Alikiba Nikipata Tuzo Nyingine Itapendeza Zaidi!

Staa wa Bongo, Ali Kiba.

 

HUKU Hamorapa akiwa chimbo anapanga atoke na kiki gani, bodaboda na mama ntilie wakibishana juu ya ukweli wa ndoa ya Dogo Janja na Irene Uwoya, Dk Louis Chika akijikusanyia kijiji kila anakopita na msemo wa ‘Itapendeza Zaidi’, Lulu akiyaanza maisha nyuma ya nondo gerezani, anaibuka Mmanyema mmoja na kuchafua hali ya hewa.

 

Mmanyema huyo si mwingine bali ni Alikiba ambaye hali hiyo ya hewa anaichafulia kwenye hoteli ya nyota tano ya Eko ambayo ni maarufu sana katika Kisiwa cha Victoria kilichopo jijini Lagos, Nigeria. Hoteli hiyo ipo umbali wa kilometa 29.9 kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Murtala Muhammed mpaka kwenye Mtaa wa 1415 Adetokunbo Ademola ilipotulia, ambapo umbali huo ni sawa na mtu kutumia saa moja na dakika 12, akiendesha gari kwa mwendo wa kawaida kabisa.

Ni katika ukumbi wa hoteli hiyo uitwao Convention Centre ambapo hivi karibuni Kiba alitangazwa kutwaa tuzo mbili. Ni Tuzo kubwa za Afrima (All Africa Music Awards), mbali na Kiba kwa Bongo, mwanamuziki wa kike Nandy naye amefanikiwa kuibuka na tuzo. Alikiba amevuna tuzo hizo kupitia ngoma yake ya Aje.

 

Tuzo hizo alizochukua ni katika vipengele vya Best Africa Collaboration kupitia wimbo wa Aje aliomshirikisha M.I na pia kwenye kipengele cha Best Artist or Group in Africa and RnB and Soul. Nandy ameshinda kwenye kipengele cha Best Female Artist In Eastern Africa Award.

 

Kwa upande wa Kiba, tuzo hizo alizochukua zinaendelea kuonesha mafanikio makubwa anayoyapata kwenye muziki wake. Katika hesabu za kawaida, kutokana na kupata tuzo hizo kupitia Wimbo wa
Aje ambao ni wimbo wa nyuma wa Seduce Me uliofanya vizuri zaidi, utagundua kuwa tuzo nyingine kwake zitapendeza zaidi! Si ajabu kwa mwaka unaoanza mkali huyu wa Bongo Fleva akaendelea kuorodheshwa kwenye tuzo nyingine nyingi kama MTV BASE, B.E.T. na AFRIMMA.

 

Nasema hivyo kwa sababu ukijaribu pia kuchunguza kwa mwaka huu utaona kwamba kwake umekuwa ni mwaka wa tuzo hasa za kimataifa. Ikumbukwe Alikiba aliufungua mwaka huu akibeba Tuzo ya MTV EMA ambayo aliipata baada ya kumshinda mpinzani wake wa kimataifa Wizkid ambaye awali alitangazwa mshindi wa tuzo hiyo kimakosa.

Katika muziki wetu hili ni jambo la kujivunia kuona mwanamuziki mkongwe kama Alikiba anakuwa mstari wa mbele kuhakikisha nchi yetuinavuna sifa kitaifa na kimataifa kupitia yeye. Mbali na sifa hizo lakini Alikiba anageuka kuwa kioo kwa wanamuziki wengine wenye kiu ya mafanikio kufika pale alipo au zaidi.

Kina Feza Kessy, Vee Money na Lady Jaydee ambao hawakufanikiwa kupata tuzo ya Afrima wanaweza pia wazidi kukomaa maana kuingia tu kwenye ushindani ni ushindi tosha. Lakini wana mengi ya kujifunza kuanzia namna ambavyo Kiba ameweza kuhakikisha kazi iliyompa mafanikio hayo aliyoyapata kuzidiwa ubora na kazi mpya ambayo anaitazamia kumpa mafanikio sasa na baadaye.

 

Kama taifa ni vyema kuwasapoti watu ambao wanajitoa kwenye kazi kwa ajili ya kuleta mafanikio ya kitaifa, maana kuwasapoti kwao ni sawa na kuwatia moyo wengine ambao wanainukia kufika huko walipo wao!

STORI: BONIFACE NGUMIJE | GLOBAL PUBLISHERS – IJUMAA

Toa comment