The House of Favourite Newspapers

Anaswa Akiuza Wasichana Kama Vitumbua

0

kamanda-Ramadhani-NganziMusoma:

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara linamshikilia Julita Lucas (30), mkazi wa kijiji cha Masinki Wilaya ya Serengeti kwa tuhuma za kufanya biashara haramu ya  kusafirisha binadamu anaowauza kuanzia Sh150,000 hadi Sh300,000.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Ramadhani Ng’anzi amesema Septemba 3, saa 9.00 alasiri, Lucas alikutwa akiwa na wasichana watano (majina yamehifadhiwa) aliokuwa amewaficha nyumbani kwake kwa lengo la kuwauza na wengine kuwaozesha kwa wanaume wenye kuhitaji.

Amesema baada ya mama huyo kuhojiwa alikiri kufanya biashara ya kuuza wasichana kwa bei ya kati ya Sh 150,000 hadi 300,000, kwa kuangalia ukubwa wa umbo na siyo umri.

“Baada ya kufanya mahojiano na wasichana hao wenye umri kati ya miaka 15 hadi 28, walisema wametokea katika kijiji cha Muhejangila Wilaya ya Karagwe Mkoa wa Kagera,” amesema.

Kamanda Ng’anzi  amesema polisi wanaendelea na uchunguzi dhidi ya mama huyo, ili kubaini mtandao wa biashara hiyo haramu ya binadamu.

 “Tunaendelea kumuhoji, tunataka kujua iwapo kituo cha mwisho cha biashara hiyo ni hapa ndani tu au ni hadi nje ya nchi , biashara hiyo ilianza lini na idadi ya wasichana waliokwisha uzwa na waliuzwa wapi,”

Kamanda Ng’anzi alisema baada ya upelelezi kukamilika, mama huyo atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.

Leave A Reply