The House of Favourite Newspapers

Aliyewagonga Watu Watatu na Kusababisha Vifo vyao Afikishwa Mahakamani

0
Afisa Elimu Taaluma wilayani Kwimba mkoani Mwanza, Samwel Kulinga (44) amefikishwa mahakamani na kusomewa mashtaka manne likiwemo la kuendesha gari kwa mwendokasi, kuwagonga na kuwasababishia vifo watu watatu.
Amesomewa mashtaka hayo katika kesi ya trafiki namba 5383/2024, leo Januari 30, 2024, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kwimba, Dastan Ndeko.
Akisoma mashtaka hayo Wakili wa Serikali Frank Nchanila amesema shtaka lingine linalomkabili afisa elimu huyo ni kuendesha gari bila ya leseni katika barabara ya Umma.
Wakili Nchanila amesema waliofariki kwa kugongwa na afisa elimu huyo katika ajali iliyotokea Disemba 30,2023, eneo la Ilamba wilayani Kwimba mkoani humo ni mwendesha baiskeli, Shauri Masasi (62), Robert Matata (35), na Sara Faustine (43).
“Mshtakiwa ukiwa unaendesha gari binafsi yenye namba ya usajili T. 374 EEV Toyota Wish kwa mwendokasi uliwagonga watumiaji wengine watatu wa barabara na kuwasababishia vifo kinyume na Kifungu namba 40 (1) na 63 (2) (a) cha Sheria ya Usalama Barabarani sura ya 168 marejeo ya  mwaka 2002,” amesema Wakili Nchanila.
“Pia ulitenda kosa la kuendesha gari kwenye barabara ya Umma bila leseni kinyume na Kifungu namba 52 (a) na 63 (2) (e) cha Sheria ya Usalama Barabarani sura namba 168 marejeo ya mwaka 2002,” amesema.
Hakimu, Ndeko
Hata hivyo, mshtakiwa ameachiwa huru baada ya kukidhi masharti ya dhamana ambayo ni kuwa na mdhamini mmoja mwenye barua ya utambulisho kutoka kwa kiongozi wa wa Serikali za mitaa, mdhamini atakayesaini bondi ya mali isiyohamishika yenye thamani ya TSh 5 milioni na nakala ya Kitambulisho cha Taifa (Nida) ama Mpiga Kura.
Hakimu huyo, ameahirisha shauri hilo hadi Februari 19, 2024, litakapoitwa kwa ajili ya mshtakiwa kuanza kusomewa hoja za awali.
*Kutoka Dawati la Habari Polisi Mwanza*
Leave A Reply