Aveva, Kaburu Wafutiwa Dhamana na Kurejeshwa Mahabusu

Aliyekuwa Rais wa Klabu ya Simba, Evance Aveva na Godfery Nyange (Kaburu) wameshindwa kuachiwa kwa dhamana baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) , kukata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwaondolea kosa la utakatishaji fedha.

 

Washitakiwa hao waliondolewa kosa la utakatishaji fedha Septemba 19, 2019 baada ya mahakama hiyo kutowakuta na kesi ya kujibu katika kosa hilo isipokuwa mengine 7. Mshtakiwa mwengine katika kesi hiyo ni Zackaria Hanspope.

 

Hayo yamebainika leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Thomas Simba ambapo washitakiwa hao walitarajia wangetimiza masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh.Mil 30 kwa kila mmoja.

 

Wakili wa Serikali Mwandamizi Wankyo Simon amemueleza Hakimu Simba kuwa upande wa mashtaka umekata rufaa ya kupinga uamuzi uliotolewa Septemba 19, 2019 na mahakama hiyo.

Wankyo ameieleza mahakama hiyo kuwa upande wa mashtaka haujajiandaa kutoa hoja juu ya rufaa hiyo, hivyo ameomba kuahirishwa hadi siku nyengine.

 

Hata hivyo, Wakili wa utetezi Nehemia Nkoko ameieleza mahakama kuwa upande huo upo tayari kwa utetezi na kwamba wao walikuwa mahakamani hapo tangu asubuhi sambamba na mashahidi wao.

Nkoko ameeleza kuwa upande wa Jamhuri ulikuwa na notisi ya rufaani tangu asubuhi wangeweza kuwasilisha hoja zao.

 

Nkoko ameeleza kuwa upande wa Serikali haujapinga dhamana ya washtakiwa na kwamba ilishatolewa tangu jana.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili Hakimu Simba amesema kuwa misingi ya mahakama ni kusikiliza itakuwa haijautendea haki upande wa Jamhuri kwenye rufaa yao.

 

Amesema kuwa atasikiliza hoja za upande huo siku ya Septemba 23, 2019 na kwamba hajafuta dhamana ya washtakiwa. Aveva na wenzake wamerejeshwa mahabusu.


Loading...

Toa comment