The House of Favourite Newspapers

Aussems akesha akimfikiria Kagere

KOCHA Mkuu wa Simba, Mbelgiji, Patrick Aussems amesema kuwa wakati kikosi chake kikiendelea kujifua kwa ajili ya kupambana na Mtibwa Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu Bara hivi karibuni, alijikuta akitumia muda mwingi kumfikiria mshambuliaji wake, Mnyarwanda, Meddie Kagere.

 

Aussems alikumbwa na hali hiyo baada ya kupata taarifa kuwa Kagere aliumia katika mchezo wa kimataifa wa kuwania kufuzu kushiriki Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwaka 2022 huko nchini Qatar wakati alipokuwa akiitumikia nchi yake ya Rwanda dhidi ya Shelisheli, Septemba 5, mwaka huu.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Aussems alisema kuwa baada ya kupata taarifa hizo, aliamua kumtafuta Kagere ili kupata ukweli wake kwani kwa sasa ndiye mchezaji anayemtegemea katika kikosi chake upande wa washambuliaji.

 

“Baada ya kumtafuta aliweza kuniondoa wasiwasi kuwa alipata maumivu ya kawaida tu lakini yupo fiti na kunitaka nisiwe na wasiwasi.

 

“Kwa sasa Kagere ndiye mshambuliaji ninayemtegemea katika kikosi changu upande wa washambuliaji kutokana na John Bocco kuwa majeruhi lakini pia Mbrazili, Wilker Henrique da Silva bado hajawa fiti kutokana na kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kwa majeraha japokuwa ameishaanza kufanya mazoezi magumu,” alisema Aussems.

 

Hata hivyo, leo jioni Kagere atakuwa uwanjani akiitumikia kwa mara nyingine tena timu yake ya taifa dhidi ya Shelisheli katika mchezo wa marudiano utakaochezwa nchini Rwanda.

Katika mchezo wa kwanza, Rwanda iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 huku bao moja kati ya hayo likifungwa na Kagere.

Comments are closed.