The House of Favourite Newspapers

Al Hilal Mtakiona Jumapili…. Mabosi wa Yanga Wahamia Kambini Avic Town, Kigamboni

0
Wachezaji wa Yanga wakifanya yao.

KATIKA kuhakikisha morali na hamasa inaongezeka, baadhi ya viongozi wa Yanga wamechukua maamuzi ya kukaa karibu na wachezaji wao huko kambini Kijiji cha Avic Town, Kigamboni nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

 

Hiyo ni katika kuelekea mchezo wa marudiano wa hatua ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika watakaocheza dhidi ya Al Hilal huko nchini Sudan, Jumapili hii.

 

Timu hizo katika mchezo wa kwanza waliocheza Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar, walitoka sare ya bao 1-1.

 

Mmoja wa mabosi wa timu hiyo, ameliambia Championi Jumatano kuwa mabosi hao wamechukua maamuzi ya kukaa kambini hapo kwa lengo na kukaa pamoja na wachezaji na kikubwa ni kuongeza hamasa.

 

Bosi huyo alisema kingine ni kuwatengeneza kisaikolojia wachezaji hao kwa kuwapa matumaini ya kupambana uwanjani katika mchezo huo wa marudiano ili wapindue matokeo ugenini kwa ushindi wa aina yoyote, wafuzu makundi.

Aliongeza kuwa viongozi hao wanahudhuria program zote za mazoezi kuanzia juzi Jumatatu asubuhi ambao wachezaji wao walianza kwa mazoezi ya gym kabla ya jana kufanya ya kimbinu chini ya Kocha Mkuu Mtunisia, Nasreddine Nabi.

 

“Viongozi wamepania kwenda kupindua meza Sudan kwa kuwafunga Al Hilal, tayari wamewatanguliza wengine kwa ajili ya kwenda kupangua fitina na hujuma walizozipanga wapinzani wetu.

 

“Baadhi ya viongozi wapo kambini Avic Town ambako timu imeweka kambi huko tangu jana (Jumatatu) ambao wenyewe wapo karibu na wachezaji kwa lengo la kuwatengeneza kisaikolojia na kuwapa matumaini ya kupata matokeo mazuri ugenini.

 

“Katika mchezo uliopita tulifanikiwa kupata sare ya bao 1-1 nyumbani, lakini bado uongozi una matumaini makubwa ya kuwafunga Al Hilal kutokana na ubora wa kikosi chetu,” alisema bosi huyo.

 

Alipotafutwa Ofisa Habari wa timu hiyo, Ally Kamwe, kuzungumzia hilo simu yake ya mkononi iliita bila ya mafanikio ya kupokelewa.

 

Na alipotafutwa Nabi kuzungumzia hilo, alisema kuwa: “Kwa sasa sitaweza kuongea chochote kuhusiana na maandalizi ya timu yangu, kwani nikiongea nitakuwa ninatoa siri za kambi kwa wapinzani wangu.”

STORI: WILBERT MOLANDI NA MUSA MATEJA

YANGA WANAKWENDA KUPINDUA MEZA SUDAN, MGUNDA AULA SIMBA | SPORTS ZONE

Leave A Reply