The House of Favourite Newspapers

Anakupiga Mzinga? Hii Inakuhusu!

0
love, family, finance, money and happiness concpet - smiling couple with money and piggybank ot table at home
love, family, finance, money and happiness concpet – smiling couple with money and piggybank ot table at home

U hali gani msomaji wangu wa safu hii ya Sindano za Mahaba. Mi mzima naendelea vyema na kazi, kwa wagonjwa niwaombee tu mtapona.

Leo nimeona nizungumzie juu ya tabia za baadhi ya watu walio katika uhusiano kupenda kuwapiga ‘mizinga’ wenzi wao, namaanisha kuomba pesa bila mpangilio. Tabia hii ipo zaidi kwa upande wa wanawake, ingawa ipo hata kwa wanaume kwani nao wameingia katika mkumbo huu.

Siku hizi imekuwa jambo la kawaida kwa baadhi ya wanawake hao, tena wanaonesha hadharani kabisa, utamsikia; “Ohh bwana wangu hapa hatoki! Nikimwambia tu ninashida ya kitu kikubwa ananipa, maisha yanaendelea.”

Si hivyo tu, wapo wanaume ambao ni kero kwa wapenzi wao, yaani wamegeuka wanaume kama mabinti kwa tabia zao za kutegemea kupewa kila kitu na wapenzi wao hata kama wanao uwezo wa kuvipata vitu hivyo kama wataji-shughu-lisha.

Unaweza kumsikia mwanaume akisema; “Aaah! Yule demu kazimika ile mbaya na mapigo yangu, kila ninachotaka ananipa anajua akinizingua namtosa, hadi mshahara wake akipata ananigawia. Yule ndiyo mwanamke wa kuwa naye bwana!”

Ninachotaka kusema leo ni kwamba, mapenzi ya kweli hayana uhusiano wowote na pesa, ukiona mpenzi wako anaweka pesa mbele na ukishindwa kumpatilizia anachokitaka anakasirika, jua penzi lake lina walakini, hakupendi bali anataka kukutumia kisha kukuacha.

Katika mapenzi hatukatai suala la kusaidiana, mpenzi wako akiwa na shida fulani akaomba umsaidie, kama unao uwezo msaidie na kama huna mueleze kwamba huna kisha muangalie jinsi gani mnaweza kusaidiana katika kutatua tatizo linalomkabili.

Itakuwa siyo busara kama utakuwa na tatizo lakini ukaona kwamba ukimweleza mpenzi wako ataona kwamba unamchuna. Wapenzi wanaopendana kwa dhati hawachunani bali wanasaidiana na hili ni kwa pande zote mbili.

Kinachokera ni kutoishiwa na matatizo na wakati mwingine unakuta kuchuna kwingine ni kwa mambo ya starehe. Yaani sasa hivi umemuomba mpenzi wako vocha, hajakaa vizuri umemtaka akija akuletee chipsi mayai, baadaye unataka akutoe ‘out’ bila kujali kwamba wakati huo mpenzi wako ana fedha au hana. Katika mazingira hayo unadhani mpenzi wako atashindwa kukuchoka?

Akikuacha kwa sababu hiyo utamlaumu nani? Fanya mabadiliko tafadhali. Kimsingi ukiwa na mpenzi mwenye tabia ya kutaka kukuomba pesa kila wakati tena katika matumizi mengine ambayo siyo ya msingi, vipengele vifuatavyo vinafaa sana kwako.

MFUNDISHE KUKUSAIDIA

Wanaume wengi wanalisahau jambo hili la kutokuwafundisha wapenzi wao wajibu wa kutoa! Utakuta kila kitu ananunua yeye, hata nauli ya daladala analipa, wakati mpenzi wake ana kazi yake. Ifike wakati kwa makusudi, mwanaume ampe majukumu ya kufanya mpenzi wake, hiyo itamsaidia mwanamke kujua namna pesa zinavyokuwa hazitoshi na akaweza kubana matumizi.

KUWA BAHILI

Wapo wanaume tangu wanatongoza wanakuwa ni wafujaji wakubwa wa pesa kwa kutoa ofa na zawadi kibao. Hii inaweza kumjengea imani mpenzi wako kuwa wewe unazo! Wakati akiwa anaamini hivyo, ukweli ulionao moyoni ni kwamba huna fedha za kutosha.

Unachotakiwa kufanya mapema ni kudhibiti matumizi yako hata kama pesa zinakuwepo. Ifahamike kuwa kutoa hakusababishi uhitaji, kadiri unavyotoa ndivyo unavyoongeza mahitaji. Weka maisha yako katikati usijidai tajiri kumbe ni kapuku tu.

MUWEKE WAZI

Mueleze wazi kuwa huna wakati mpenzi wako anakuomba na kamwe usijaribu kutoa ahadi ambazo huenda ukashindwa kuzitimiza. Usiwe mtu wa kutoa ahadi za uongo, mara nitakununulia hiki na kile. Mwanaume hatakiwi afahamike siku ana pesa au hana. Maana kuna wenzangu ambao siku za mishahara wanabadilisha hadi kutembea! Mwanamke akijua hilo naye ataongeza mizinga ili afaidi.

Ishi kawaida, kuwa mkweli kwake siku zote, utakapokuwa mkweli kwake atakuheshimu kwa uwazi wako. Siku zote zilingane, uwe una fedha au huna asijue, hilo litakusaidia kwa kiwango kikubwa sana katika maisha yako ya kimapenzi.

Elewa tu mapenzi si kukomoana, mapenzi ni kusaidiana. Jenga tabia ya kumsaidia mwenzako ili siku moja na wewe ukiwa na tatizo akusaidie. Kitu unachotakiwa kukiepuka ni kuwa tegemezi hadi unakuwa kero. Kumbuka kumpiga ‘mizinga’ mpenzi wako kila mara kunapunguza mapenzi.

Tuonane wiki ijayo kwa mada nyingine.

Leave A Reply