The House of Favourite Newspapers

Aliyemuua Mumewe Ahukumiwa Jela Siku 1, Mwenyewe Ashangaa

0

MWANAMKE mmoja kutoka Kaunti ya Siaya ambaye ameingia kwenye headlines kwa kufungwa jela kwa siku moja baada ya kukutwa na kosa la kumuua mumewe, amezunguza kuhusu ndoa yake iliokumbwa na migogoro.

 

Truphena Ndonga Aswani alikubali mbele ya mahakama kwamba alimuua mumewe James Oyengo Obochi kwa kumkata kwa panga ambapo amesema kifungo cha siku moja jela alichofungwa ni muujiza wa ajabu ambao hakuwa ametarajia.

 

 

Aswani amesema alijua maisha yake yamefikia kikomo na huenda angehukumiwa kunyongwa au kifungo cha maisha jela. Akiwa kwenye mahojiano na The Standard, mjane huyo alisema alimpenda sana mumewe licha ya ugomvi na migororo ya kawaida katika ndoa.

 

 

Aliongeza kuwa hakukusudia kumuua mumewe lakini siku aliyotekeleza kitendo hicho, mumewe alifika nyumbani akiwa mlevi chakari na kuanza ugomvi. Marehemu alitaka kumshambulia kwa panga lakini alifanikiwa kumpokonya na kisha akamkata nayo ikiwa ni njia moja ya kujikinga.

 

Akitoa simulizi lake, Aswani alisema marehemu mumewe alifariki dunia kutokana na kuvuja damu kwa wingi, hata hivyo amesema ataiomba familia yake msamaha wakati ufaao kwa sababu kwa sasa anajua bado wana machungu naye.

 

 

“Nilimpenda sana mume wangu, alinifanya niitwe mama mwaka wa 2010, namheshimu kwa jambo hilo kwa sababu ndoa yangu ya kwanza sikujaliwa mtoto.

 

 

“Najua kifo chake bado kinawauma, najua wanaomboleza bado, sikukusudia kumuua mume wangu ila nilikuwa najikinga nisiuawe pia, ningependa kurudi kwangu lakini sio kwa sasa,” alisema Aswani.

 

 

Kwa sasa mama huyo anaishi nyumbani kwa kakake wa kambo mjini Webuye kwa sababu anahofia kurejea nyumbani kwake. Aswani alifungwa jela kwa siku moja baada ya mahakama kuamua kwamba kesi yake ilikuwa ya mauaji ya ukatili na tayari ameshatoka.

Leave A Reply