The House of Favourite Newspapers

Ajib, Kiiza wafuata nyayo za Ngoma

0

Hans Mloli, Dar es Salaam
SIMBA inaendeleza vipigo katika Ligi Kuu Bara na imani sasa imerejea kwa mashabiki wa klabu hiyo katika mbio za kusaka ubingwa lakini ghafla timu hiyo imejikuta ikiingia kwenye mkumbo mbaya wa kukosa penalti ambao awali ulikuwa ukionekana kuiathiri Yanga pekee.

Katika michezo miwili iliyopita, Simba imejikusanyia pointi sita na kuzidi kuikimbiza Yanga kileleni lakini ikajikuta ikikosa idadi ya mabao mengi baada ya kukosa penalti mbili walizozipata katika michezo hiyo.
Cha kushangaza ni kwamba hata Yanga imesakamwa na balaa hilo mfululizo kipindi cha nyuma, walikuwa wakijitahidi kubadili wapigaji penalti lakini bado wakawa wanakosa, kitu kinachoonekana ni sawa na Simba ambao tayari katika penalti hizo mbili, wamepiga wachezaji wawili tofauti na bado wakakosa.
Tangu kuanza kwa msimu huu, Simba imepata penalti tatu, katika hizo imepata moja na kukosa mbili. Awali Hamis Kiiza alifunga kwa penalti katika ushindi wa 2-1 dhidi ya JKT Ruvu, wakapata penalti nyingine walipoumana na Mgambo JKT, Kiiza akakosa tuta hilo katika mechi hiyo waliyoshinda 5-1.
Wekundu hao walipocheza dhidi ya Kagera Sugar wikiendi iliyopita, wakazawadiwa penalti nyingine, Ibrahim Ajib akapiga lakini akakosa.
Ikumbukwe kuwa katika mechi za ligi msimu huu, Yanga imezawadiwa penalti tano lakini imekosa tatu na kufanikiwa kupata mbili pekee. Donald Ngoma alikosa mbili, moja dhidi ya Prisons ambapo waliibuka kidedea kwa ushindi wa 3-0 na nyingine dhidi ya Toto African ingawa walishinda kwa mabao 4-1.
Thabani Kamusoko naye alishindwa kufunga penalti walipoumana na Azam, mwisho matokeo yakawa ni sare ya 1-1. Katika nusu fainali ya michuano ya Mapinduzi iliyomalizika Zanzibar Januari 13, mwaka huu, Yanga ilipofika kwenye matuta dhidi ya URA ya Uganda, Geofrey Mwashiuya na Malimi Busungu walikosa mikwaju na kuipa tiketi URA kuingia fainali.

Leave A Reply