The House of Favourite Newspapers

AMREF, USAID Wafanya Semina Ya Afya Shirikishi Ileje

0

hirika lisilo la kiserikali la AMREF ambalo linafanya kazi na TCDC kupitia ufadhili wa USAID kwenye Mradi wa USAID Afya Shirikishi kwa pamoja mnamo Novemba 9, 2023 walifanya semina elekezi ya Afya Shirikishi katika Halmashauri ya Wilaya ya Ileje Mkoa wa Songwe.

Semina hiyo ilihusisha madiwani wote wa kuchaguliwa pamoja na wale wa viti maalum ambapo suala kuu ilikuwa ni kupanga na kutekeleza mikakati ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa kifua kikuu ndani ya wilaya hiyo.

Akizungumza wakati wa uwasilishaji na uwezeshaji wa mada, Mratibu wa TB wa Mradi wa USAID Afya Shirikishi chini ya AMREF, Dkt. Malneste James amethibitisha kuwepo kwa wagonjwa 62 wa kifua kikuu ndani ya Wilaya ya Ileje kwa mwaka 2023 ambapo wagonjwa 31 wametambuliwa na wahudumu wa afya ngazi ya jamii (CHWS) ambao hupita nyumba kwa nyumba kutoa elimu na kubaini waathirika wa kifua kikuu huku wengine 31 wakiwa ni wale ambao wamehudhuria zahanati na hospitali na baada ya kupima wakabainika kuwa na maambukizi ya kifua kikuu.

Kwa upande wake, Mratibu wa TB Halmashauri ya Wilaya ya Ileje Dkt. Feliciana Mubi amethibitisha kuwa Wilaya ya Ileje pekee imegundua jumla ya wagonjwa 109 wa kifua kikuu kuanzia kipindi cha mwaka 2020-2023 huku akibainisha baadhi ya changamoto zinazokwamisha zoezi hilo kufanikiwa kwa asilimia kubwa ikiwemo ukosefu wa rasilimali fedha, idadi ndogo ya wahudumu ndani ya jamii pamoja na mila potofu miongoni mwa wananchi.

Kwa upande wao, Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje wakiongozwa na mwenyekiti wao, Ubatizo Songa wamebainisha mikakati mbalimbali ya namna ya kuunga mkono juhudi hizo zinazofanywa na mashirika hayo ambapo wameazimia kuwepo na uwezekano wa kupunguza gharama za X-Rays kutoka kiasi cha shilingi 20,000 hadi shilingi 10,000.

Pia halmashauri hiyo kupitia kwa madiwani wake, imepanga kuangalia uwezekano wa kutenga bajeti maalumu kwa ajili ya kusaidia mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Leave A Reply