visa

Amchinja Mkewe Mjamzito Siku ya Kupatana

ANTHONY ASENGA (33) mkazi wa Kijiji cha Mrere wilayani Rombo, anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za mauaji ya mkewe, Happiness Sianga, aliyekuwa na ujauzito unaokadiriwa kuwa wa miezi minane. Asenga anatuhumiwa kumuua mwanamke huyo kwa kutenganisha kiwiliwili na kichwa chake usiku wa kuamkia jana na kisha akajisalimisha katika kituo cha polisi cha Mashati.

 

Tukio hilo limeacha simanzi katika Kijiji hicho na Kamanda wa Polisi mkoani humo, Salum Hamduni, amesema wanamshikilia mtu huyo wakimhusisha na mauaji hayo.

 

“Ni kweli kuna tukio la mume kumuua mke wake huko Rombo. Tunamshikilia mtuhumiwa.   Uchunguzi unaendelea na utakapokamilika hatua nyingine za kisheria zitafuata,” alisema.

 

Akisimulia, mwenyekiti wa kitongoji cha Sembalo, kijiji cha Mrere, Faustina Urassa, alisema walikuta mwili wa marehemu ukiwa umefunikwa kitandani mithili ya mtu aliyelala na kwamba wanandoa hao waliwahi kugombana na kutengana kwa muda mrefu, na kwamba siku ambayo tukio limetokea ndiyo waliyopatana na kuanza kuishi tena pamoja.

 

“Tunashangaa tukio hili la kikatili kutokea siku ambayo wawili hawa walipatana na kuamua kurudiana, kwani baada ya kutengana, mume alifanya kila jitihada ili warudiane. Sasa hatujui ni nini kilichotokea hadi kufikia hatua ya kumchinja shingo kama kuku na kumuua.

 

“Baada ya kuachana na mumewe, mwanamke huyo aliondoka na mtoto wake wa miaka miwili na kwenda kuishi kwa wazazi wake, na hatukuwahi kujua ni nini kiliwasibu hadi kugombana. Waliporudiana hatukuwa tumejua ni nini pia kilitokea hadi kufikia hatua hiyo,” alisema Urassa.

 
Toa comment