The House of Favourite Newspapers

ASKARI ZIMAMOTO WADAIWA ‘KUWAPIGA’ WACHIMBAJI

MBEYA: Baadhi ya askari wa Jeshi la Zimamoto mkoani Mbeya wanatuhumiwa ‘kupiga’ tozo kwa vitisho wakitumia silaha na kuwaweka mahabusu wachimbaji wadogo wa madini Wilaya ya Chunya na kutotoa stakabadhi kwa mujibu wa sheria.

 

Tuhuma hizo zilitolewa mapema wiki hii na wachimbaji hao mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mhandisi Maryprisca Mahundi katika Ukumbi wa Sapanjo Chunya mjini.

 

Aidan Mdimi na George Mtasha ni miongoni mwa wachimbaji wadogo ambao walipata kadhia hiyo.

“Mimi nimewahi kutozwa fedha zaidi ya shilingi milioni moja na maafisa wa Zimamoto Mbeya, nilipojaribu kuhoji walinikamata kisha kuniweka ndani wakidai nakaidi sheria. Pamoja na kulipa lakini sikupewa stakabadhi,” alisema Mdimi akimuomba mkuu huyo wa Mwilaya kumhakikishia ulinzi.

 

Kwa upande wake Mtasha ambaye ni Mwenyekiti wa Wachimbaji Wilaya ya Chunya alisema, awali alidaiwa na maafisa hao wa Zimamoto Mbeya kulipa shilingi milioni sita alipojitetea kuwa hana fedha hizo, akaambiwa atoe kiasi kilichopo kisha atapatiwa stakabadhi.

 

Hata hivyo, Mtasha alifanikiwa kutoa kiasi cha shilingi milioni moja na laki saba ambazo pia hakupewa stakabadhi. “Binafsi nimetumiwa ujumbe wa vitisho kutoka kwa mmoja wa maafisa wa Zimamoto wakinishinikiza kulipa fedha hizo bila hata kupatiwa elimu na ukaguzi,” alisema Mtasha.

 

Madai hayo yaliungwa mkono na Mwenyekiti wa Wachimbaji Mkoa wa Mbeya, Leonard Manyesha ambaye alisema alipokea kero nyingi kutoka kwa wachimbaji wakilalamikia Jeshi la Zimamoto kutoza tozo kinyume cha sheria, hali iliyolazimu kupeleka malalamiko ofisi ya Mkuu wa Wilaya.

 

Akitolea ufafanuzi malalamiko hayo ya wachimbaji, Mkuu wa Wilaya, Maryprisca Mahundi alisema ofisi yake ilipokea malalamiko kutoka kwa wachimbaji na alichukua hatua ya kuwaita maafisa hao, lakini hakuridhishwa na majibu yao.

 

Mahundi alisema hana mamlaka ya kumwajibisha mtumishi kutoka sekta nyingine hivyo suala hilo alilipeleka kwa Kamanda wa Zimamoto Mkoa wa Mbeya.

 

Abdallah Maundu ni Kamanda wa Zimamoto Mkoa wa Mbeya ambaye alikiri kupokea malalamiko kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Chunya na hatua za awali alifanya kikao na maafisa wake na kusimamisha zoezi hilo. Maundu alisema kitendo kilichofanywa na maafisa wake ni kinyume cha sheria kwani afisa yeyote anapofanya ukaguzi anapaswa kutoa elimu na tozo zozote hulipwa benki na si vinginevyo.

 

“Kwa sasa ninawasiliana na mwanasheria wa Jeshi la Zimamoto ili kama ikithibitika, maafisa hao watashitakiwa kijeshi na kupelekwa mahakamani kwa hatua zaidi,” alisema Maundu.

 

Kamanda Maundu alitoa rai kwa wananchi kupiga simu namba 114 endapo kuna dharura yoyote kuhusiana na Zimamoto na wasitozwe fedha mkononi kwani malipo yote ya Serikali hufanyika benki.

Pamoja na tozo za Zimamoto katika Wilaya ya Chunya, wilaya hiyo haina gari la Zimamoto hivyo kutegemea gari kutoka Mbeya, umbali wa zaidi ya kilometa 70.

Stori: EZEKIEL KAMANGA, IJUMAA

Comments are closed.