The House of Favourite Newspapers

ASHAROSE MIGIRO AULA TENA UN

0
Balozi wa Tanzania Nchini Uingereza, Dk Asha-Rose Migiro.

MWANADIPLOMASIA ambaye pia ni Balozi wa Tanzania Nchini Uingereza, Dk Asha-Rose Migiro ameula tena katika Baraza la Umoja wa Mataifa (UN) baada ya kuteuliwa kuwa mmoja kati ya jopo la wataalam 18 watakaokuwa na kazi ya kuhakikisha wanatumia uzoefu wao kukabiliana na changamoto ya migogoro duniani kwa njia ya kidiplomasia.

 

 

Kwa mujibu wa habari zilizosambazwa jana kwenye vyombo vya habari, Dk Migiro aliteuliwa na Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres na hatua hiyo imeelezwa kuwa ni uthibitisho mwingine wa namna Tanzania ilivyo mshiriki muhimu katika kusaka amani duniani.

 

Jopo hilo ambalo linafahamika kama Bodi ya Ngazi ya Juu ya Ushauri Kuhusu Usuluhishi, limeundwa kwa kuzingatia usawa wa kijinsia na uwakilishi wa kikanda. Pia likizingatia historia ya wahusika katika masuala ya kidiplomasia na utatuaji wa migogoro.

 

 

Mbali na Dk Migiro aliyewahi pia kuwa Naibu Katibu Mkuu wa UN, wengine walioteuliwa ni aliyekuwa Mke wa Rais wa Msumbiji na baadaye akaolewa na Rais Nelson Mandela wa Afrika Kusini, Graca Machel, Rais Mstaafu wa Nigeria, Olesegun Obasanjo, Rais wa zamani wa Chile, Michelle Bachallete na Rais Mstaafu wa Finland, Tarja Halonen.

 

Pia wamo wanadiplomasia, mawaziri wa zamani, watu waliowahi kuongoza taasisi za kimataifa na wengine mashuhuri. Jopo hilo, pamoja na kazi nyingine, litakuwa na jukumu la kumshauri Katibu Mkuu wa UN kuhusu njia zinazopaswa kuzuia migogoro na kushiriki kutatua mizozo katika maeneo yanayokumbwa na hali hiyo.

Leave A Reply