ASKARI WAFARIKI DUNIA WAKIFUKUZANA NA RAIA

ASKARI wa wanyama pori wa Hifadhi ya Taifa (Tanapa), Charles Ndakama na mwenzake, John Magwe wamefariki dunia baada ya kufukuzana na majangili wanaotumia mbinu ya kulisha mifuko kwenye Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa kujifanya wanalisha wanyama.  

Askari hao imeelezwa kwamba walifariki dunia hivi karibuni baada ya kukimbizana na wananchi hao kando ya Mto Mara kisha kuteleza na kujikuta wakitumbukia mtoni na maji yaliwaua wakati wakitetea rasilimali za taifa za Hifadhi za Mbuga ya Serengeti.

Mashuhuda walioomba majina yao kuhifadhiwa walisema askari hao baada ya kuangukia mtoni na kuzidiwa na maji walianza kuomba msaada wa kuokolewa na wananchi ambao hawakuwapa licha ya kushuhudiwa wakitapatapa kuokoa roho zao.

Hali hiyo ilitokana na kile kilichoelezwa na mashuhuda hao kuwa ni kuwapo na uhusiano mbaya kati ya jamii hiyo na askari wa wanyama pori kwa kutuhumiana mabaya pande zote mbili, raia wakidai kupigwa na kunyanyaswa na askari hao na askari wakidai wanavunja sheria.

“Wananchi wanadai wanaingiza mifugo mbugani baada ya maeneo ya kuchungia, kufugia, kulima, kuishi, na kujenga nyumba za makazi yao kukosekana kutokana na kuongezeka kwa watu katika vijiji vya Nyandage, Kegonga, Masanga, Kenyamsabi, Nyabirongo, Karakatonga, na Gibaso katika Kata za Nyanungu, Goron’ga na Kwihancha,” alisema shuhuda huyo.

Askari nao wanadai kwamba hicho ni kisingizio tu kwani kuna baadhi ya wananchi wanafanya ujangili mbugani baada ya kuvamia eneo linaloitwa Gibaso Open Area na kuishi ndani ya mita 500.

Miili ya askari hao, Charles ulifikishwa nyumbani kwao katika Kijiji cha Nyakasungwa, Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza wakati mwenzake, John Magwe ulifikishwa kwao katika Kijiji cha Nyansurumunti wilayani Serengeti

Mkoa wa Mara kwa mazishi na kupokelewa kwa vilio na ndugu, jamaa, marafiki, majirani na wazazi na kisha kuzikwa. Miili hiyo ilisindikizwa na wafanyakazi wenzao akiwamo Mkuu wa Kanda ya Kaskazini ya Hifadhi ya Mbuga ya Serengeti ya Taifa Wilaya ya Tarime, Lameck Matungwa aliyemfikisha kijijini marehemu Charles Ndakama.

Julai 16 mwaka huu Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Khamis Kigwangalla alitoa notisi ya siku 90 watu waliomo ndani ya mita 500 katika eneo lililotengwa kwa ajili ya uingizaji wa mapato ya vijiji vilivyopo jirani na hifadhi hiyo na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime wawe wamehama.

Wakati utekelezaji wa notisi ya Serikali ikisubiriwa, wenyeviti wa Serikali za vijiji vya Gibaso, Nyabirongo, Karakatonga, Nyandage, Kegonga, na Kenyamsabi kwa niaba ya wananchi wa vijiji vyao mefungua kesi namba 194/2018 Mahakama Kuu ya Tanzania Mwanza wakipinga kuondoka katika eneo hilo wakidai kuwa siyo la serikali bali ni lao.

Wamemshitaki Waziri Kigwangalla, Mkuu wa Mkoa Adam Malima, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na viongozi wa hifadhi.

Stori: IGENGA MTATIRO, Mara

Loading...

Toa comment