The House of Favourite Newspapers

Aliyemla Nyama mwanaye huyu hapa

0

aliyemla-nyama-mwanaye-huyu-hapa-902x1024Issa Mnally, UWAZI

DODOMA: Unyama! Hali bado si shwari kwenye Kitongoji cha Sekule, Kijiji cha Mongoroma, Kondoa mkoani hapa kufuatia Sisha Idi Mkirangi (35), kudaiwa kuwaua kwa kuwapiga marungu mkewe, Tabu Twaha na watoto wake, Kamilioni Festo na Hadija Amir kisha kumbanika motoni binti huyo na kula nyama yake, Uwazi limechimbua hadi eneo la mauaji.

Tukio hilo la kushangaza lilijiri Juni 14, mwaka huu kwenye kijiji hicho ambapo habari zinasema kuwa, sababu kubwa ya mtuhumiwa huyo kufanya mauaji hayo ni ugomvi wa kifamilia.

Akizungumza  na wanahabari baada ya kutokea kwa tukio hilo la ajabu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa kwanza alithibitisha kutokea kwa tukio hilo akisema ilikuwa asubuhi ya saa 2.

Alisema mtuhumiwa huyo alianza kwa kumuua mkewe, Tabu (35), mkazi wa Mtaa wa Ubondeni.

ACHOMA MWILI WA MTOTO, AMLA NYAMA

 “Alianza kumuua mama kisha akawageukia watoto ambao hawana hatia. Kibaya zaidi baada ya hapo alichukua mwili wa mtoto mmoja (Hadija) na kuutupia kwenye moto mkubwa aliokuwa ameuandaa na kuuchoma kama nyama. Baada ya kuona umeiva akaanza kukata mkono na kula,” alisema Kamanda Mambosasa.

AWAITA MAJIRANI

Kamanda huyo alisema baada ya hapo, mtuhumiwa huyo ambaye anashikiliwa, aliwakaribisha majirani zake ili wajumuike naye kula nyama ndipo waliposhtuka na kuanza kumshambulia kwa kipigo.

APELEKWA MIREMBE

Kamanda Mambosasa alisema kutokana na hali hiyo, wamelazimika kumpeleka mtuhumiwa huyo katika Hospitali ya Mirembe, Dodoma ili aweze kupimwa akili.

UWAZI ENEO LA TUKIO

Kufuatia taarifa hizo, mwishoni mwa wiki iliyopita, mwandishi wetu alifunga safari mpaka kijijini hapo kwa lengo la kuwasikia wanakijiji wanasemaje kuhusu tukio hilo na pia kushuhudia eneo la tukio.

Wakizungumza na gazeti hili, baadhi ya wanakijiji walisema siku moja kabla ya tukio hilo, mtuhumiwa aligombana na mwanamke huyo na kwenda kwa rafiki wa mwanaume, aitwaye Hassan Sadick kwa ajili ya kusaka suluhu.

“Walipofika kule, walisuluhishwa, ugomvi ukaisha. Lakini ugomvi wenyewe umebaki kuwa siri yao. Walilala pale, asubuhi alianza kuondoka mwanamke kurudi nyumbani na watoto, baadaye akafuata mwanaume.

“Lakini cha ajabu, alipofika, alimvamia mkewe na kummaliza, akafuatia mtoto Kamilioni kisha akamaliza na Hadija. Kama mlivyosikia, akachukua mwili wa Hadija na kuuchoma kisha kula nyama yake kama mishikaki, ajabu sana,” alisema jirani mmoja.

UWAZI LASHUHUDIA DAMU

 Uwazi lilioneshwa eneo ambalo mauaji hayo yalifanyika ambapo damu zilizokauka ziliashiria kuwepo kwa tukio hilo zito.

KUNI ZA MITI PORI

Baadhi ya majirani waliliambia gazeti hili kuwa, ilikuwa lazima Hadija aive kwa moto ule kwani kuni alizotumia mtuhumiwa huyo ni za miti ya porini ambayo kiasili zikichomwa huwa kama mkaa kwenye jiko.

ALIVYOUNGUA

Uwazi lilishuhudia picha za mtoto aliyebanikwa ambapo, aliungua sehemu ya katikati ya mwili kuanzia mabegani hadi kiunoni kiasi cha kubaki mifupa na mbavu huku mkono mmoja ukiwa umetoka na ndiyo ule ambao mtuhumiwa alianza kuula baada ya kuiva.

KUMBE SI WATOTO WAKE

Kwa mujibu wa mjumbe wa mtaa huo, Hussein Bakari, watoto hao si wa marehemu huyo na kwamba aliwakuta kwa mwanamke akiwa amezaa na wanaume wawili tofauti.

NI NDANI YA WIKI MBILI

“Ukiachilia mbali kusema si watoto wake, lakini pia huyu bwana alikuwa na mke na mtoto mmoja ambaye alimkimbia kutokana na kutishia kumuua kwa kumchinja.

“Baada ya hapo, aliishi peke yake kwa muda na baadaye akampata huyo marehemu. Tangu aanze kuishi na marehemu hii ni wiki ya pili imefika au inakaribia.”

KISA CHA MKE WA KWANZA

“Kisa cha mke wa kwanza kukimbia ni kwamba, siku moja mtoto wao alikuwa akicheza mpira peke yake. Kwa bahati mbaya alipiga mpira juu ukatua kwenye bati la nyumba, ndipo baba mtu akamshika na kutaka kumchinja.

“Sasa mke kuingilia kati, akamwacha mtoto akataka kumchinja mke, akakimbia na mtoto wake mpaka leo hawajarudi. Lakini yeye alifikishwa Kituo cha Polisi Kondoa, baadaye akaachiwa,” alisema mjumbe huyo.

MATUKIO YAKE YA AJABU

Mjumbe huyo aliendelea kusema: “Ukiacha hili la kuua safari hii, huyu bwana ana matukio mengi ya kushangaza. Aliwahi kusimama nje ya nyumba yake na kuwaambia wanaopita watoe pesa kama kodi jambo ambapo lilileta mzozo na watu wa kitongoji hiki.

“Lakini pia aliwapiga marufuku dada zake wawili wasikanyage nyumbani kwake, la sivyo wakikanyaga atawachinja. Kifupi kuchinjachinja au kuua kwake ilikuwa si jambo geni kumtoka kwenye kinywa chake.”

MAZISHI

Mazishi ya marehemu hao yalifanyika Ijumaa iliyopita kwenye Kijiji cha Duni, Kondoa ambako ni nyumbani kwa mdogo wa marehemu, Tabu aitwaye Zainabu.

Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi. Amina. 

Leave A Reply