The House of Favourite Newspapers

ANASWA UTEKAJI MTOTO!

WAKATI mfanyabi-ashara bilionea namba moja nchini, Mohammed Dewji ‘MO’ akifikisha siku ya tisa tangu atekwe na watu wasiojulikana, binti mmoja mkazi wa Kigogo Bonde la Jaba jijini Dar, Mariam Hassan, amenusurika kuuawa baada ya kunaswa akidaiwa kuhusika na utekaji wa mtoto Shadya Juma (2).

ENEO LA TUKIO

Tukio hilo lilijiri Jumatano wiki hii ambapo baadhi ya wakazi wa Manzese-Argentina jijini Dar walitaka kuchukua sheria mkononi baada ya binti huyo kudaiwa kuhusika na utekaji wa mtoto huyo kinyemela na kunaswa naye siku ya pili baada ya ndugu na jamaa kumsaka kila kona kwa kufanya matangazo sehemu mbalimbali ikiwemo misikitini.

Kwa mujibu wa mashuhuda, baada ya hofu kutanda juu ya taarifa za utekaji wa mtoto huyo, msako mkali ulifanyika tangu Jumanne asubuhi ndipo Jumatano, Mariam akanaswa ‘live’.

 

MARIAM AJITETEA

Baada ya kukamatwa, Mariam alijitetea kuwa, alimchukua mtoto huyo kwa nia njema hivyo muda huo alikuwa akimrudisha kwa wazazi wake. Hata hivyo, ilisemekana kwamba maelezo hayo hayakuwaingia akilini raia wenye hasira kali waliomkamata. Hivyo, walimtaiti na kumpeleka ofisi za Serikali ya Mtaa wa Ndugumbi- Mpakani, Manzese- Argentina wanapoishi wazazi wa mtoto huyo.

 

SERIKALI YA MTAA

Ilielezwa kuwa alipofikishwa Serikali ya mtaa, wazazi wa mtoto huyo aliyedaiwa kutekwa waliitwa ambapo familia nzima iliungana akiwemo mama mzazi, bibi na ndugu wengine ambao walikusanyana kwenye ofisi hiyo.

Wakati zoezi hilo likiendelea, gazeti hili lilifika ofisini hapo na kukuta sekeseke hilo. Katika utetezi wake, Mariam alisema kuwa, hakumchukua mtoto huyo kwa nia mbaya kwa kuwa mama yake anamfahamu na muda huo waliomkamata ndiyo alikuwa njiani akimrudisha.

 

MWENYEKITI AWEKA MAMBO SAWA

Wakiwa kwenye mjadala wa suala hilo, ndipo mwenyekiti wa mtaa huo, Salehe Kawambwa akajaribu kuweka mambo sawa na kuwatuliza wananchi walikuwa wamepaniki ambao walikuwa wakitaka kumpa kipondo Mariam. Wakati hayo yakiendelea, Mariam alikuwa akiendelea kumuomba msamaha mama wa mtoto huyo aliyejitambulisha kwa jina la Sharifa Mussa na kumwambia hakumchukua mtoto huyo kwa nia mbaya.

 

MARIAM ABANWA MASWALI

Wakati Mariam akiomba msamaha, mwenyekiti huyo alimuuliza kama alikuwa na nia gani na mtoto huyo na kwa nini hakuwataarifu wazazi wake kama alikuwa akitaka kumchukua? Baada ya kuulizwa hivyo, Mariam hakuwa na jibu zaidi ya kuendelea kuomba msamaha huku akijitahidi kuficha sura kwa aibu.

 

Mwenyekiti huyo alimuuliza swali lingine kuwa mtoto huyo alimlaza wapi ambapo Mariam alisema alilala naye nyumbani kwake, Kigogo-Bonde la Jaba ambapo amepanga. Mwenyekiti huyo alimgeukia mama wa mtoto huyo ambapo alimuuliza kama kuna hatua yoyote ambayo anataka ichukuliwe kuhusu kesi hiyo, ambapo mama huyo alisema kwa kuwa amempata mwanaye, basi anaomba akabidhiwe na hakutaka kesi.

 

WAKABIDHIWA MTOTO

Sharifa na ndugu zake walikabidhiwa mtoto huyo na kuondoka naye huku Mariam naye akiruhusiwa kuondoka kimyakimya huku akificha uso ambapo mwenyekiti aliwaomba wananchi wasimdhuru. Baada ya mwenyekiti huyo kumaliza zoezi hilo kwa amani, mwandishi wetu alizungumza na jirani wa mtoto huyo ambaye alisema alimuonea huruma mama wa mtoto huyo na wote hawakulala usiku kucha wakimsaka kutokana na taarifa zilizoenea kuwa alitekwa.

 

MAMA MTOTO SASA

Kwa upande wake, mama wa mtoto huyo alipoulizwa na gazeti hili kama alikuwa akifahamiana na Mariam alikana kumfahamu. “Simfahamu hata kidogo, lakini kwa kuwa nimempata mwanangu namshukuru Mungu,” alisema mama huyo.

 

WIMBI LA UTEKAJI

Hivi karibuni kumeibuka wimbi la utekaji na upoteaji wa watu nchini, jambo linalosababisha hofu miongoni mwa wanajamii.

STORI: Richard Bukos, Risasi Mchanganyiko

BREAKING: Ajali mbaya ilivyoua 5 leo Singida

Comments are closed.