Mama Abanwa Madai ya Ndoa ya Kiba Kuvunjika

DAR ES SALAAM: Wakati hali ikiwa si shwari kwenye mitandao ya kijamii kufuatia madai ya staa kunako Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’ kudaiwa kuvunjika kwa ndoa yake na Amina Khalef kutoka Mombasa, Kenya, mama mzazi wa staa huyo amebanwa.

 

TUJIUNGE NA VYANZO

Madai yaliyopo mitandaoni ni kuwa staa huyo aliyefunga ndoa Aprili, mwaka jana na kujaliwa kupata mtoto mmoja wa kiume amempa talaka tatu Amina baada ya kushindwa kupata muafaka juu ya ugomvi wao unaohusisha ndugu zake akiwemo na mama yake.

 

Vyanzo vingine vinadai Amina alikuwa akitaka ndugu wa mumewe huyo watoke ndani ya nyumba aliyokuwa akiishi naye maeneo ya Tabata-Chang’ombe jijini Dar, wakajitafutie maisha yao na wajitegemee, jambo ambalo lilizua taharuki na ugomvi mkubwa kati ya ndugu wa Kiba na Amina.

 

“Amina alidai ni vigumu kuishi na watu wengi vile ndani ya nyumba moja hata kama ni ghorofa na bado kuwe na amani, hivyo alimshauri Kiba awape mitaji wakajitegemee au awapangie nyumba nyingine,” kilisema chanzo.

IJUMAA KAZINI

Baada ya madai hayo kuenea kwa kasi huku kukiwa hakuna jibu kutoka kwa upande hata mmoja, Gazeti la Ijumaa lilifunga safari hadi nyumbani kwa mama yake Kiba maeneo ya Kariakoo jijini Dar ambapo lilimbana kwa kumuuliza madai yanayomhusisha yeye na mwanaye.

 

Ijumaa: Kuna madai kuwa, mama umehusika katika kuvunjika ndoa ya mwanao Kiba na Amina, kuna ukweli kiasi hapa?

Mama Kiba: (Huku akicheka), unajua sipendi hayo mambo ya mitandaoni na wala sitakagi kabisa kuonekana kwenye vyombo vya habari. Si unaona maisha yangu yenyewe ni ya Uswahilini? Sasa huko kwenye ma-TV nikatafuate nini?

 

Ijumaa: Lakini inadaiwa wewe ndiyo chanzo cha ndoa kuvunjika, je, hili likoje?

Mama Kiba: Ali (Kiba) kama ameachana na mkewe ninyi haiwahusu kabisa, halafu mimi siyo msemaji wa familia yake, mtafuteni yeye mwenyewe (Kiba) ndiyo mumuulize hayo maswali yenu, naamini atawajibu vizuri kwa sababu yeye ndiye staa na huwa anashinda sana mitandaoni kuliko mimi.

 

Ijumaa: Ukweli upo wapi sasa mama, Kiba ameachana na mkewe au yupo naye, na ni kweli anaishi na ndugu wengi kama isemavyo mitandao?

Mama Kiba: Naomba muondoke, siku nyingine mkihitaji kula ugali karibuni nitawapikia, lakini siyo kuja kuniuliza mambo ya Ali na familia yake. (alijigeuza nyuma na mbele kwa kutaka waandishi wamuache).

 

ALIKIBA AIBULIWA

Gazeti hili lilimtafuta Kiba kwa njia ya simu ambapo alipokea na baada ya kuulizwa maswali alionesha kukwepakwepa.

Ijumaa: Kiba mambo vipi?

Kiba: Safi tu!

 

Ijumaa: Unazungumza na mwandishi kutoka Global, Kiba kuna madai yanayoeenea kwa kasi kuwa ndoa yako imevunjika na sababu inaelezwa kuwa ni baada ya Amina kukataa kuishi nyumba ambayo imejaa ndugu zako wengi, unazungumziaje hilo?

Kiba: Kwanza nitajuaje kama kweli ninazungumza na mwandishi wa Global?

Ijumaa: Ondoa shaka mimi ni mwandishi wa Global, unazungumziaje madai haya?

Kiba: Sipo tayari kuzungumzia hilo suala. (Akakata simu).

Stori: MEMORISE RICHARD NA IRENE MARANGO, Ijumaa


Loading...

Toa comment