The House of Favourite Newspapers

Asilimia 87% Huduma Za WCF Zinafanyika Kwa Njia Ya Mtandao

0
Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini wa Mfuko huo, Dkt. Abdulsalaam Omar, akizungumza na washiriki Juni 5, 2023

Akiongea kwenye mafunzo kwa maafisa Rasilimali Watu, Utawala na Usalama na Afya mahali Pa kazi kutoka taasisi za Binafsi na Umma, jijini Mwanza, Dkt. Omar alisema kutokana na matumizi hayo ya teknolojia ya kisasa katika kuwahudumia wadau, afisa wa WCF anaweza kuingia kwenye mtandao na kutoa huduma yoyote ya Mfuko wakati wowote na mahli popote pale ilimradi kuna mtandao (mawasiliano ya internet).

Wakati wa ufunguzi Dkt. Omar amesema “Dhumuni kubwa la mafunzo haya ni kuwapa uelewa kuhusu huduma zitolewazo na WCF, hatua za kufuata wakati wa kuwasilisha madai hususan kuwasilisha madai kwa njia ya mtandao (Online Notification System-ONS) inayopatikana kwenye portal.wcf.go.tz na masuala ya Usalama na Afya mahali pa kazi” Alifafanua

Katika kikao hicho, maeneo makubwa matatu yaliyojadiliwa ni pamoja na kukuza uelewa wa namna ya kudhibiti ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.

Dr. Omar ameongeza kuwa dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya sita chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuhakikisha Tanzania ina uchumi endelevu na kuwakwamua wananchi kutokana na umasikini kwa kutoa fursa mbalimbali za uwekezaji nchini.

Amesema ili kuendana na dhamira hiyo nzuri wadau wote kwa namna moja ama nyingine hawana budi kuongeza ubora wa bidhaa na huduma bali vilevile kuboresha mazingira ya uzalishaji ili kuepuka au kuzuia changamoto mbalimbali za ajali na magonjwa mahali pa kazi.

“Hivyo basi dhamira hii itawezekana pale ambapo tutakuwa na wafanyakazi wenye uhakika wa usalama wa afya zao katika maeneo yao ya kazi na endapo itatokea bahati mbaya wakapata madhara wakiwa wanafanya kazi basi wawe na kinga ya kipato na hata ikitokea mfanyakazi amefariki basi wategemezi wake waweze kupata fidia stahiki na kwa wakati.” Alisema.

Alisema ndio maana WCF itaendelea kutoa elimu hiyo kwa maafisa hao kutokana na umuhimu wao katika utoaji wa taarifa zinazohusiana na fidia kwa wafanyakazi pindi wanapokumbwa na changamoto za ajali au magonjwa yatokanayo na kazi.

“Ni jambo jema kuona wadau kutoka maeneo tofauti tofauti hususan maeneo ya migodi na ninafahamu juhudi kubwa ambazo zinafanyika huko katika kulinda afya na usalama wa wafanyakazi na pia ninafahamu wapo wanaotoka katika taasisi za umma wanaosimamia rasilimali watu, wote hawa tungependa wajue mambo ya msingi katika kudhibiti ajali na magonwja yatokanayo na kazi.” Alifafanua.

Aidha aliwakumbusha Maafisa Rasilimali Watu/Utumishi kujenga mahusiano mazuri baina ya ofisi zao na wafanyakazi katika kulinda haki zao ikiwa ni pamoja na kufahamu masuala yahusuyo fidia baada ya mfanyakazi kuumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi.

 Amesema awali mafunzo kama hayo yaliwahusisha Maafisa Rasilimali watu pekee “Hata hivyo tuliona ni muhimu kundi la Maafisa Usalama Mahali pa Kazi wakiungana na Maafisa Utumishi/ Utawala kwa pamoja waweze kupata elimu hii ili wajue namna ya kudhibiti ajali na magonjwa yatokanayo na kazi na jinsi ya kuwasilisha taarifa pindi matukio hayo ya ajali au ugonjwa yapotokea ili kuwasilisha taarifa kwenye Mfuko kwa wakati na hii itawezesha wafanyakazi kupata haki zao za msingi.” Amefafanua.

Ninyi ni daraja muhimu kati ya WCF na wafanyakazi wote wanaopata changamoto. Wewe ukiweza kujua taratibu zinazohitajika kuwasilisha madai WCF utasaidia kwa kiasi kikubwa hawa wafanyakazi kuweza kupata stahiki zao, alisema Dkt. Omar.

Aidha mmoja wa washiriki Bi. Izmina Ally Meneja wa Afya na Usalama kazini kampuni ya SBC, alisema amefurahishwa na jinsi WCF ilivyotoka kwenye matumizi ya analojia na kwenda kidigitali katika kuwasilisha madai ya wafanyakazi wanaoumia au kuugua kazini

“Hii itaturahishia sana katika kuwasilisha taarifa pindi panapotokea matukio hayo kwa mfanyakazi na itaondoa lawama ya kuchelewa kutoa taarifa na hili nitalifikisha kwenye utawala na wafanyakazi wote wajue.” amesema.

Leave A Reply