The House of Favourite Newspapers

Apigwa, afa akidaiwa gauni la krismasi

0

IMG-20151206-WA0006Marehemu Eva Luhumba enzi za uhai wake.

Na Francis Godwin, IRINGA
DUNIA hii! Eva Luhumba (50), mkazi wa Ipogolo C, Iringa amefariki dunia baada ya kupigwa na stuli kichwani kisa ni gauni la Krismasi ambalo aliazima kwa jirani yake aliyetajwa kwa jina moja la Dori.

Kwa mujibu wa mashuhuda, Juni mwaka huu, marehemu alikwenda kwa Dori kuazima gauni la kuvaa mtoto wake kwenye sherehe ya Kipaimara lakini hakulirejesha. Ndipo Desemba 5, mwaka huu, Dori alimfuata Eva nyumbani kwake na kumtaka kumrudishia gauni hilo ili mwanae alivae kwenye Sikukuu ya Krismasi inayokuja (Desemba 25).

Hata hivyo, imeelezwa kuwa, Eva alilirudisha gauni hilo likiwa limechakaa ndipo ugomvi ulipoanza ambapo Dori alitaka jipya au alipwe shilingi 20,000.

“Dori alilipwa pesa hiyo, lakini akamtaka Eva amuongezee shilingi 10,000 kwa ajili ya usumbufu jambo ambalo lilipingwa na Eva.

“Walianza kurushiana maneno, kisha Dori akaenda kwake kuchukua stuli. Aliporudi alimpiga nayo kichwani Eva,” alisema shuhuda mmoja.

Jamila Luhumba ni mdogo wa marehemu Eva, yeye alisema baada ya Eva kupigwa stuli, alianguka. Akachukuliwa na kukimbizwa Hospitali ya Mkoa wa Iringa kwa matibabu ambako alilazwa kwa siku tatu.

“Wakati akiwa hospitali, mtuhumiwa alifikishwa polisi na kukaa kwa kwa siku mbili, akatoka kwa dhamana.

“Kitendo cha Dori kutoka kwa dhamana kiliwakwaza watoto wa marehemu, wakaenda kumlalamikia hivyo Dori akaenda polisi kushtaki, watoto wakawekwa ndani kwa madai walimfanyia vurugu.

“Baada ya Eva kutoka hospitali, mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Ipogolo C alituma wajumbe nyumbani kwa Eva akimtaka wakae kikao na kumaliza suala hilo. Dada akiwa nyumbani kwa mwenyekiti kwa ajili ya kikao, alianguka na baadaye kufariki dunia,” alisema Jamila.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Ipogolo C, Magdalena Mbala alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Alisema siku hiyo, Eva alifuatwa na kukutwa kwenye klabu cha pombe na kupewa ujumbe wa kuhitajika kwa mwenyekiti, lakini hakufika.

“Ilipofika saa mbili usiku, alifuatwa nyumbani na kukutwa anakula. Alipomaliza akaongozana na mama yake mzazi hadi nyumbani kwa mwenyekiti.

“Baada ya kufika aliulizwa sababu ya kupuuza wito wa serikali wa kumtaka kufika katika kikao ambapo aliomba msamaha. Lakini ghafla alionesha dalili za kuishiwa nguvu, akasogea miguuni mwa mama yake na kujilaza.

“Hali hiyo ilitafsiriwa kuwa, Eva hakupenda kumkuta mtuhumiwa. Lakini hali ilizidi kuwa mbaya, akatolewa nje ambapo alianza kutapika, ikalazimika kumkimbiza hospitali tena ambako alipoteza maisha akiwa katika matibabu,” alisema mjumbe huyo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhan Mungi amethibitisha kutokea kwa kifo hicho na kuwa mtuhumiwa amekamatwa na atafikishwa mahakamani.

Leave A Reply