The House of Favourite Newspapers

Amuacha mumewe kitandani, aenda kujinyonga kwao

RUVUMA: Mkazi wa Kijiji cha Nakayaya wilayani Tunduru mkoani Ruvuma, Awetu Makunula (44) mwishoni mwa wiki iliyopita amejinyonga hadi kufa kwa kutumia mtandio jirani na nyumbani kwa wazazi wake.

 

Mume wa marehemu Awetu, Salum Namtikwe, alisema usiku walilala wote na kabla ya tukio hilo mkewe aliamka saa 11 alfajiri na kumuaga kuwa anatoka nje kwa ajili ya kufagia nje ya nyumba yao.

Alisema baada ya kupewa maelezo hayo yeye aliendelea kulala lakini baadaye alishangaa kupata taarifa za mkewe kukutwa akiwa amejinyonga hadi kufa kwa kujining’iniza katika mti uliopo jirani na nyumbani kwa wazazi wake.

 

“Baada ya kupatiwa taarifa hizo niliamka na kwenda eneo la tukio na kumtambua marehemu mke wangu, baadaye tulitoa taarifa kwa viongozi wa serikali kwa ajili ya taratibu za kuuondoa mwili huo katika eneo hilo,” alisema.

Akisimulia maisha ya mkewe, Namtikwe alisema hajawahi kugombana naye lakini alikuwa mgonjwa wa homa za mara kwa mara licha ya kwamba siku aliyojinyonga hakulalamika kuumwa.

 

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, ASCP Gemin Mushy (pichani), alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kusema polisi inaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo cha kifo hicho.

Stori:Mwandishi Wetu, RISASI MCHANGANYIKO |JANUARI 02-04|2019

Comments are closed.