The House of Favourite Newspapers

Atekwa Akidaiwa Dawa za Kulevya Zenye Thamani ya shilingi milioni 50

0
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga Almachius Mchunguzi

WATU wanaodhaniwa kuwa vigogo wa mtandao wa dawa za kulevya wamemteka mshirika wao na kumzungusha maeneo mbalimbali ya Jiji la Tanga wakishinikiza kulipwa shilingi milioni 50 au arudishe mzigo wa dawa zinazodhaniwa kuwa za kulevya ambazo walimkabidhi mshirika waliyemteka.

Tukio la kutekwa kwa mtu huyo aliyetajwa kwa jina la Muki Kizinga lilitokea Februari 14 mwaka huu katika Halmashauri ya Jiji la Tanga na Kamanda wa Polisi Mkoani Tanga Almachius Mchunguzi amethibitisha tukio hilo

Katika taarifa yake kwa waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga Almachius Mchunguzi amesema baada ya polisi kupokea taarifa za kutekwa kwa Kizinga walianza uchunguzi na kufanikiwa kumkamata Khalid Mwarangi aliyedaiwa kumteka Kizinga.

Alisema, chanzo cha mtu huyo kutekwa ni watekaji kudai walipwe shilingi milioni 50 au kurudishiwa dawa zinazodhaniwa kuwa za kulevya ambazo walimkabidhi mtekwaji kuzisafirisha kwa lengo la kuuza.

Kamanda Mchunguzi alisema watekaji walikuwa wakimshinikiza Kizinga kuwarejeshea dawa zao au kuwalipa shilingi milioni 50 huku mtekwaji huyo akiwaeleza kuwa alikamatwa Ethiopia.

Kwa mujibu wa Kamanda Mchunguzi, Mwarangi ambaye ni mkazi wa Kimara Jijini Dar es Salaam anashikiliwa na polisi ambapo alikutwa akiwa na Kilogram 25 za dawa zinazodhaniwa kuwa ni za kulevya huku akiwa na hati mbili za kusafiria.

Aidha mtu aliyekuwa ametekwa naye amepatikana akiwa salama.

Leave A Reply