The House of Favourite Newspapers

Athari za Tofauti ya Kundi la Damu la Mama na Mtoto

KWA kawaida makundi ya damu (blood groups) kwa binadamu yapo manne ambayo ni; A, B, AB na O. Makundi haya pia yamegawanyika katika sehemu kuu mbili ziitwazo ‘rhesus factors’ au inatamkwa ‘rizasi fakta’. Rizasi fakta hizi zipo za aina mbili ambazo ni hasi (negative) na chanya (positive).

Kama mama atakuwa rizasi hasi na baba atakuwa rizasi chanya, basi mtoto akiwa tumboni ni lazima atarithi kundi la baba na atakuwa na rizasi chanya. Damu ya mtoto inaweza kupenya kwenda kwa mama wakati mtoto akiwa tumboni au wakati wa kuzaliwa hivyo husababisha madhara makubwa kwa mtoto.

 

Endapo damu ya mtoto itapenya kwenda kwa mama wakati wa ujauzito, itapita kwenye kondo la nyuma ‘placenta’. Wakati wa kujifungua damu ya mtoto inaweza kujipenyeza katika mishipa midogomidogo ya mama.

 

Damu ya mtoto ambayo ni rizasi chanya inapoingia kwa mama, husababisha mama atengeneze kinga ya mwili iitwayo Antibodi, dhidi ya damu ya mtoto au kundi la damu la mtoto hivyo husababisha hatari kubwa kwa mtoto kwani Antibodi za mama zitashambulia chembechembe nyekundu za damu ya mtoto hivyo husababisha madhara kwa mtoto ambayo kitaalam huitwa ‘Hemolytic Disease of the new Born’.

 

Ugonjwa huu huambatana na; Hydrops foetalis ambayo mtoto akiwa tumboni mwa mama huvimba au hujaa maji ‘Oedematous’ hivyo huweza kufia tumboni au huzaliwa njiti au kabla ya muda wake na kufariki dunia baada ya muda mfupi. Icterus Gravis Neonatorum, hali hii huambatana na; Mtoto kuzaliwa akiwa na manjano ‘Jundice’ kutokana na chembechembe nyingi nyekundu za damu kuharibiwa na Antibodi za mama. Mtoto hupata upugufu
mkubwa wa damu siku chache baada ya kuzaliwa.

 

Mtoto hupata athari za ubongo na kutokuwa na akili vizuri, hata ukuaji wake siyo mzuri. Ini la mtoto linaweza kushindwa kufanya kazi hivyo mtoto huishi kwa siku kadhaa na kufariki dunia.

 

NINI CHA KUFANYA? Tofauti hii ya kundi la damu la wazazi huleta madhara makubwa kwa watoto wanaozaliwa kwani wakinusurika kufariki dunia hupata ulemavu wa kudumu, aidha wa viungo kulegea au kukakamaa na wakati mwingine husumbuliwa na degedege la mara kwa mara kwa kuwa ile hali ya kuwa na manjano kali husababisha athari kwenye ubongo. Watoto wa aina hii ukuaji na maendeleo huwa duni.

 

Ulemavu huwa wa viungo na akili, hivyo wanapoishi muda mrefu huendelea kuwa wahitaji kwenye familia na jamii. Wazazi nao huathirika kisaikolojia na kiuchumi kwa kuwa hujikuta muda mwingi wanautumia kuuguza na kumtunza mtoto, mtoto huyu anapozaliwa na matatizo hukaa muda mrefu hospitali akiuguzwa kwenye taa yenye mwanga maalum huku akipata tiba nyingine.

 

Anapoendelea kukua hufanyiwa mazoezi ya viungo ili kumpunguzia maumivu na kuboresha misuli ya mwili. Inashauriwa kila mwanamke afahamu mapema kundi la damu yake hasa rizasi fakta na kupata ushauri kwa daktari.

 

Kwa ujauzito wa kwanza mtoto anaweza kuzaliwa bila matatizo endapo kama mama ni hasi na baba ni chanya, ila mara tu baada ya kujifungua mama anatakiwa apate sindano ya kinga ili isije kutokea tatizo katika ujauzito unaofuata. Kinga hutolewa pia hata baada ya mimba kutoka.

 

Ni muhimu kabla ya kufunga ndoa au kushirikiana tendo la kujamiiana kwa lengo la kupata watoto, watu wapime afya zao pamoja na kuangalia maradhi mengine, kundi au group la damu ni muhimu na endapo sasa hivi wewe ni mjamzito na upo katika tatizo hili, basi unashauriwa haraka umuone daktari bingwa wa matatizo ya uzazi akupe ushauri

Comments are closed.