The House of Favourite Newspapers

Airtel, Maendeleo Benki Wazindua Huduma za Mikopo kwa Vikoba Kupitia Simu

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel, Beatrice Singano akibadilishana mkataba wa makubaliano na Mkurugenzi Mtendaji wa Maendeleo Benki, Ibrahim Mwangalaba.
Viongozi hao wakitiliana sahihi za mikataba yao.
Hafla hiyo na wanahabari ikiendelea
Askofu wa Kanisa la KKKT Dk. Alex Malasusa naye alipata fursa ya kuzungumza jambo.
Viongozi hao wakiwa katika picha ya pamoja baada ya hafla hiyo kuisha

KAMPUNI ya Simu za Mkononi ya Airtel kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo wamezindua huduma mpya ijulikanayo kama Timiza Vikoba yenye lengo la kuviwezesha vikundi vya vikoba nchini kutumia njia ya kisasa na salama itakayorahisisha ukusanyaji wa michango, kutoa mikopo na marejesho ya mikopo kwa urahisi.

Akizungumza na wanahabari wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Airtel, Beatrice Singano alisema huduma ya Airtel Money imekuwa ikiongoza kwa huduma za kibunifu na kisasa zaidi na leo imeona izindue ushirikiano wa kipekee na Benki ya Maendeleo kupitia huduma hiyo ili kuwawezesha wafanyabiashara katika vikundi vya Vikoba nchi nzima kufanya miamala yao ya kifedha kwa njia salama, uhakika na urahisi zaidi.

Aliongeza kuwa, huduma hiyo ya Timiza Vikoba inawawezesha wateja wa Airtel walio katika vikundi vya kuanzia watu 5 hadi 50 kupata huduma za kifedha saa 24 kwa muda wa siku saba za wiki kwa gharama nafuu kwa kupiga *150*60# na kisha kuingia kwenye menu ya Airtel Money na kusajili kikundi kisha kufungua akaunti ili kufaidika na huduma ya kutuma michango yao ya kila wiki, kuomba mikopo na kufanya marejesho ya mikopo wakiwa nyumbani au mahali popote pale kwa usalama na urahisi zaidi.

Huduma hii italeta uwazi na kuviwezesha vikundi vya vikoba kuhakiki taarifa zao za mikononi. Tunaamini huduma hii itachochea wafanyabiashara bila kujali maeneo walipo kujiunga kutengeneza vikundi vya vikoba ili kunufaika na kukuza biashara zao.

Timiza Vikoba ni uthibitisho wa dhamira yetu ya kutoa huduma za kibunifu zinazoendana na mahitaji ya wateja wetu hasa kuleta unafuu na urahisi kupitia huduma yetu ya kifedha,” alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Maendeleo Benki, Ibrahim Mwangalaba alisema:

Maendeleo Benki ni benki inayokuwa kwa kasi nchini kwa kutoa huduma mbalimbali yenye gharama nafuu, zenye urahisi wa kutumia ikiwemo ile ya akaunti za kuweka akiba, kutoa mikopo na huduma nyingine nyingi.”

Leo tunajisikia fahari kushirikiana na Airtel katika kuleta huduma za TimizaVikoba, huduma hii itasaidia wajasiriamali wadogo na wakati kuweza kuweka akiba zao kupitia simu zao za mkononi na pia huduma hii inawawezesha wateja wetu kukopa kupitia simu zao ili kufungua fursa mpya katika huduma za kifedha nchini.”

Mwangalaba alieleza kuwa kupanuka kwa huduma za kifedha na kuwafikia wale watumiaji wenye kipato cha chini ndio lengo halisi la Maendeleo Benki kwani mikakati yao waliojiwekea ni kuwafikia wateja hao kwa kuwapatia huduma nzuri na nafuu zinazoendana na utoaji wa mikopo kwa makundi.

Lengo letu Maendeleo Benki ni kuhakikisha tunaendelea kuleta na kurahisisha zaidi huduma za kifedha kwa kuweka mikakati kama hii itakayoleta tija katika maendeleo ya jamii nchini.

Mteja ukitumia huduma hii ya mikopo ya Timiza Vikoba unajitengenezea historia yako ya mkopo kidogo na baadae kujipatia mkopo mkubwa kwa masharti rahisi zaidi,” alimalizia Mwangalaba.

Comments are closed.