, hadi mwandishi wetu anaondoka eneo la tukio, wananchi hao hawakufukua kaburi hilo kwa kile kilichoelezwa kuwa hadi wapate kibali cha mahakama.

 

BABA MZAZI ANASEMAJE?

Baba mzazi wa kijana aliyefufuka, mzee David Kimario ameshangazwa na kurejea kwa mwanaye nyumbani baada ya kudaiwa kufufuka kwani alikufa na wakamzika lakini alisema amefurahi kumpata tena kijana wake kwa sababu kifo chake kilikuwa cha utata na kilitokea ghafla.

“Ninachotaka kujua kwa sasa ni kwamba mwanangu alikuwa wapi na alikuwa akifanya nini na kwenye kaburi tulizika nini?” alihoji mzee Kimario.

Habari zilizotufikia wakati tunakwenda mitamboni zinasema Richard sasa hivi karejea nyumbani kwake na yupo vizuri.

 

MKUU WA WILAYA ANENA

Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Agness Hokororo akizungumzia suala hilo amesema kwamba mara baada ya kulisikia tukio hilo aliamua kutuma kamati yake ya ulinzi na usalama ya wilaya kwenda eneo hilo.

“Kamati ilifika na kukuta umati uliokuwa na shauku ya kumwona marehemu aliyefufuka,” alisema mkuu huyo wa wilaya.

 

DIWANI ALICHOKIONA

Naye Diwani wa Kata ya Makidi, Rombo Mkuu, kulipotokea tukio hilo, Simon Kinabo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na akasema baada ya kupata taarifa hizo alikwenda kuwajulia hali waliopatwa na jambo hilo.

“Nilikwenda kuijulia hali familia hiyo na kwa kweli hili tukio limetokea na limetushangaza wengi,” alisema Diwani Kinabo.

Stori: Joseph Ngirisho, Amani.

 

BREAKING: RPC Kinondoni Azungumzia Sakata la Mwalimu ST Florence

Comments are closed.