The House of Favourite Newspapers

AMEUVUNJA MOYO WAKO NA KUKUACHA NA MAJONZI ? SOMA HAPA- 2

Related image

NAKUSHUKURU mpendwa msomaji wangu ambaye umetumia muda wako ‘kushea’ nami kuhusu mada hii kama tulivyoianza wiki iliyopita. Nimepokea meseji nyingi za kawaida na za WhatsApp kutoka kwa watu mbalimbali, wakieleza ni kwa namna gani mada hii imekuwa dawa kwenye mioyo yao.  Nilichokigundua ni kwamba wapo watu wengi wanaoteswa na mapenzi, wapo watu waliovunjika mioyo yao kutokana na mapenzi na kukata tamaa kabisa. Kama na wewe ni miongoni mwao, basi tambua kwamba unayo nafasi ya kusimama tena na kusonga mbele bila yeye.

Nimevutiwa zaidi na ushuhuda wa msomaji wangu mmoja ambaye ameomba jina lake lihifadhiwe. Yeye alikuwa na mke lakini mwaka 2014, mkewe alimbadilikia na kuanza kumletea vituko vingi mwisho akamtamkia kwamba hamtaki tena kwa sababu hana mvuto, hana fedha na haoni kama ana dalili za kufanikiwa.

Akaondoka na kumuacha na watoto wawili, akapitia kipindi kigumu sana, mwili ukadhoofika, kazi akafukuzwa kwa sababu ya stress, akawa ni mtu wa kumuomba sana Mungu. Hatimaye maombi yake yakajibiwa, akakutana na mwanamke mwingine, mzuri kuliko yule aliyemkimbia na hakika amemfuta machozi.

Hivi sasa wamefunga ndoa na ukimtazama, amenawiri vizuri, amepata kazi nyingine nzuri zaidi na maisha yanaendelea vizur  kabisa, huku mkewe mpya akiwapenda na kuwalea vizuri wanaye. Huu uwe ushahidi kwako unayelia leo kwamba inawezekana kabisa ukasimama tena hata kama unapitia kipindi kigumu kiasi gani kwa sababu ya kuumizwa na yule uliyempenda. Tunaendelea na mbinu za nini cha kufanya unapovunjwa moyo.

JITATHMINI

Mara nyingi inapotokea amekuacha, huwezi kupata muda wa kujitathmini mwenyewe na kujiuliza ni nini hasa kilichosababisha akakuacha. Wengi hubaki na majuto, wakiamini kwamba wameachwa kwa sababu hawajakamilika, hawana fedha, hawana mvuto na kadhalika.

Wakati mwingine, anayekuumiza anakuwa yeye ndiye mwenye makosa, tamaa zimemzidi nguvu na kumfanya akuone hauna maana tena. Usiyaamini maneno machafu na ya kuvunja moyo anayokuambia, jitathmini na kama kuna sehemu na wewe ulikuwa na makosa, basi ichukulie hiy kama changamoto itakayokusaidia katika uhusiano wako ujao.Related image

USIWE NA PAPARA

Jambo lingine la muhimu, ukiona uhusiano wako umevunjika, usikimbilie kuanzisha uhusiano mwingine. Acha papara, jipe muda ili moyo wako upone kwanza majeraha uliyoyapata, iache akili yako itulie.

Unapoharakisha kuingia  kwenye uhusiano mwingine kabla ya kujipa muda wa kutosha, unakuwa ni kama unatega bomu jingine kwenye moyo wako kwa sababu huyo uliyenaye, hutampenda kwa dhati na matokeo yake, utakaribisha maumivu mengine siku za baadaye.

MSHIRIKISHE MUNGU WAKO

Jambo jingine la muhimu, unapopitia kwenye kipindi kigumu kama hiki, ni kumshirikisha Mungu wako.

Bila kujali wewe unaamini katika dini ipi, muombe Mungu wako, mshirikishe kwenye matatizo yako na baada ya muda, utaona ule mzigo wote uliokuwa nao ndani ya moyo wako unapungua na taratibu utaanza kurudi kwenye hali yako ya kawaida.

Comments are closed.